Na Hussein Makame, NEC
TUME ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imesema itafikisha
Elimu ya Mpiga Kura mpaka katika ngazi ya vijiji ili kuhakikisha wananachi wanaoishi vijijini wanapata elimu hiyo.
Hayo yamesemwa na Mkurugenzi wa Uchaguzi wa NEC
Bw. Kailima Ramadhani wakati akitoa Elimu ya Mpiga kura kupitia kipindi cha Hot
Mix cha televisheni ya Afrika Mashariki (EATV) juzi usiku.
Bw. Kailima alikuwa akijibu swali la mtazamaji wa
kipindi hicho aliyetambulika kwa jina moja la Jumanne, aliyeiomba Tume iwe na
wafanyakazi wengi kwani Elimu ya Mpiga kura inahitaji kufika hadi vijijini.
Msikilizaji huyo alisema Elimu hiyo ni muhimu
kwani hata mwananchi wa kijijini anaihitaji kwa kuwa anahusika katika kuchagua
viongozi kwenye chaguzi mbalimbali nchini.
Akijibu swali la mtazamaji huyo, Bw. Kailima
alisema moja ya mikakati ya NEC kuwafikia wapiga kura kwa sasa, ni kuwatumia
wenyeviti wa vijiji na tayari imeshaandika barua Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa
na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) kuiomba iiwezeshe Tume kutekeleza hilo.
Alisema Tume imeiomba TAMISEMI iipatie ratiba za
mikutano ya kamati za halmashauri za mikoa, Wilaya na kamati za maendeleo za
kata ambazo wajumbe wake ni wenyeviti wa
mikutano mikuu ya vijiji ambao ni wenyeviti wa vijiji.
“Kamati ya Halmashauri ya mkoa inakusanya watu wengi
pale kwenye mkoa, tunataka tukawaelimishe pale....Katika mkutano mkuu wa kijiji
mjumbe wake ni kila mwananchi mwenye umri wa miaka 18, kwa hiyo tutafika mpaka
kwenye ngazi ile ya chini” alisisitiza Bw. Kailima na kuongoeza kuwa:
“Tuwaombe tu kwamba wakisikia Tume ipo kwenye
mkutano wa kijiji kabla hawajaanza
mkutamo wao, basi waje tuwasikilize.
Lakini pia tutawafuata viongozi wa dini
tuweze kutoa elimu ya mpiga kura”.
Alibainisha kuwa kupatia viongozi wa dini, Tume
itawaomba wanapojumuika kwa ajili ya ibada zao kwenye makanisa au misikiti
waialike NEC iwaelimishe waumini wao kuhusu elimu ya mpiga kura.
“Kwa hiyo tutakwenda katika kila kona taratibu
hadi kufikia mwaka 2020, Mungu akituweka hai nchi itabadilika na mwananchi atafahamu
utaratibu mzima wa kuandikisha wapiga kura, kupiga kura na shughuli za Tume.” alisema
Bw. Kailima.
Alifafanua kuwa miakakati hiyo ikifanikiwa
kutekelezwa itapunguza kwa kiwango kikubwa upotoshaji unaofanywa kuhusu
mchakato wa Uchaguzi kwani wananchi watakuwa wanafahamu majukumu ya NEC na majukumu
ya kwenye Uchaguzi.
Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) inatekeleza
mikakati wa kutoa Elimu ya Mpiga nchi nzima na sasa inashiriki kwenye Wiki ya
Vijana, Sherehe za Uzimaji wa Mwenge wa Uhuru na Kumbukumbu ya Kifo cha Mwalimu.
Julias Nyerere mkoani Simiyu.
Hivyo Bw. Kailima aliwataka wananchi wafike kwenye
banda la NEC kwenye uwanja wa Halmashauri ya Bariadi zinapofanyika shughuli
hizo ili kuapata Elimu ya Mpiga kura inayotolewa.
No comments:
Post a Comment