
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akimfariji Said Khamis Mohamed wa Kijiji cha Shengejuu aliyevunjiwa nyumba na kuharibiwa mali zake zenye thamani ya zaidi ya shilingi 5,610,000/- kwa sababu za itikadi za kisiasa. (Picha zote na Hassan Issa – OMPR – ZNZ)
Nyumba ya Said iliyopo katika Kijiji cha Shengejuu inayoonekana kuharibiwa vibaya pamoja na kun’golewa madirisha yake yote katika hujuma iliyofanywa kwa sababu za itikadi za kisiasa.
Mkuu wa Wilaya ya Wete, Rashid Hadid (wa pili kulia) akimpatia maelezo Makamu wa Pili wa Rais, Balozi Seif Iddi kuhusu hujuma alizofanyiwa mwananchi Said Khamis na hatua za awali zilizochukuliwa na Ofisi yake, katika kukabiliana na vitendo vya hujuma.
Balozi Seif akimfariji mfanyakazi wa Idara ya Upigaji chapa na Mpiga chapa Mkuu wa Serikali, kisiwani Pemba, Kai Shaame Kai nyumbani kwake, Mkoa wa Kaskazini Pemba baada ya kushambuliwa kwa virungu na mikwaju na watu alipofika bandarini Kiuyu, Micheweni kununua samaki.
Balozi Seif Iddi akimpa pole Bibi Raya Yussuf Hamadi, mzazi wa ndugu Said Khamis wa Kijiji cha Shengejuu aliyepigwa jiwe zito kifuani kwa sababu za kisiasa na kumsababishia maumivu makali yaliyopelekea kulazwa Hospitali ya Wete Pemba, kwa ajili ya kupatiwa matibabu.
Sheha wa Maziwang’ombe, Bibi Asha Yussuf Hamadi, akifarijiwa na kupewa pole na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Ali Iddi baada ya kuvamiwa usiku wa manane kwa lengo la kuhujumiwa.
Nyumba ya Sheha wa Shehia ya Maziwang’ombe, Bibi Asha Yussuf, iliyobomolewa sehemu ya nyuma na kikundi cha watu kwa sababu za kisiasa na kumsababishia hasara kubwa.
Balozi Seif Ali Iddi akimjuilia hali na kumtakia Ramadhani njema inayokuja, Mzee Hassan Omar Abdulla (Shezume), alipomtembelea nyumbani kwake, Wilaya ya Micheweni, Mkoa wa Kaskazini Pemba.
Mwakilishi wa Wahandisi wa Ujenzi wa Hospitali ya Abdulla Mzee, Mkoani Kusini Pemba, Bwana Zhang Dou (aliyenyoosha kidole) akimfahamisha Balozi Seif Ali Iddi hatua ya ujenzi wa hospitali hiyo, ulipofikiawakati alipotembelea kuona maendeleo ya ujenzi wake. Wa kwanza kulia ni Mkuu wa mkoa huo, Mhe. Mwanajuma Majid Abdullah.
Mwonekano wa Majengo ya Hospitali ya Abdulla Mzee yalivyo, yakiwa katika hatua za mwisho za ujenzi wake.
Na Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
21/5/216.
MAKAMU wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi ameonya kwamba uvumilivu wa Serikali wa kumtaka kila Raia kutii sheria bila ya shuruti umefikia kikomo chake baada ya kustahamili kwa muda mrefu
ikitarajia kwamba watu au vikundi vyenye tabia ya kutishia amani ya nchi vitaendelea kuheshimu sheria.
Alisema uamuzi wa Serikali kwa sasa ni kumchukulia hatua za kisheria mtu au kikundi chochote kinachoendesha vitisho, kutishia na hata kuhujumu Wananchi wasio na hatia na mali zao kwa sababu tu za itikadi za Kisiasa.
Balozi Seif Ali Iddi alitoa onyo hilo wakati alipofanya ziara maalum ya kuwafariji na kuwaa pole Wananchi waliohujumiwa kwa kupigwa vipigo tofauti, kuvunjiwa nyumba zao, kuvurugiwa kwa mazao kama Migomba,
Mipunga na Mihogo katika Wilaya za Wete na Micheweni ndani ya mkoa wa Kaskazini Pemba.
Waliopatwa na mitihani hiyo ni pamoja na Ndugu Said Khamis Moh’d wa Kijiji cha Shengejuu aliyebomolewa nyumba yake, kuibiwa milango,
kukatwa migomba na mipunga wakati mama yake mzazi Bibi Raya Yussuf Hamad alipigwa jiwe na kumsababishia maumivu makali ya kifua yaliyopelekea kulazwa Hospitali ya Wete kwa matibabu.
Wengine ni Sheha wa Shehia ya Maziwang’ombe Bibi Asha Yussuf Hassan aliyavamiwa usiku kwa kutaka kuhujumiwa na familia yake, kubomolewa kwa nyumba yake na kukatwa kwa mapanga migomba yake yote pamoja na mfanyakazi wa Idara ya uchapaji Pemba Nd. Kai Shaame Kai aliyevamiwa
kwa kuigwa virungu kwa sababu za kisiasa wakati akijiandaa kununua samaki micheweni.
Balozi Seif alisema husda kwa baadhi ya watu hivi sasa inaonekana kupamba moto kwa kuchanganywa na Siasa za kijinga ambazo kamwe hazitalifikisha mahali popote Taifa zaidi ya kurejesha nyuma maendeleo ya wananchi kwa kuhujumiwa miradi yao wanayoitegemea kimaisha.
“Serikali imestahamili vya kutosha kwa sasa haitakuwa tayari kumvumilia mtu au kikundi chochote chenye nia ya kutaka kuvuruga amani ya nchi, uhuru wa wananchi sambamba na mali zao ”. Alisema Balozi Seif.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alisema wakati jeshi la Polisi Mkoa wa Kaskazini Pemba likiwashutumu watu Saba kuhusika na vitendo hivyo
ambapo Watano kati yake wanashikiliwa aliviagiza vyombo vinavyosimamia sheria kuhakikisha kwamba vinatekeleza jukumu lao ili kupunguza au kuondoa kabisa vita vitendo hivyo viovu.
Hata hivyo Balozi Seif alitahadharisha watendaji wa vyombo hivyo kwamba Serikali haitosita kumuwajibisha mtendaji ye yote atakayeamua
kutekeleza majukumu yake kwa ushabiki wa Kisiasa.
Balozi Seif aliwaomba Wananchi wote waliopatwa na mitihani hiyo kuendelea kuwa na moyo wa subira na Serikali wakati wote itajitahidi kuwahakikishia usalama wao na Wananchi wote kwa ujumla unapatikana.
Mapemba Muathirika wa matukio hayo wa Kijiji cha Shengejuu Ndugu Said Khamis Moh’d aliyepata hasara ya zaidi ya shilingi 5,610,000/- kutokana na hujuma aliyofanyiwa alisema matukio hayo yamesha zoeleka tokea kuanza kwa mfumo wa vyama vingi vya siasa hapa Nchini.
Ndugu Saidi alisema Kijiji hicho kimekuwa kikikumbwa na vurugu za kisiasa kila baada ya kumalizika kwa uchaguzi tokea mwaka 1985
ulipoanza mfumo wa vyama vingi vya kisiasa hali inayopelekea wanachaka wa chama cha Mapinduzi wa maeneo hayo kuwa katika mazingira ya hatari
ya maisha na mali zao.
Muathirika huyo wa hujuma za Kisiasa aliipongeza Serikali kwa juhudi iliyochukuwa ya kuviamrisha vyombo vya ulinzi kufuatilia matukio ya hujuma hizo na kuchukuwa hatua za kisheria dhidi ya wahusika wa matukio hayo.
Alisema yeye pamoja na wenzake wamefarajika na ujio wa viongozi wao wakiwemo Wakuu wa Mikoa, Wilaya na Maafisa wao kuwapa misaada mbali mbali ya kiutu iliyorejesha matumaini kwao na familia zao.
Naye Sheha wa shehia ya Maziwang’ombe akiwa miongoni mwa wananchi waliofanyiwa hujuma hizo Bibi Asha Yussuf Hassan alimueleza Makamu
wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif kwamba baadhi ya wananchi wa shehia hiyo wanaendelea kukabiliwa na tatizo la kutengwa kutokana na itikadi za kisiasa.
Bibi Asha alisema wapo wafanyabiashara ambao wanafanya biashara kwa kuzingatia mfumo wa kibaguzi kinyume na kanuni na taratibu zilizowekwa
na Halmashauri za Wilaya zinazowaelekeza kutoa huduma kwa jamii bila ya upendeleo.
Akitoa ufafanuzi katika ziara hiyo Mkuu wa Wilaya ya Micheweni Nd. Abeid Juma alimueleza Balozi Seif baadhi ya hatua zilizoanza kuchukuliwa na Serikali ya Wilaya hiyo kupitia Halmashauri yake.
Nd. Abeid akiuongoza ujumbe wa Kamati ya Ulinzi na Usalama pamoja na Halmashauri ya Wilaya ya Micheweni tayari wameshakutana na wafanyabiashara wote kuwaonya kuacha tabia ya kuwabagua wananchi wakati wanapofanya biashara zao.
Alisema Uongozi wa Wilaya hiyo umeshatoa onyo kali mbele ya kikao hicho kwamba hautasita kumchukulia hatua kali na za kisheria mfanyabiashara ye yote atakayeamuwa kufanya biashara kwa misingi ya
ubaguzi ikiwemo kumnyang’anya leseni ya biashara.
Mapema asubuhi Makamu waPili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi aliitembelea Hospitali ya Abdulla Mzee iliyopo Wilaya ya Mkoani inayoendelea kujengwa ya kisasa kwa msaada wa Serikali ya Jamuhuri ya Watu wa China.
Katika ziara hiyo Balozi Seif alionyesha kuridhika kwake na hatua iliyofikiwa ya muendelezo wa ujenzi huo unaoleta matumaini makubwa kwa wananchi wa Wilaya ya Mkoani, Mkoa wa Kusini na Kisiwa kizima cha Pemba ya kupata huduma bora za afya.
Mwakilishi wa wahandisi wa ujenzi wa Hospitali hiyo Bwana Zhang Dou alisema ujenzi huo unatazamiwa kukamilika baada ya miezi mitatu ijayo na inatarajiwa kukabidhiwa kwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar mwishoni mwa Mwezi wa Augasti mwaka huu.
Bwana Zhang alisema wagonjwa wapatao 130 wanaweza kulazwa kwa wakati mmoja kwenye Hospitali hiyo zikiwemo huduma zote muhimu kama vyumba Vitatu vya upasuaji, chumba cha wagonjwa mahututi (ICU), Wodi ya wazazi pamoja na jengo la msikiti litakalotumiwa na wagonjwa pamoja na
familia zao kwa ajili ya inbada.
Hospitali hiyo inayojengwa katika mfumo wa teknolojia ya kisasa utakaokuwa na uwezo wa kutoa huduma mbali mbali ikiwemo zile za upasuaji mkubwa, uchunguzi wa maradhi mbali mbali itaweza kukidhi mahitaji ya huduma za Kiafya kwa wancchi walio wengi ndani ya Visiwa vya Zanzibar pamoja na uykanda wa mwambao wa Tanzania.










No comments:
Post a Comment