TANGAZO


Thursday, August 25, 2016

JENISTA MHAGAMA KUFUNGUA MAONESHO YA WAJASIRIAMALI

Katibu Mtendaji wa Baraza la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi (NEEC) Bi. Benga’i Issa wa kwanza kulia akiongea na waandishi wa habari hawapo pichani kuhusu maonesho ya wajasiriamali yataofanyika Septemba 26 mwaka huu jijini Dar es Salaam. Kushoto ni Mkurugenzi Mtendaji waTaasisi ya Sekta Binafsi nchini (TPSF), Bw.Godfrey Simbeye.
Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Sekta  Binafsi nchini (TPSF)  Bw. Godfrey Simbeye kushoto akiongea na waandishi wa habari hawapo pichani kuhusu maonesho ya wajasiriamali yataofanyika Septemba 26 mwaka huu jijini Dar es salaam, kulia ni Katibu Mtendaji wa Baraza la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi (NEEC) Bi. Benga’i Issa.Habari/Picha Na Ally Daud. 
  
WAZIRI wa Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Walemavu Mhe. Jenista Mhagama anatarajiwa kufungua maonesho ya wajasiriamali yatakayo fanyika Septemba 26 katika viwanja vya Mlimani City ambayo yameandaliwa na Taasisi ya Ujasiriamali na ushindani Tanzania (TEEC) kwa kushirikiana na Baraza la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi (NEEC) pamoja na Taasisi ya Sekta  Binafsi nchini (TPSF) ili kukuza uchumi wa nchi.

Akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es salaam Katibu Mtendaji wa NEEC Bi. Beng’i Issa amesema kuwa maonesho hayo yatalenga kuwawezesha wananchi kuwa wabunifu katika sekta ya biashara ili kupiga hatua kufikia uchumi wa kati.

“Maonesho ambayo yatafanyika kesho ni kwa ajili ya wajasiriamali wote wakubwa, wa kati na wadogo ili kuwawezesha kiujuzi na kiushindani katika soko la biashara” alisema Bi. Issa.

Aidha Bi. Issa amesema kuwa siku hiyo kutakuwa na kliniki ya biashara kwa watu wote kutoka kwa wataalamu wa biashara ili kuweza kuwapatia mafunzo wajasiriamali wakubwa na wadogo ili waweze kupata mafanikio yao na jamii kwa ujumla kupitia biashara zao.

Kwa upande wa Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Sekta Binafsi nchini (TPSF)  Bw. Godfrey Simbeye amesema kuwa maonesho hayo  yatawajengea wajasiriamali fursa za masoko kwa biashara nchini na Afrika kwa ujumla.

“Kupitia maonesho hayo wajasiriamali watapata fursa ya kutengeneza masoko ya biashara zao kwa ubora zaidi nchini na afrika kwa ujumla ili waweze kujitangaza kimataifa” alisema Bw. Simbeye.

Aidha Bw. Simbeye amesema kuwa wana mpango wa kuwaelimisha wajasiriamali kwa wingi zaidi ili waweze kuwa wabunifu na kukuza uchumi wa nchi kupitia sekta ya biashara ndani na nje ya Tanzania.

Mbali na hayo Mkurugenzi Simbeye amesema kuwa anawakaribisha watu wote wajasiriamali wakubwa na wadogo kufika katika maonesho hayo ambayo hayana kiingilio ili waweze kupata ujuzi wa kutosha kwa maendeleo ya biashara zao na kuinua uchumi wa nchi.

No comments:

Post a Comment