Na
Ally Daud, Maelezo,Dar
es Salaam
29.9.2016
IMEBAINIKA kuwa ulaji
wa vyakula visivyo bora husababisha maradhi ya magonjwa ya moyo kwa watu wazima
wa miaka 45 hadi 60.
Aidha tafiti
zinaongeza kuwa watoto wadogo pia ni miongoni mwa waathirika wa ugonjwa wa moyo,
wanaoupata kutokana na kurithi kutoka kwa wazazi wao.
Hayo yamesemwa leo
Jijini Dar es Salaam na Msemaji Mkuu wa Taasisi
ya Moyo ya Jakaya Kikwete Bw. Maulid Kikondo wakati wa maadhimisho ya siku ya moyo duniani ambapo kitaifa ilifanyika
katika taasisi hiyo.
Kikondo alisema kuwa
katika kuadhimisha siku hiyo Taasisi hiyo imeamua kupima wagonjwa wa moyo bure ili kuwasaidia
wananchi kuweza kufahamu njia bora za kuweka kukabiliana na magonjwa hayo.
Kikondo alisema kuwa
wazee na watoto hupata maradhi ya moyo kwa wingi nchini kutokana kula vyakula
visivyo na mpangilio pamoja na kukosa kufanya mazoezi kwa muda mrefu.
“Ugonjwa wa moyo
huwapata zaidi watoto kutokana kwa kurithi au kutopata mlo ulio bora na
mpangilio wakati wazee hupata ugonjwa huu kutokana na msongo wa mawazo pamoja
na kutofanya mazoezi mara kwa mara hivyo kupelekea kupata presha na mwisho wake
ni ugonjwa wa moyo” alisema Kikondo.
Aidha Kikondo alisema
kuwa wagonjwa wa moyo wanaopatikana kwa siku ni kuanzia wagonjwa 200 na
kuendelea kiasi ambacho ni hatari kwa maendeleo ya nchi hasa kwa taifa
linaloelekea katika uchumi wa kati.
Kwa upande wa taarifa
iliyotolewa na Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi hiyo Dkt. Delilah Kimambo imesema
kuwa inasadikika duniani kote kati ya watu milioni 17.3 hupoteza maisha yao
kutokana na ugonjwa wa moyo.
Siku ya Moyo Duniani
huadhimishwa Septemba 29 kila mwaka ili kuhamasisha watu kuhusu afya ya Moyo
ambapo kauli mbiu ya mwaka huu ni “YAPE NGUVU MAISHA YAKO”
No comments:
Post a Comment