TANGAZO


Wednesday, May 18, 2016

KATIBU MKUU DK. CHAMURIHO AFANYA ZIARA YA KUSHTUKIZA KWENYE FLOW MITA YA MAFUTA



Meneja Mradi /Msimamizi wa Ujenzi wa mradi wa Mita za kupimia mafuta Mhandisi Mary Mhayaya (kushoto), akitoa maelezo kwa  Katibu Mkuu wa Uchukuzi Dkt Leonard Chamriho (kushoto) kuhusu mfumo wa kompyuta wa mita ya kupimia mafuta unavyofanya kazi kwa kutoa taarifa kuhusu mwenendo wa wa utendaji kazi wa mita hiyo.
Kaimu Meneja wa Bandari ya Dar es Salaam Hebel Mhanga (wa pili kushoto) akitoa ufafanuzi kwa Katibu Mkuu wa Uchukuzi Dkt Leonard Chamriho (kulia) kuhusu ufanyaji kazi wa mifumo ya kuendesha mita ya kupimia mafuta (flow meter) uliojengwa eneo la Kwa Mwingira Mji Mwema Kigamboni Jijini Dar es Salaam wakati wa ziara ya kushtukiza iliyofanywa na katibu Mkuu huyo leo Mei 18,2016. 

Katibu Mkuu wa Uchukuzi Dkt Leonard Chamriho (kulia), akipatiwa maelezo.
Katibu Mkuu wa Uchukuzi Dkt Leonard Chamliho akipanda ngazi kuelekea kwenye pambu na valvu zilizofungwa kwenye mita ya kupimia mafuta(Flow Meter) wakati alipofanya ziara ya kushtukiza kukagua utendaji kazi wa mita hiyo leo Mei 18,2016. 
Meneja Mradi /msimamizi wa Ujenzi wa mradi wa Mita za kupimia mafuta Mhandisi Mary Mhayaya (kushoto) akitoa maelezo kwa Katibu Mkuu wa Uchukuzi Dkt Leonard Chamliho (wa pili kushoto) kuhusu hitilafu iliyojitokeza katika moja ya valvu zilizoko kwenye  mita hiyo, upande unaoendeshwa  kwa kutumia  mfumo wa digitali  hali iliyosababishwa na mvua zilizokuwa zikiendelea kunyesha hivi karibuni Jijini Dar es Salaam.Mita hiyo sasa inatumia mfumo wa analojia na  hatua ya urejeshaji wa valvu hiyo katika hali yake ya awali inafanyiwa kazi na mkandarasi aliyepewa zabuni ya kujenga mita hiyo leo. 
Katibu Mkuu wa Uchukuzi Dkt Leonard Chamliho ( wa pili kulia) akitoa maagizo kwa Mamlaka ya Bandari kuyafanyia kazi mapungufu yaliyojitokeza ikiwemo hitilafu ya kamera za ulinzi na baadhi ya valvu kwenye mita ya kupimia mafuta na kuwasilisha taarifa ofisi kwake Jumatatu Mei 23 namna ya watakavyoshughulikia mapungufu yaliyojitokeza. 
Meneja Mradi /msimamizi wa Ujenzi wa mradi wa Mita za kupimia mafuta Mhandisi Mary Mhayaya akitoa maelezo kwa Katibu Mkuu wa Uchukuzi Dkt Leonard Chamliho (mwenye Kaunda suti) kuhusu ufanyaji kazi wa mtambo unaochuja mafuta kwa lengo la kudhibiti na kuzuia mafuta machafu kuingia nchini kupitia Bandari ya Dar es Salaam leo Mei 18,2016. 
Mita ya Kupimia Mafuta (Flow Meter) iliyojengwa eneo la kwa mwingira, mji Mwema Kigamboni  Jijini Dar es salaam . Utaratibu wa kujenga uzio na paa kufunika mtambo huo unaendelea kupitia mkandarasi aliyepewa jukumu la kujenga mradi huo ili kuhimarisha ulinzi na usalama wa mita hiyo.(Picha zote na Raymond Mushumbusi na Aron Msigwa-Maelezo)

Na Lorietha Laurence -  Maelezo,Dar es Salaam.
KATIBU Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Uchukuzi) Mhandisi Dkt. Leornad Chamuriho ameupa siku mbili uongozi wa Bandari unaosimamia Mita ya Kupimia mafuta nchini (Flow Meter) iliyoko Kigamboni jijini Dar es Salaam kuhakikisha kuwa unatoa taarifa ndani ya siku mbili kuhusu hitilafu iliyojitokeza kwenye mfumo wa kufungua valvu za mita hiyo upande wa umeme. 

Aidha, ameuagiza uongozi huo kutoa taarifa kuhusu hitilafu ya kamera 2 za usalama zilizoungua na kushindwa kufanya kazi kwa takribani mwezi mzima. 

Katibu Mkuu huyo ametoa maagizo hayo mara baada ya kufanya ziara ya kushtukiza katika mita hiyo eneo la mji Mwema Kigamboni leo jijini Dar es salaam na kubaini upungufu wa utendaji wa baadhi ya maeneo.

Maeneo hayo ni pamoja na  kamera za kufuatilia mwenendo wa usalama wa mita hiyo, valvu zilizoshindwa kufanya  kazi upande wa mfumo wa umeme hivyo kubakiwa na njia ya analoji kutokana na hali ya mvua zilizokuwa zikiendelea kunyesha jijini Dar es salaam.

“Ifikapo Jumatatu nipatiwe taarifa kuhusu matengenezo ya vifaa hivi, hatua zilizochukuliwa na mnieleze lini ukarabati wake utakamilika pia ujenzi wa paa kuzuia athari ya mvua kwenye mita hii” amesema Dkt. Chamuriho.

Ameongeza kuwa dhumuni la Serikali ni kuhakikisha vifaa hivyo vinafanya kazi katika viwango vinavyostahili ili kulinda mapato yanayotokana na mafuta yanayoingia nchini ili Serikali ipate kodi halali na hivyo kuongeza mapato ya nchi na kuondoa malalamiko kwa wateja.

Kwa upande wake Meneja Mradi wa Ujenzi wa Mita hiyo  kutoka Mamlaka ya  Bandari nchini Mhandisi Mary Mhayaya ameeleza kuwa uharibifu wa vifaa hivyo umesababishwa na mvua zilizonyesha hivi karibuni na tayari vifaa hivyo vimeanza  kukabarati.

"Kisichofanya kazi ni mfumo wa kufungua mafuta upande wa umeme kwenye baadhi ya valve, upande wa analoji unafanya kazi vizuri na kazi ya upakuaji mafuta kupitia mfumo wa analojia inaendelea kama kawaida" Amesisitiza.

Amesema kuwa tayari wamemweleza mkandarasi aliyefunga vifaa hivyo kuvifanyia marekebisho haraka iwezekanavyo.

Naye Kaimu Meneja wa Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) Hebel Mhanga amesema kuwa ofisi yake inajukumu la kuhakikisha inatoa huduma sahihi kwa wateja wanaotumia mitambo hiyo iliyopo bandarini  hapo na Serikali inapata mapato kulingana na huduma iliyotolewa.

Mita ya Kupimia Mafuta yalnayoingia nchini iko katika hatua ya majaribio kwa kipindi cha mwaka mmoja ambapo tayari meli tatu zimefanyiwa majaribio ya upakuaji wa mafuta huku moja ikiwa imefanyiwa vipimo.

No comments:

Post a Comment