TANGAZO


Monday, May 23, 2016

SERIKALI KUJENGA NYUMBA 9500 KWA AJILI YA ASKARI MAGEREZA

Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Mhe. Hamad Yusuf Masauni

Na Fatma Salum- MAELEZO, Dodoma.
SERIKALI kupitia Jeshi la Magereza imesaini Mkataba na Kampuni ya Poly Technologies ya China kujenga nyumba 9,500 kwenye vituo vyote vya Magereza nchini.

Hayo yamesemwa na Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Mhe. Hamad Yusuf Masauni wakati akijibu swali kuhusu kuboresha makazi ya askari lililoulizwa na Mhe. Devota Minja (Mb) leo bungeni mjini Dodoma. 

Mhe. Masauni alibainisha kuwa  kupitia mkataba huo Serikali itapunguza kwa kiasi kikubwa changamoto iliyopo ya uhaba wa nyumba kwa ajili ya askari wa jeshi hilo ambapo mahitaji kwa sasa ni nyumba 14,500 wakati zilizopo ni nyumba 4,221 hivyo kupelekea upungufu wa nyumba 10,279. 

“Serikali inafahamu kuwa lipo tatizo la baadhi ya askari wa Jeshi la Magereza na Polisi kuishi katika nyumba chakavu zisizokuwa na hadhi, hivyo katika kukabiliana na tatizo hili Serikali imeendelea kuzifanyia ukarabati mkubwa baadhi ya nyumba na pia kujenga nyumba mpya”. Alisema Masauni.

Mhe. Masauni alifafanua  kuwa mgawanyo wa ujenzi wa nyumba hizo mpya ni Makao Makuu ya Magereza nyumba 472, Arusha nyumba 377, Dar es Salaam nyumba 952, Dodoma 356, Kagera 364, Kigoma 272, Kilimanjaro 390, Lindi 233, Manyara 206, Mara 378, Mbeya 622, Iringa 336, Morogoro 669, Mtwara 215, Mwanza 398, Pwani 384, Rukwa 358, Ruvuma 320, Shinyanga 337, Singida 299, Tabora 408, Tanga 382, KMKGM Dar es Salaam 219, Chuo cha Ukonga 115, Chuo cha Kiwira 183, Chuo cha Ruanda 62, Chuo KPF 27, Bohari Kuu 82 na Bwawani nyumba 84. 

Aidha, Mhe. Masauni aliongeza kuwa kwa upande wa Jeshi la Polisi, Serikali inakusudia kujenga nyumba 4,136 katika mikoa 17 ya Tanzania Bara na Zanzibar zitakazosaidia kupunguza tatizo la makazi kwa askari wa jeshi hilo. 

Mhe. Masauni alilieleza bunge kuwa Serikali itaendelea kutatua changamoto ya uhaba wa nyumba kwa kutumia njia mbalimbali ikiwemo mikopo yenye riba nafuu, Miradi Shirikishi (PPP) na kwa kutumia fedha za bajeti ya Serikali kadri hali ya uchumi itakavyokuwa inaimarika.


DAR YAONGOZA KWA AJALI ZA BARABARANI

Na Fatma Salum- MAELEZO, Dodoma.
SERIKALI imesema kuwa Jiji la Dar es Salaam linaongoza kwa  kuwa na ajali nyingi za barabarani kwa miaka mitatu mfululizo kuanzia mwaka 2013 hadi 2015 zilizosababisha vifo vya watu pamoja na majeruhi.

Taarifa hiyo imetolewa leo bungeni mjini Dodoma na Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Mhe. Hamad Yusuf Masauni wakati akijibu swali la Mbunge wa Biharamulo Magharibi Mhe. Oscar Rwegasira  kuhusu kuongezeka kwa vifo vitokanavyo na ajali za barabarani.

Kwa mujibu wa takwimu zilizotolewa na Mhe. Masauni kwenye taarifa hiyo Jiji la Dar es Salaam limeongoza kwa kuwa na ajali 18,506 kati ya ajali 46,539 zilizotokea nchi nzima kwa kipindi cha mwaka 2013 hadi 2015.

“Takwimu za nchi nzima zinaonesha kuwa Mwaka 2013 zilitokea ajali 23,842 zilizosababisha vifo 4,002 na majeruhi  20,689. Mwaka 2014 zilitokea ajali 14,360 zilizosababisha vifo 3,760 na majeruhi 14,530 na mwaka 2015 zilitokea ajali 8,337 zilizosababisha vifo 3,468 na majeruhi 9,383.” alisema Masauni. 

Mhe. Masauni alieleza kuwa kwa mwaka 2013 Mkoa wa Kipolisi Kinondoni uliongoza kwa kuwa na ajali zipatazo 6,589 ukifuatiwa na Mkoa wa Kipolisi Ilala uliokuwa na ajali 3,464 wakati Mkoa wa Simiyu na Tanga kulikuwa na ajali chache ambapo Simiyu zilitokea ajali 67 na Tanga ajali 96. 

Mwaka 2014 Kinondoni na Ilala ziliongoza tena kwa kuwa na ajali 3,086 zilizotokea  Kinondoni  na Ilala ajali 2,516 na mikoa iliyokuwa na ajali chache ni Simiyu ajali 55 na Kagera ajali 29.

Aidha, Mhe. Masauni alisema kuwa mwaka 2015 Mkoa wa Kipolisi Ilala uliongoza kwa kuwa na ajali nyingi za barabarani ambapo ajali 2,516 zilitokea mkoani humo ikifuatiwa na Temeke uliokuwa na ajali 1,420 wakati mikoa ya Rukwa na Arusha ilikuwa na ajali chache. 

Mhe. Masauni alibainisha kuwa mfumo endelevu wa wazi uliopo wa kutoa takwimu  hizo ni kupitia taarifa za mwaka za Jeshi la Polisi (Polisi Annual Report) ambapo kila mtanzania anaweza kupata taarifa hizo za ajali.

No comments:

Post a Comment