TANGAZO


Sunday, August 16, 2015

Tamasha kuuombea Uchaguzi Mkuu kufanyika Septemba 4 jijini Dar es Salaam

Mkurugenzi Mkuu wa Msama Promotions, Alex Msama, akizungumza na waandishi wa habari, Dar es Salaam leo, kuhusu Tamasha la kuombea Tanzania kuelekea Uchaguzi Mkuu ujao, Oktoba 25, mwaka huu, litakalofanyika jijini Dar es Salaam Septemba 4 na kisha kuendelea Mikoa mingine minne nchini. (Picha zote na Kassim Mbarouk-www.bayana.blogspot.com)
Mkurugenzi Mkuu wa Msama Promotions, Alex Msama, akielezea jambo, wakati alipozungumza na waandishi wa habari, Dar es Salaam leo, kuhusu Tamasha la kuombea Tanzania kuelekea Uchaguzi Mkuu ujao, Oktoba 25, mwaka huu, litakalofanyika jijini Dar es Salaam Septemba 4 na kisha kuendelea Mikoa mingine minne nchini.  
Mkurugenzi Mkuu wa Msama Promotions, Alex Msama, akijibu maswali ya waandishi wa habari, Dar es Salaam leo, wakati alipozungumza nao, kuhusu Tamasha la kuombea Tanzania kuelekea Uchaguzi Mkuu ujao, Oktoba 25, mwaka huu, litakalofanyika jijini Dar es Salaam Septemba 4 na kisha kuendelea Mikoa mingine minne nchini. 

Na Mwandishi wetu
KAMPUNI ya Msama Promotions imeandaa Tamasha la kihistoria ambalo halijawahi kufanyika tangu kupatikana Uhuru wa nchi hii, mwaka 1961, la kuiombea Tanzania inayoelekea katika Uchaguzi Mkuu, unaotarajiwa kufanyika Oktoba 25, mwaka huu.

Akizungumza jijini Dar es Salaam leo, Mkurugenzi wa Kampuni ya Msama Promotions Alex Msama, alisema kuwa tamasha hilo, ambalo litafanyika Oktoba 4 jijini, litazunguka katika Mikoa mikubwa minne, ambayo itatajwa hapo baadaye.

Msama alisema tamasha hilo, linatarajia kushirikisha waimbaji mbalimbali wa nyimbo za Injili wa ndani na nje ya nchi, ambao wanatamba katika tasnia ya muziki huo.

“Watanzania wajiandae kuiombea amani Tanzania kupitia muziki wa Injili, lengo kubwa likiwa ni kuivusha nchi yetu na machafuko kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi mkuu, uchaguzi wenyewe, pamoja na siku ya kutangazwa matokeo yenyewe", alisema

Msama alisema kuwa waimbaji mbalimbali wa kutoka nje ya Tanzania watashiriki katika tukio hilo muhimu, ambalo alisema hadi sasa bado wako katika mchakato wa mahali litakapofanyika.

“Tamasha hilo kubwa kimaudhui linakaribia tamasha kubwa la Kusifu na Kuabudu la Pasaka, ambalo hufanyika kila mwaka,” alisema Msama.

Aidha, Msama aliongeza kuwa baada ya tamasha hilo, kufanyika jijini Dar es Salaam, watahamishia maombi hayo, katika majiji mengine manne, lengo likiwa ni kuombea uchaguzi huo Mkuu na nchi kwa ujumla.  

Alizitaja nchi watakazotoka waimbaji hao, watakaosindikiza maombi hayo, kuwa ni pamoja na Afrika Kusini, Rwanda, Kenya, Uganda, Zambia, Burundi na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).

No comments:

Post a Comment