Pierre-Emerick Aubameyang, Andre Ayew, Riyad Mahrez, Sadio Mane au Yaya Toure, mmoja wao leo atatawazwa mshindi wa Tuzo ya BBC ya Mwanakandanda Bora wa Mwaka.
Mashabiki kutoka kila pembe ya dunia walimpigia kura mchezaji waliyetaka atunukiwe tuzo hii mwaka 2016.
Orodha hii ya wachezaji itapunguzwa kutoka watano hadi watatu, bila kufuata utaratibu wowote, moja kwa moja katika kipindi cha Sport Today cha idhaa ya BBC World Service na katika tovuti mwendo wa saa 15:40 GMT (saa moja kasoro dakika ishirini Afrika Mashariki).
Na mshindi atatangazwa moja kwa moja katika runinga na redio ya BBC Focus on Africa na mtandaoni saa 17:45 GMT (saa tatu kasorobo Afrika Mashariki).
Mshambuliaji wa Borussia Dortmund na Gabon Aubameyang anashindania tuzo hii kwa mwaka wan ne mtawalia, naye kiungo mshambuliaji wa West Ham na Ghana Andre Ayew - mshindi wa mwaka 2011 - naye pia anashindania kwa mara ya nne.
Mshambuliaji wa Leicester na Algeria Mahrez ndiye mchezaji pekee ambaye hajawahi kuteuliwa kushindania tuzo hii awali.
Mshambuliaji wa Liverpool na Senegal Mane aliteuliwa kushindania tuzo hii mara ya kwanza mwaka jana.
Kiungo wa kati wa Manchester City na Ivory Coast, YayaToure, ameshindania tuzo hii kwa miaka minane mtawalia na ameshinda mara mbili.
Aubameyang, 27, amefana sana mwaka 2016, ambapo amefunga mabao 30 akichezea Dortmund.
Aliibuka Mwafrika wa kwanza kutawazwa mchezaji bora wa mwaka Bundesliga, na raia wa kwanza wa Gabonese kutawazwa Mchezaji Bora wa Mwaka wa Shirikisho la Soka Barani Afrika na pia alikuwa kwenye orodha ya wachezaji walioteuliwa kushindania tuzo ya Ballon d'Or ya mwaka 2016.
Mwezi Agosti, West Ham walivunja rekodi yao ya ununuzi wa wachezaji na kumnunua Ayew, ambapo walitoa £20.5m kwa Swansea, ishara ya uchezaji wake bora mwaka 2016.
Uchezaji wa mwanasoka huyu wa miaka 26 ni wa kuridhisha, amefunga mabao 12 katika mechi 35, na alijizolea tuzo ya mchezaji mpya bora wa mwaka Swansea mwisho wa msimu mwezi Mei.
Mchezaji mwingine wa Ligi Kuu ya Uingereza, Mahrez alijivunia ufanisi mkubwa na alisaidia Leicester - ambao uwezekano wao kushinda ligi ulikuwa 5,000-1 - kushinda taji lao la kwanza ligini.
Mahrez, 25, alifunga mabao 17 ligini na alitawazwa Mchezaji Bora wa mwaka Chaguo la Wachezaji - Mwafrika wa kwanza kushinda tuzo hiyo. Aidha, aling'aa sana na kusaidia Algeria kufuzu kwa michuano ya Kombe la Taifa Bingwa Afrika mwaka 2017.
Mane, 24, aliibuka mchezaji ghali zaidi Mwafrika katika historia alipojiunga na Liverpool majira ya joto kwa £34m.
Amechangia sana uchezaji Anfield, ambapo amewafungia mabao saba katika mechi 15. Kabla ya kuhama kwake, alifunga mabao manane ligini mwaka huu akichezea Southampton, yakiwemo mabao matatu mechi moja dhidi ya mabingwa wa wakati huo Manchester City.
Toure alijishindia kombe jingine mwaka 2016 - lake la 17 katika uchezaji wake - aliposhinda Kombe la Ligi Uingereza akiwa na Manchester City, ambapo alifunga mkwaju wa penalty uliowawezesha kuwashinda Liverpool kwenye matuta fainali.
Huu ulikuwa mwaka ambao mchezaji huyo wa miaka 33 alistaafu soka ya kimataifa.
Lakini ametangaza kwamba hajafifia, na amerejea kucheza tena kwa ustadi Manchester City.
No comments:
Post a Comment