Shirika la kukadiria ubora wa bidhaa nchini Kenya KEBS limefunga viwanda sita vya kupakia maji ya chupa kwenye kampeni inayoendelea ya kudhibiti maji machafu ya kunywa.
Aidha serikali ya kaunti ya Mombasa pia imepiga marufuku uuzaji wa baadhi ya maji chupa baada ya kuzipata na maradhi.
Zaidi ya kampuni mia sita nchini Kenya zina leseni ya kupakia maji ya chupa, lakini kuna hofu kwamba kampuni bandia ni zaidi ya hiyo.
Maji ya chupa huuzwa sana kwenye maduka ya bara Afrika, lakini nchini Kenya si yote ni masafi.
Shirika la kukadiri ubora linaonya wateja kwamba maji ya chupa wanayokunywa si masafi kama yanavyouzwa.
Jijini Mombasa pekee, kampuni sita zimefungwa kwa kupakia maji machafu.
Aidha idara ya afya Mombasa imepiga marufuku uuzaji wa baadhi ya maji yanayouzwa baada ya chembe za bacteria zinazopatikana kwenye kinyesi kupatikana kwenye maji hayo.
Mombasa imekabiliwa na kuenea kwa ugonjwa wa Hepatitis A, ambao husambazwa kwa virusi Zaidi kutokana na kwa kunywa maji au kula chakula kilicho na virusi hivyo.
Wakazi wengi kwenye miji ya Kenya hawaamini kunywa maji ya mifereji baadhi ya wataalamu wengine huonya kwamba maji ya mifereji huchanganyika na maji taka kwenye mabomba.
Shirika sasa linapania kuboresha alama yake ya viwango, ili kutenga bidhaa duni kutoka sehemu za mauzo.
No comments:
Post a Comment