Mamilioni ya watu watakuwa wakipiga kura katika uchaguzi mkuu wa Uingereza leo Alhamisi
Vituo vya kupigia kura karibu 50,000 nchini kote vitafunguliwa saa moja asubuhi kwa saa za Uingereza.
Jumla ya wabunge 650 watachaguliwa kuingia bunge la nchi hiyo, kukiwa na watu karibu milioni 50 waliojiandikisha kupiga kura.
Kama ilivyo kwa uchaguzi mkuu, kuna viti zaidi ya 9,000 vya madiwani vinavyogombewa katika serikali za mitaa 279.
Mameya pia watachaguliwa katika miji ya Bedford, Copeland, Leicester, Mansfield, Middlesbrough na Torbay.
Hii ina maana kuwa karibu kila mpiga kura wa England, ukiondolewa mji wa London ambako hakuna uchaguzi wa serikali za mitaa, atapewa karatasi mbili za kupigia kura watakapofika katika kituo cha uchaguzi.
Baadhi ya kura tayari zimekwishapigwa kupitia vituo vilivyoko nje ya Uingereza kwa kutuma kura kwa njia ya posta. Kura hizi zilikuwa ni asilimia 15% ya kura zilizopigwa katika uchaguzi mkuu wa 2010 wakati watu waliojitokeza walikuwa asilimia 65%.
Masanduku ya kupigia kura yamepelekwa katika vituo vya uchaguzi.
Kwa mara ya kwanza, watu waliweza kujiandikisha kupiga kura kupitia njia ya mtandao.
Vituo vingi vya kupigia kura viko katika majengo ya shule, kumbi za vituo vya kijamii na kwenye kumbi za parokia, lakini migahawa, maeneo ya kufua na kunyosha nguo na basi la shule pia vitatumika kama vituo vya kupigia kura.
Vituo vya kupigia kura vitafungwa saa nne usiku kwa saa za Uingereza, lakini maafisa wa uchaguzi wamesema mtu yeyote ambaye atakuwa kwenye mstari kufikia wakati huo ataweza kupiga kura yake.
BBC itatangaza moja kwa moja kuanzia saa tatu na dakika 55 usiku shughuli za uchaguzi katika kaunti 220.
Matangazo kamili kuhusu matokeo yanavyopokelewa yatakuwa katika ukurasa wa mtandao wa BBC politics online live na katika sehemu ya mbele ya ukurasa wa uchaguzi, ikiwa ni pamoja na taarifa zote mpya kutoka sehemu mbalimbali nchini na uchambuzi wa waandishi wa habari.
No comments:
Post a Comment