Waziri
wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy mwalimu
akizungumza na viongozi na baadhi ya wazee wa mkoa wa Dar es Salaam katikati
ni Mwenyekiti wawazee hao Mzee hemed Mkali na kulia ni Katibu wa wazee hao
Mzee Mohamed Mtulia.
Na Raymond Mushumbusi
MAELEZO
Dar es Salaam
23/03/2016
SERIKALI
imeazimia kuanzisha Mfuko wa Wazee utakaowasaidia kupambana na changamoto
zinazowakabili kwa kuwawezesha kiuchumi.
Akitoa
azimio hilo mbele ya viongozi na baadhi ya wazee wa mkoa wa Dar es
Salaam,Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy
Mwalimu alisema Wizara imeazimia kuanzisha mfuko huo utakaowasaidia wazee
nchini ili waweze kujikwamua kiuchumi.
“Wazee
bado wanaweza kuchangia katika maendeleo ya taifa kama watashirikishwa katika
kuendesha sekta mbalimbali kwani bado tunahitaji ujuzi na mchango wao katika
kusongesha mbele gurudumu la maendeleo ya nchi yetu” alisema Mhe. Ummy.
Waziri
Ummy ameongeza kuwa mfuko huo utawasaidia wazee kupata na kuongeza kipato chao kwa
kufanya shughuli mbalimbali za kiuchumi ambazo zitawasaidia kupata huduma bora
za afya.
“Serikali
ya Awamu ya Tano imedhamiria kuwasaidia wazee, nimeshapeleka mapendekezo kwa
kila halmashauri kuanzisha mfuko wa wazee utakaowasaidia kujikwamua kiuchumi
katika maeneo yao” alisema Mhe. Ummy.
Naye
Mwenyekiti wa wazee hao Mzee Hemed Mkali amesema wanahitaji sana mfuko huo ambao
utawawezesha kujishughulisha na kupata kipato na pia kuboresha huduma za afya
ambazo bado ni changamoto kwa wazee nchini.
Aidha,
Waziri Ummy alisistiza kuwa wanashirikiana na Wizara ya Fedha na Mipango ili
kuandaa mpango wa kuanzisha mfuko huo kwa kushirikisha taasisi za kifedha,
makampuni na mashirika mbalimbali katika kuchangia maendeleo ya mfuko huo kwa
maendeleo ya wazee na jamii kwa ujumla.
Wazee
nchini wanakabiliwa na changamoto nyingi zikiwemo upatikanaji wa huduma za afya
na ushirikishwaji wao katika shughuli mbalimbali za kiuchumi na kutoa maamuzi
katika jamii zao ambao idadi yao inakadiriwa kuwa ni asilimia 5.6 ya watanzania
wote.
No comments:
Post a Comment