UDHIBITI WA
UTOROSHAJI NA BIASHARA HARAMU YA MADINI
Moja
ya majukumu ya Wakala wa Ukaguzi wa madini Tanzania (TMAA) ni kufuatilia na
kuzuia utoroshaji/magendo na biashara ya madini unaopelekea ukwepaji wa ulipaji
mrabaha kwa kushirikiana na taasisi nyingine husika za Serikali zikiwemo
Mamlaka ya Viwanja vya Ndege (TAA), Jeshi la Polisi, Idara ya Usalama wa Taifa,
Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na Idara ya Uhamiaji.
Taarifa za matukio ya udhibiti wa utoroshaji
na biashara haramu ya madini zilizopo zinaonesha kuwa katika kipindi cha
kuanzia mwezi Julai 2015 mpaka Januari 13, 2016 kulikuwepo na jumla ya matukio
14 ya utoroshaji wa madini ambapo madini yenye thamani ya Dola za Marekani 1,474,194
milioni (zaidi ya Shilingi bilioni 3,235,856,181) yalikamatwa na
wakaguzi wa Wakala kupitia Madawati ya Ukaguzi yaliyopo katika viwanja vya
ndege vya Dar es Salaam (JNIA), Kilimanjaro (KIA) na Mwanza.
Katika
matukio ya hivi karibuni ya ukamataji wa madini katika viwanja vya ndege, madini
yenye thamani ya jumla ya Shilingi milioni
11,217,300 yalikamatwa na wakaguzi
wa Wakala wa Ukaguzi wa Madini Nchini (TMAA) kwa kushirikiana na vyombo vingine
vya dola.
Raia mmoja wa kigeni na
mwingine wa Tanzania walikamatwa wakiwa na madini hayo bila kuwa na kibali
chochote cha usafirishaji kulingana na Sheria ya Madini ya mwaka 2010. Raia wa
kigeni (jina limehifadhiwa) ambaye alikuwa anasafiri kwenda Bangkok alikamatwa akiwa
na madini aina mbalimbali ikiwemo almasi,
aquamarine, sapphire, green tourmaline, quartz na rhodolite.
Tukio la pili, mtuhumiwa
mwingine ambaye ni raia wa Tanzania aliyekuwa akisafiri kwenda Ujerumani alikamatwa
akiwa na madini mbalimbali ikiwemo amethyst,
moonstone cabochon, rulilated quartz (cabochon),
rulilated quartz(faceted), chrysoprase, green tourmaline, ruby,
red garnet, green quartz, zircon na rhodolite.
Kufuatia Matukio hayo wahusika
wote wamechukuliwa hatua za kisheria ikiwamo kufunguliwa kesi mahakamani.
Wakala unatoa rai kwa Umma kujiepusha na
shughuli za utoroshaji/magendo na biashara haramu ya madini, kwani hatua kali
zitaendelea kuchukuliwa kwa yeyote atakayebainika/kukamatwa akijihusisha na
shughuli hizo. Aidha, madini yatakayokamatwa yakisafirishwa kinyume cha sheria
na taratibu zilizopo yatatafishwa na Serikali.
Aidha, Serikali kupitia Wizara ya Nishati na
Madini inatoa wito kwa yeyote atakayetoa taarifa za utoroshaji/magendo na
biashara haramu ya madini kwa Kamishna wa Madini au Wakala ambazo zitawezesha
ukamataji wa madini, atazawadiwa fedha taslimu ambazo ni sawa na asilimia 5 ya thamani ya madini
yatakayokamatwa na kunadiwa. Kwa mawasiliano ya haraka, wananchi watumie barua
pepe info@tmaa.go.tz na simu 022-2137142 au 022-2601819.
IMETOLEWA NA
DOMINIC RWEKAZA
MTENDAJI MKUU
WAKALA WA UKAGUZI WA MADINI TANZANIA
15 JANUARI, 2016
No comments:
Post a Comment