TANGAZO


Saturday, October 3, 2015

JK kuongoza maelfu kuombea Nchi amani, Uchaguzi Mkuu kesho Jumapili Oktoba 4

*Makhabane, Mahlangu watua kukoleza utamu
Msanii wa nyimbo za Injili raia wa Uingereza, Ifheanyi Kelechi (katikati) , akiwasili leo kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) jijini Dar es Salaam, tayari kutumbuiza katika Tamasha la Amani linalofanyika leo Uwanja wa Taifa Dar. Kulia ni Mkurugenzi wa Msama Promotions wanaoratibu tamasha hilo, Alex Msama. Kushoto ni Mratibu, Hudson Kamoga. (Picha na Francis Dande)

Na Mwandishi wetu
RAIS Jakaya Kikwete kesho Jumapili Oktoba 4 anatarajiwa kuwaongoza maelfu ya watanzania katika Tamasha la kuombea amani Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 25, linalofanyika katika Uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam chini ya uratibu wa kampuni ya Msama Promotions.

Akizungumza jijini Dar es Salaam jana, Mkurugenzi wa Msama Promotions, Alex Msama alisema maandalizi yote yamekamilika ikiwemo kuwasili kwa waimbaji wa kimataifa Sipho Makhabane na Solly Mahlangu kutoka Afrika Kusini na Ifeanyi Kelechi kutoka nchini Uingereza.

Alisema waimbaji hao nguli wa muziki wa injili Afrika, wamekuja kuungana na wengine mahiri wa hapa nchini kupamba Tamsha hilo la kihistoria litakalohudhuriwa na viongozi wa kiroho wa ndani na nje ya nchi wakiwamo wachungaji zaidi ya 200 na maaskofu 50.

“Hili ni tukio la aina yake kwani tunaingia katika kipindi kigumu cha uchaguzi mkuu unaotarajiwa kuwa na ushindani mkubwa pengine kuliko yote iliyopita, hivyo tuna kila sababu ya kumtanguliza Mwenyezi Mungu, tuweze kuvuka salama,” alisema Msama.

Alisema lengo la kuandaa Tamasha hilo ni kutokana na kutambua umuhimu wa tunu ya amani kwa ustawi wa nchi iwe kijamii hata kiuchumi na kuongeza kuwa amani iliyopo inapaswa kulindwa na kila mmoja kwa nafasi yake.

Msama alisema kwa vile Mungu ni wa wote bila kujali dini, jinsia wala kabila na amekuwa akisikia maombi ya watu wake na kuyajibu, wananchi hawana budi kujitokeza kwa wingi katika tamsha hilo  kuomba nchi ivuke salama katika uchaguzi huo wa Oktoba 25.

Kwa upande wa buruidani, mbali ya Mahlangu na Makhabane kutoka Afrika Kusini, waimbaji wengine wanaotarajiwa kupamba tamasha hilo ni Ephraem Sekeleti kutoka Zambia, Sarah K kutoka Kenya na Solomon Mukubwa, raia wa DR Congo anayeishi nchini Kenya.

Waimbaji wa Tanzania, ni Rose Muhando, Upendo Nkone, Jesca BM, Martha Mwaipaja, Christopher Mwahangila, Bonny Mwaitege, John Lissu, Kwaya ya Uinjilisti Kijitonyama, St. Andrew Anglican ya Dodoma na AIC Chang’ombe ya jijini Dar es Salaam.

Msama alisema viingilio kwa viti maalumu ni shilingi 5,000, jukwaa kuu shilingi 3,000 kwa wakubwa na watoto watalipa shilingi 1,000 na kuongeza ameweka kiwango hicho kutoa nafasi wengi kushuhudia na baada ya uwanja wa Taifa, litahamia katika mikoa mingine.

CHADEMA WALONGA 
Kwa kutambua umuhimu wa amani kwa mustakabali wa taifa, Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimepongeza uwepo wa tamasha hilo na kusema litumike pia kumwombea Rais Kikwete akubali kuyapokea matokeo ya aina yoyote yatakayoamuliwa na wananchi kupitia sanduku la kura.

Akizungumza jijini Dar es Salaam jana, Kaimu Katibu Mkuu wa Chadema, John Mnyika alisema wanatoa angalizo hilo kutokana na baadhi ya viongozi wa chama tawala (CCM) kwa nyakati tofauti kusema hawatakubali kuachia upinzani Ikulu.

Mnyika amesihi Tamasha hilo litumike pia kuombea Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) chini ya Jaji Mstaafu, Damian Lubuva, isimamie uchaguzi huo kwa mujibu wa sheria na taratibu ili uweze kuwa wa huru na haki.

No comments:

Post a Comment