TANGAZO


Monday, May 9, 2016

TIB IMETOA MIKOPO YA SHILINGI BIL. 550 KWA WATANZANIA

Naibu Waziri, Wizara ya Fedha na Mipango, Mhe. Ashatu Kijaji akijibu maswali mbalimbali kuhusu Benki ya TIB na TADB katika kupunguza umaskini, leo Bungeni mjini Dodoma. (Picha na Benedict Liwenga-Maelezo, Dodoma)

Na Benedict Liwenga-Maelezo, Dodoma
HADI kufikia mwaka jana (2015) Benki ya Uwekezaji Tanzania (TIB) imewawezesha Watanzania wengi kupambana na umaskini kwa kutoa mikopo ya zaidi ya shilingi bilioni 550 katika sekta mbalimbali za kiuchumi.

Taarifa hiyo imetolewa leo Bungeni Mjini Dodoma na Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Ashatu Kijaji wakati akijibu swali toka kwa Mbunge wa Karagwe, Mhe. Innocent Bashungwa (Mb) lililotaka kujua Serikali ina mpango gani wa kuhakikisha kuwa Benki za TIB na TADB zinajielekeza kwenye utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM.

Mhe. Kijaji ameeleza kuwa, madhumuni ya kuanzishwa kwa benki ya TIB na TADB kama benki za maendeleo ni kutoa mikopo ya muda wa kati na muda mrefu kwa lengo la kufadhili miradi ya kimkakati, hivyo katika kutimiza azma ya kufadhili miradi ya kimkakati ya kufungua fursa za kiuchumi na kupunguza umaskini, TIB imetoa mikopo katika maeneo ya miji kupitia NHC, Viwanda vya kubangua korosho, maghala, mabomba ya maji, sukari na kilimo cha miwa, kukoboa na kusindika kahawa, kusindika matunda, mifuko ya kuhifadhia mazao na nyaya za umeme; vinu vya pamba na uzalishaji wa mafuta yatokanayo na mbegu za pamba na hoteli.

Aidha, TIB imetoa mkopo wa shilingi bilioni 489.2 kwa ajili ya utekelezaji wa miradi 181 ya kusambaza umeme vijijini kupitia REA na kaya 257,000 zimenufaika na mradi huo. Pia vikundi 17 vya wachimbaji wadogo wadogo vimenufaika na mikopo jumla ya shilingi bilioni 8.

“Mikopo ya TIB kwa sekta na taasisi mbalimbali imesaidia kwa kiasi kikubwa kutoa ajira na kuendeleza zilizopo. Pia mikopo ya TIB imetumika kuongeza uzalishaji wa bidhaa zinazouzwa nje kama vile maua, kahawa na dhahabu”, alisema Kijaji.

Aliongeza kuwa pamoja na benki ya Kilimo kuchelewa kuanza kutoa mikopo, ni wazi kuwa benki ya TIB imejielekeza kwenye utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM pamoja na utekelezaji wa Mipango na mikakati mbalimbali ya maendeleo ikiwemo Dira ya Taifa ya 2025, FYDB, SDGs 2030 pamoja na Afrika 2063.

TIB imewekeza katika mashirika ya umma kama vile Shirika la Reli (TRL), pia imeiwezesha TPDC katika mradi wa gesi na kuipatia Shirika la Ugavi Umeme Tanzania (TANESCO) mkopo kwa ajili ya fidia kwa wananchi ili kuweka njia mpya ya kusafirisha umeme.

No comments:

Post a Comment