TANGAZO


Sunday, May 24, 2015

Wanachama CUF wahimizwa kujitokeza kugombea nafasi ya uteuzi wa Urais Zanzibar

Mkurugenzi Mipango wa CUF, Omar ali shehe

Na Mwinyimvua Nzukwi, Zanzibar
CHAMA cha wananchi CUF kimewataka wanachama wake wenye sifa za kugombea urais wa Zanzibar kujitokeza kugombea uteuzi wa nafasi hiyo katika mchakato wa uchaguzi unaoendelea ndani ya chama hcho.

Akitangaza ratiba ya mchakato huo katika ofisi za chama hicho wilaya ya mjini unguja Vuga, Mkurugenzi Mipango Omar Ali Shehe alisema zoezi la uchukuaji na ureshaji wa fomu litaanza kesho (Jumatatu 25/5/2015) na kukamilika Mei 31 mwaka huu.

Alisema wanachama hao wanapaswa kujipima na kuzingatia matakwa ya katiba na kanuni za uchaguzi za chama hicho sambamba na katiba ya nchi kabla ya kwenda kuchukua fomu hizo zitakazokuwa zinatolewa katika ofisi za makatibu wa wilaya za chama hicho.

Shehe ambaye pia ni mjumbe wa Baraza la Wawakilishi kutoka jimbo la Chake chake Pemba aliwataka wanachama hao kuitumia vyema fursa hiyo ili kuepusha kasumba zinazotolewa na baadhi ya vyama kuwa nafasi ya kugombea urais ndani ya chama hicho haitolewi bali ni maalum kwa kiongozi mmoja tu.

“Chama kinachofanya ni kutoa fursa na wanachama wenyewe ndio wenye maamuzi ya kugombea au kuacha lakini sisi kama chama tunawahamasisha kuitumia vyema fursa hii ili kuonesha jinsi CUF ilivyo na demokrasia ya kweli”, alisema Shehe.

Alizitaja baadhi ya sifa za msingi za mgombea wa nafasi hiyo kuwa ni pamoja na kuwa mwanachama hai wa chama chao pamoja na kukidhi masharti ya katiba ya Zanzibar ya 1984 pamoja na kulipia ada ya sh. laki tano (500,000/=)  ambayo alidai imepunguzwa kwa lengo la kutoa nafasi kwa wanachama wengi kutumia haki yao ya kuchaguliwa.

Aidha alisema mara baada ya kukamilika kwa hatua hiyo waombaji wote watapelekwa katika vikao vya kamati tendaji ya chama hicho ambavyo vitapendekeza majina matatu kwa baraza kuu la chama hicho kwa ajili ya uteuzi kabla ya kupeleka jina la mgombea aliyeteuliwa kwa ajili ya kuidhinishwa.

Akizungumzia uwepo wa makundi yanayomuunga mkono Katibu Mkuu wa chama hicho Maalim Seif Sharif Hamad, shehe alisema chama chake kinaheshimu maamuzi ya wanachama wao na kamwe hawawafungi mikono kuonesha hisia zao kwa mtu wanayeona anawafaa na jambo hilo halijakatazwa kama ilivyo katika vyama vingine vya siasa.

Akizungumzia maendeleo ya mchakato wa upatikanaji wa wagombea wa ubunge na uwakilishi, shehe alisema hatua za awali zimekamilika na hatua zilizobakia sasa ni kufanyika kwa vikao vya maamuzi.

“vikao vya uchaguzi wa wagombea ubunge na uwakilishi wa majimbo na viti maalum umeshafanyika na sasa tunasubiri maamuzi ya vikao vya baraza kuu ambalo litapokea matokeo ya chaguzi hizo kama mapendekezo”, alisema Mkurugenzi huyo.

Hatua hiyo imekuja baada ya chama hicho kukamilisha mchakato wa awali wa upatikanaji wa wagombea wa nafasi za uwakilishi na ubunge huku kumbu kumbu zikionesha ya kuwa toka 1995 ni mara moja tu kati ya tatu ambazo chama hicho kimeshiriki uchaguzi mkuu ambapo maalim seif alikuwa akiwa ni mgombea pekee.

Katika hatua nyengine Shehe alieleza kuwa chama chake kimesikitishwa na hatua ya jeshi la polisi kukataa kuwapa dhamana wanachama wa chama hicho Said Ali Said (26) na Hussein Mageni Hussein (27) wanaotuhumiwa kwa makosa ya kutoa kauli za uchochezi na matusi dhidi ya Rais wa Zanzibar, Makamo wa pili wa Rais wa Zanzibar na jeshi la polisi.

Alisema hatua ya jeshi hilo inaonesha ni jinsi gani taasisi hiyo ya dola isivyoheshimu haki za raia na kwa imekuwa ikifanya kazi zake kwa upendeleo jambo ambalo slinapaswa kuepukwa.

“Kama hoja ni matusi, tumekuwa tukiyasikia matusi yakitolewa dhidi ya Makamo wa Kwanza wa Rais Maalim Seif Sharif Hamad bila ya polisi kuchukua hatua yoyote lakini vijana wale ambao waliokuwa wakitoa maoni yao na tahadhari juu ya hali ya nchi na utendaji wao, wamekuwa wakosa”, alisema.

Mapema wiki hii, Naibu Mkurugenzi wa Makosa ya jinai, Kamishna Msaidizi wa polisi (DCI) Salum Msangi alisema kuwa jeshi hilo, limewakamata vijana hao waliokuwa wakitoa maneno ya vitisho, dharau na uchochezi na kisha kusambaza kwa njia ya mitandao ya kijamii, huku mmoja wa watuhumiwa hao (Beko), akidaiwa kumtukana makamo wa Pili wa Raisi, Balozi Seif Ali Iddi na kumtolea matusi ya nguoni.

No comments:

Post a Comment