Mkurugenzi wa Uchaguzi wa tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), Bw. Kailima Ramadhani
Hussein
Makame, NEC
TUME ya Taifa ya Uchaguzi imeandaa programu ya
kutoa elimu ya mpiga kura katika vyuo vikuu nchini ili kutoa fursa kwa wanavyuo
kufahamu taratibu na Sheria zinazoongoza uchaguzi.
Hayo yamesemwa na Mkurugenzi wa Uchaguzi wa tume
hiyo Bw. Kailima Ramadhani, wakati akitoa tathmini ya utekelezaji wa mkakati wa
kutoa elimu ya mpiga kura nchini juzi jijini Dar es Salaam jijini.
Alisema program hiyo itaanza kwa kutoa elimu hiyo
kwenye Chuo Kikuu cha Dodoma, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na baadaye kutoa
elimu hiyo kwenye vyuo vingine nchini.
Mkurugenzi Kailima alieleza programu hiyo
kufafanua mikakati ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi kuhakikisha kuwa inatoa elimu
ya mpiga kura kwa makundi mbalimbali nchini ambayo kwa sasa inatolewa kwa
wanafunzi wa shule za Sekondari nchini.
“Lakini niseme
vyuo vikuu hatujavisahau kwa sababu tuna program hivi sasa kwamba tumepanga
tutakapokwenda vyuo vikuu, tutakwenda Chuo Kikuu cha Dodoma na chuo kingine”
alisema Bw. Kailima na kuongeza kuwa:
“Lakini tuna mpango wa kwenda Chuo Kikuu cha Dar
es Salaam na vyuo vingine vyote tuzungumze nao, labda niseme hapa kwamba
hatwendi kuzungumza kuhusu uhalali wa katiba au sheria zilizopo”
“Tunakwenda kuzungumza katiba ya sasa inasemaje
kuhusu taratibu za uchaguzi na utaratibu mzima na mfumo wake ukoje, tunakwenda
kuzungumza Sheria za sasa za Uchaguzi.”
Bw. Kailima aliweka wazi kuwa asingependa mikutano
hiyo na vyuo vikuu kujadili kuhusu katiba bali kuzungumzia Sheria zinazoiongoza
tume kusimamia na kuratibu uchaguzi.
“Wewe ukiwa na hoja yako ya katiba sio hii, hiyo
ina jukwaa lingine watakuja wenye jukwaa lao kuzungumzia suala hilo lakini sisi
tunakuja kukwambia Sheria inasema Tume isimamie na kuratibu uandikishaji wa
wapiga kura kwa ajili ya uchaguzi wa Rais na wabunge kwa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania” alisema.
Alieleza kuwa Tume iliona umuhimu wa kuanza kutoa
elimu hiyo kwa ngazi ya sekondari ili kuwawezesha wanafunzi wa ngazi hiyo
kupata elimu ya mpiga kura mapema na kuepusha vurugu zinazotokana na kukosekana
kwa uelewa wa taratibu za uchaguzi.
“Unajua
haya mambo kama hamyazungumzi mapema ndio baadaye mnakuja kuyaona ni mageni,
yanaleta vurugu watu wanakatana mapanga lakini ikiwa ni kitu cha kawaida na
kinazunguzika vurugu zinakwisha” alifafanua Bw. Kailima.
Aliongeza kuwa wanafunzi wa shule za sekondari
ndio wagombea wa Urais na ubunge watarajiwa na ni wenyeviti, makatibu na wajumbe
wa vyama vya siasa watarajiwa na wakipata elimu mapema itawajenga kujua Sheria
ya Uchaguzi.
“Yule wa chuo kikuu tayari ni mjumbe wa chama
fulani, mwingine tayari ni mgombea, ueleweshaji wake utakuwa sio mgumu kuliko
yule wa shule ya sekondari” alisema.
Tume ya Taifa ya Uchaguzi mbali na kutoa elimu ya
mpiga kura kwa wanafunzi wa shule za Sekondari nchini, imepanga kuanzisha klabu
za uchaguzi katika shule hizo ili kukuza uelewa wa masuala mbalimbali ya
uchaguzi kwa wanafunzi wa ngazi hiyo.
Sanjari na kutoa elimu hiyo kwa shule za
sekondari, NEC pia inashiriki katika maonesho na mikutano mbalimbali nchini ili
kukutana na wananchi ana kwa ana na kuwapa elimu hiyo.
No comments:
Post a Comment