Mkurugenzi wa Uchaguzi wa Tume ya Taifa (NEC), Kailima
Ramadhani.
Na Clarence Nanyaro- NEC
TUME ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), imesema haitambui
kujitoa kwa Chama cha Wananchi (CUF), katika uchaguzi wa Mbunge Jimbo la
Kijitoupele hapa Zanzibar unaotarajiwa kufanyika Jumapili licha ya kuwa Tume imepokea
barua rasmi toka kwa uongozi wa Chama hicho.
Mkurugenzi wa uchaguzi wa Tume ya Taifa Bw. Kailima
Ramadhani amesema Tume imefikia maamuzi hayo kutokana na ukweli kuwa barua hiyo
ya CUF imechelewa huku maandalizi ya uchaguzi
huo yakiwa yamekamilika na ni Wananchi tu kwa sasa Wanasubiriwa kwenda kupiga kura.
Aidha, Bw. Kailima ameeleza kuwa, kwakuwa karatasi
za kupigia kura zilishachapishwa na kuwasili hapa nchini tayari kwa uchaguzi huo,
zitaendelea kuwa na picha za Wagombea wa CUF hata kama wamejitoa katika uchaguzi
huo.
Awali, wajumbe wa Tume ya Taifa ya uchaguzi wakiongozwa
na Makamu Mwenyekiti wa Tume Jaji mstaafu Hamid Mahamood Hamid walitembelea katika
vituo mbalimbali vya kupigia kura katika Jimbo la Kijitoupele ili kujiridhisha na
maandalizi ya uchaguzi huo kabla ya uchaguzi kufanyika jumapili.
Tume ilibaini kuwepo kwa baadhi ya kasoro ndogo ndogo
katika baadhi ya vituo vya kupigia kura ikiwa ni pamoja na kubanduliwa kwa karatasi
zenye majina ya wapiga kura, mfano katika kituo cha Skuli ya sekondari Kinuni.
Jimbo la Kijitoupele lina jumla ya Wapiga kura wapatao
17,274 na vituo vipatavyo 53 vitatumiwa na wapiga kura ili kumchagua mbunge waJimbo
la Kijitoupele siku ya Jumapili.
Sambamba na Uchaguzi wa ubunge katika Jimbo la
Kijitoupele, marudio ya uchaguzi mkuu wa Zanzibar Oktoba 25,2015 ambayo matokeo
yake yalifutwa uatafanyika Jumapili hiyo pia.
Uchaguzi katika jimbo la Kijitoupele uliahirishwa mwaka
jana kutokana na hitilafu ndogo ndogo zilizojitokeza katika karatasi za kupigia
kura, kabla ya kufutwa kwa matokeo ya Uchaguzi mkuu wa Zanzibar uliofanyika Oktoba
25, 2015.

No comments:
Post a Comment