Watu sita wameuawa baada ya watu wenye silaha kushambulia mtaa mmoja mjini Mandera, kaskazini mashariki mwa Kenya.
Taarifa zinasema washambuliaji hao walivamia eneo lenye nyumba za makazi Bulla usiku wa manane.
Gavana wa jimbo la Mandera Ali Roba ameandika kwenye Twitter kwamba watu 6 wameuawa na mmoja kujeruhiwa.
Amesema watu 27 kati ya 33 waliokuwa kwenye ploti hiyo wameokolewa na maafisa wa usalama.
Kituo kimoja cha redio kinachohusishwa na kundi la al-Shabab kimesema wanamgambo hao ndio waliotekeleza shambulio hilo.
Gazeti la Daily Nation limeripoti kuwa watu walioshambuliwa walikuwa "watu wa kutoka maeneo mengine".
Gazeti la Standard nalo linasema walioshambuliwa walirusha guruneti kwanza na kisha wakaingia ndani na kufyatulia risasi waliokuwemo.
Bw Roba alisema dalili zote zinaashiria wavamizi hao walikuwa wa kundi la al-Shabab.
Eneo la Mandera limekuwa likishambuliwa mara kwa mara na wapiganaji wa al-Shabaab kutoka Somalia.
Kenya ilipeleka vikosi vyake vya jeshi nchini Somalia mwaka wa 2011 ikitaka kuzima mashambulizi ya mara kwa mara na kuisaidia serikali inayoungwa mkono na Umoja wa Mataifa.
Kundi la al-Shabab mara kwa mara hutekeleza mashambulio nchini Kenya ikiwemo mauaji ya watu 67 katika maduka ya Westgate mjini Nairobi mwaka wa 2013.
Mwezi Juni mwaka huu, wanamgambo wa kundi hilo walishambulia gari ya polisi aina ya Land Cruiser kilomita chache kutoka mji wa Mandera, na kuua maafisa watano wa polisi.
Mwaka uliopita al-Shabab walitekeleza mashambulizi katika chuo kikuu cha Garissa na kusababisha vifo vya wanafunzi 148
No comments:
Post a Comment