Waziri Ummy
Mwalimu.
Na Jacquiline Mrisho - Maelezo
WIZARA ya Afya, Maendeleo ya
Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto imetoa tahadhari juu ya ugonjwa wa homa ya
manjano ambao umethibitika kuwepo nchi ya jirani ya Kenya.
Tahadhari hiyo imetolewa leo Jijini
Dar es salaam na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy
Mwalimu alipokua akiongea na waandishi wa habari kuhusu mwenendo wa ugonjwa wa kipindupindu
nchini ambapo katika wiki ya tarehe 14 Machi hadi 20 Machi mwaka huu takwimu
zinaonyesha kuwa kati ya Mikoa 13 yenye wagonjwa wa kipindupindu , jumla ya wagonjwa 738 na vifo 16 vimeripotiwa huku Mkoa wa Manyara ukiongoza kwa kuwa na wagonjwa
wengi wa kipindupindu.
Akielezea kuhusu ugonjwa wa homa ya
manjano,Waziri Ummy Mwalimu amesema kuwa ugonjwa huu unasababishwa na virusi
ambavyo huenezwa na mbu aina ya Aedes na baadhi ya dalili zake ni homa, kuumwa
kichwa,maumivu ya misuli na mgongo,kupoteza hamu ya kula pia kutoka damu sehemu
za mwili zilizo wazi.
“Wizara inapenda kutoa tahadhari ya ugonjwa
wa homa ya manjano kwa wananchi wote na hasa wanaokaa mipakani mwa nchi ya
Kenya kwa kuwa ugonjwa huu hauna tiba kamili ila una chanjo, mgonjwa anatibiwa
kutokana na dalili zinazojitokeza ikiwa ni pamoja na kupewa dawa za kushusha
homa, maumivu, kuongezewa maji mwilini kwa kunywa au kuwekewa dripu”alisema
Waziri Ummy.
Aidha, Waziri Ummy amewaagiza Waganga
Wakuu wa Mikoa na Wilaya zote nchini kupambana na magonjwa ya kuambukiza kwa
kuimarisha mfumo wa ufuatiliaji wa
wagonjwa na utaratibu wa utoaji taarifa za magonjwa ya kuambukiza, kuhakikisha
wasafiri wanaoingia na kutoka nchi zenye hatari ya ugonjwa huo wanapewa chanjo
kabla ya kuingia nchi nyingine, kutoa elimu ya afya kwa wananchi, kuandaa timu
za wataalam, vifaa tiba na chanjo za kutosha ili kuweza kukabiliana na ugonjwa
huo endapo utajitokeza nchini kwa kusimamia na kuhimiza usafi wa mazingira na
kuzingatia kanuni za afya.
Pia, amewaonya maofisa wanaotoa chanjo
ya homa ya manjano walioko katika vituo vya Afya vya kupokelea wageni
wanaoingia na kutoka nchini kuacha mtindo wa kupokea rushwa na kuwapitisha watu
bila kupatiwa chanjo.
Mwisho, ametoa wito kwa wananchi kuchukua
tahadhari na kushirikiana kwa karibu na wataalamu wa afya walioko katika maeneo
yao kwa kutoa taarifa haraka kwenye
uongozi husika endapo kuna mgonjwa mwenye dalili za kipindupindu au homa ya
manjano.
No comments:
Post a Comment