Naibu Waziri, Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira Mhe. Luhaga
Na Tiganya Vincent_MAELEZO-Dodoma.
JUMLA ya shilingi bilioni 224.314 (224,314,313,555.30) zimepokelewa na Serikali toka kwa wafadhili ili kusaidia kupunguza athari na kuhimili mabadiliko ya tabianchi.
Kauli hiyo imetolewa leo mjini Dodoma na Naibu Waziri, Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira Mhe. Luhaga Mpina alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Jimbo la Wawi Mhe. Ahmed Juma Ngwali aliyetaka kujua serikali imeokea kiasi gani toka kwa wafadhili kusaidia kupunguza athari na mabadiliko ya tabianchi tangu 2010 hadi 2015.
Alisema kuwa kati ya fedha hizo shilingi bilioni 7,017(7,017,510,977.40) na shilingi 217.296 (217,296,802,577.90 zilipokelewa moja kwa moja kutoka kwa wadau wengine.
Mhe. Mpina alisema kuwa fedha hizo zilipatikana baada ya kuandaa miradi kwa kuzingatia vigezo na viapaumbele vya vyanzo vya fedha husika.
Alisema kuwa kati ya fedha hizo shilingi bilioni 17.2 zilipelekwa Zanzibar kwa ajili miradi ya ujenzi kutwa katika baadhi ya maeneo ya bahari ambayo yameanza kuathirika na upandaji wa mikoko ili kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.
Mhe. Mpina alisema kuwa fedha hizo zimepokelewa kutoka Mifuko iliyo chini ya Mkataba wa Mabadiliko ta Tabianchi na ushirikiano na nchi wafadhili.
MALIASILI NA UTALII KUSHIRIKIANA NA SEKTA BINAFSI KUWEKEZA KATIKA UTALII WA KUSINI MWA TANZANIA
Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii Mhe. Injinia Ramo Makani
Na Tiganya Vincent-MAELEZO_Dodoma.
WIZARA ya Maliasili na Utalii imesema kuwa inatarajia kuboresha utalii wa Kusini mwa Tanzania kupitia miradi mbalimbali kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo chini ya mradi wa REGROW unaofadhiliwa na Benki ya Dunia kwa gharama za shilingi bilioni 2.1.
Fedha hizo zinafadhiliwa na Benki ya Dunia sawa na dola za Kimarekani zisizopungua milioni moja.
Kauli hiyo imetolewa leo mjini Dodoma na Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii Mhe. Injinia Ramo Makani wakati akijibu swali Mbunge wa Jimbo la Lindi Mjini Mhe. Hassan Kaunje aliyetaka kujua mpango wa Serikali wa kuendeleza utalii wa ukanda wa kusini.
Alisema kuwa hatua hiyo inalenga kuwekeza katika miundombinu ya utalii kwa ajili ya kuutangaza utalii wa Ukanda wa Kusini mwa Tanzania ili uweze kusaidia ukuaji wa uchumi na ustawi wa Taifa.
Alisema kuwa mpango huo utajumuisha kuimarisha mafunzo ya utalii na kutenga maeneo maaalum ya utalii katika fukwe za bahari na maziwa kwa ajili hoteli za kitalii.
Mhe. Makani alisema kuwa Serikali imepanga kutekeleza mkakati wa kuutangaza maeneo ya utalii ikiwemo vivutio kihistoria na kiutamaduni kama vile mji wa kihistoria wa Mikindani, Kilwa Kivinje, Pori la Akiba Lukwika-Lumese na Pori la Akiba la Seleous.
Aliongeza kuwa ili kukuza utalii wa fukwe katika eneo hilo , Serikalai imejipanga kutenga maeneo maalum hususan kwa ajili ya hoteli za kitalii kando ya Bahari ya Hindi mkoani Mtwara na Lindi.
SERIKALI KUSOGEZA HUDUMA ZA ZIMAMOTO NA UOKOAJI KWA WANANCHI
Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhe. Mhandisi Hamad Masauni
Na Benedict Liwenga, Dodoma.
SERIKALI imesema itaendelea kusogeza huduma za Zimamoto na Uokoaji kwa wananchi kwa jinsi hali ya upatikanaji wa fedha itakavyoruhusu.
Kauli hiyo imetolewa leo Bungeni mjini Dodoma na Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhe. Mhandisi Hamad Masauni wakati akijibu swali la Mbunge wa Tunduma, Mhe. Frank Mwakajoka ambaye alitaka kujua ni lini Serikali itapeleka huduma za Zimamoto katika Mpaka wa Tunduma ili kuokoa mali za wafanyabiashara wanaosubiri kuvuka pindi ajali ya moto inapotokea.
Mhe. Msauni ameeleza kuwa, Jeshi la Zimamoto na Uokoaji katika Halmashauri ya Mji wa Tunduma lina Kituo katika eneo la mtaa wa Kilimanjaro, Wilaya ya Momba katika Mkoa wa Songwe kinachohudumia Wilaya yote ukiwemo Mpaka wa Tunduma.
"Kwa sasa Kituo hiki kina gari moja lililopo matenegenzo Jijini Mbeya, hata hivyo askari wanaendelea kutoa elimu ya Kinga na tahadhari ya Majanga ya Moto na utumiaji wa vifaa vya huduma ya kwanza vya uzimaji moto", alisema Masauni.
Aliongeza kuwa, sambamba na ukaguzi wa majengo ya kutoa ushauri kwa kandarasi au makampuni ya ujenzi kuhusu ujenzi bora wa miundombinu yenye usalama kwa umma.
"Ni azma ya Serikali kupeleka huduma ya Zimamoto katika maeneo yote ya nchi ikiwemo Tunduma, hata hivyo azma hii nzuri inategemea na upatikanaji wa rasilimali fedha, Serikali itaendelea kusogeza huduma za Zimamoto na Uokoaji kwa wananchi kwa jinsi hali ya upatikanaji wa fedha itakavyoruhusu", aliongeza Masauni.



No comments:
Post a Comment