TANGAZO


Monday, October 17, 2016

BALOZI SEIF IDDI, MBUNGE BAHATI ALI ABEID WAKABIDHI VIFAA VYA UJENZI NA KUSAMBAZA MAJI MATAWI YA CCM KAZOLE, MATETEMA KISIWANI UNGUJA

Mwakilishi wa Jimbo la Mahonda Balozi Seif Ali Idd na Mbunge wa jimbo hilo, Mhe. Bahati Ali Abeid (wa kwanza kushoto), wakimkabidhi vifaa vya Ujenzi Katibu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Tawi la Matetema Ndg. Pandu Khamis Juma aliyepo kati kati yao kwa ajili ya kuendeleza ujenzi wa Ofisi yao ya Tawi.(Picha zote na Hassan Issa – OMPR – ZNZ)
Balozi Seif  akimkabidhi vifaa vya Ujenzi Katibu wa CCM Tawi la Kazole Nd. Sharifu Makame Pandu mwenye sharubu  kwa ajili ya kuendeleza ujenzi wa Ofisi yao ya Tawi. 
Mwakilishi wa Jimbo la Mahonda Balozi Seif Iddi na Mbunge wa Jimbo hilo Mhe. Bahati wakiukabidhi uongozi wa CCM Tawi la Kazole Mipira ya kusambazia maji safi na salama kwa ajili ya Kijiji hicho. 
Mke wa Mwakilishi wa Jimbo la Mahonda Mama Asha Suleiman Iddi akiulaumu Uongozi wa CCM wa Matawi ya Matetema na Kazole kushindwa kuitisha vikao vya kujadili ripoti ya utekelezaji wa ilani ya CCM uliofanywa na  Uongozi wa Jimbo la Mahonda hapo Tawi la CCM Kazole.

Na Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
16/10/2016.

MJUMBE wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya Chama cha Mapinduzi (CCM), Balozi Seif Ali Iddi amekemea  tabia mbovu iliyoanza
kujichomoza ndani ya Majimbo hapa nchini inayoleta migogoro kwa baadhi ya Wabunge na Wawakilishi ambayo haileti sura nzuri kwa Wananchi waliokubali kuwatumikia.


Alisema yapo malalamiko kadhaa yaliyokwisha ripotiwa katika Vikao vya Kamati za Siasa za Wilaya yanayohusu migongano inayotokea ikiwahusisha Waheshimiwa Wabunge na Wawakilishi kwenye baadhi ya Majimbo malalamiko ambayo yanastahiki kupigwa vita na wanachama wenyewe.

Balozi Seif akiambatana na Mbunge wa Jimbo hilo Mh. Bahati Ali Abeid pamoja na Madiwani wa Wadi zilizomo ndani ya Jimbo hilo alitoa kemeo hilo wakati wa muendelezo wa ziara zao za kuwashukuru wana CCM na Wananchi wa Matawi ya CCM Matetema na Kazole baada ya kumalizika kwa uchaguzi Mkuu mapema mwaka huu.


Alisema kazi ya wanachama wa chama cha Mapinduzi kwa hivi sasa ni kuchunguza virusi vilivyomo ndani ya chama kubaini kasoro hiyo ili kuhakikisha wakati utakapowadia wa chaguzi za Chama wanaweka Wanachama madhubuti waliokamikia Kimaadili ya Uongozi.


Mjumbe huyo wa Kamati Kuu ya CCM Taifa ambae pia ni Mwakilishi wa Jimbo la Mahonda alisisitiza kwamba Wanachama wa CCM lazima wasimamie
ipasavyo kumpata kiongozi atakayekidhi sifa ya kuwatekelezea matakwa yao.


Alisema maeneo ya kumtafuta kiongozi bora na makini  hupatikana ndani ya Vikao vya Chama kwa vigezo sahihi zinavyohitajika na ikishindikana
wana wajibu wa kumtafuta Kiongozi mwengine kupitia vikao hivyo hivyo.


Naye Mbunge wa Jimbo la Mahonda Mh. Bahati Ali Abeid  akiwashukuru wanachama na wananchi hao wa Matawi la Matetema na Kazole aliwataka
wananchi wa maeneo hayo kukubali kuwa na moyo wa kusamehe fidia katika masuala ya maendeleo yanayoanzishwa kwenye maeneo yao.


Mh. Bahati alisema ipo miradi inayokusudiwa kuanzishwa na Serikali na hata Jamii katika maeneo yao kama huduma za Umeme, Maji na Bara bara
lakini hukumbwa na vikwazo kutokana na baadhi ya Wananchi kukataa kusamehe mazao au miti yao kwa kusisitiza kulipwa fidia.


Alisema ukosefu wa bara bara au huduma ya umeme katika maeneo ambayo watu hukataa miradi hiyo kwa kisingizio cha kulipwa fidia mara nyingi
huchelewesha kupata maendeleo ya jamii katika maeneo hayo.


Mh. Bahari alifahamisha kwamba ipo mifano hai iliyowahi kutokea ya matatizo kama hayo katika baadhi ya maeneo ambayo jamii husika hubakia
kujilaumu kwa uzembe uliokwisha tekelezwa na wenzao waliobeba tamaa zaidi.


Mapema Mke wa Mwakilishi wa Jimbo la Mahonda Mama Asha Suleiman Iddi aliwalaumu Viongozi wa Matawi ya CCM kwa kushindwa kwao kuitisha vikao
vya kujadili ripoti za utekelezaji wa Ilani ya Chama iliyofanywa na Waheshimiwa wao katika vipindi vya kila baada ya miezi Mitatu.


Mama Asha aliwaeleza wanachama hao wa CCM wa Matawi ya Matetema na Kazole kwamba utekelezaji wa Ilani kwa Viongozi hao wa Jimbo la Mahonda katika miradi ya sekta ya elimu, Afya, Maji na Bara bara tayari umepindukia gharama ya zaidi ya shilingi Milioni 100.


Alieleza kwamba kasumba zinazoendelezwa kila kukicha ni miongoni mwa ishara za upinzani kuogopa utekelezaji mzuri wa Ilani ya CCM  ya Mwaka 2015 -2020 inayosimamiwa na Viongozi wa chama hicho hasa Majimboni.


Katika ziara hiyo ya shukrani Wahesimiwa hao wa Jimbo la Mahonda walikabidhi vifaa vya ujenzi kwa ajili ya kuendeleza Ofisi za CCM za Matawi ya Matetema na Kazole ili zilingane na hadhi ya chama chenyewe.


Vifaa hivyo ni pamoja na Mchanga, Saruji na fedha taslimu za mafundi ili kupiga plasta ya majengo hayo sambamba na mipira ya kusambazia maji safi na salama kwa Kijiji cha Kazole vikiwa na thamani ya
shilingi Milioni 2.820.

No comments:

Post a Comment