Makamu Mwenyekiti wa CUF, Juma Duni Haji, akizungumza wakati akimkaribisha Mwenyekiti wake, Profesa Ibrahim Lipumba (katikati), kukifungua kikao cha kawaida cha Baraza Kuu la Uongozi la chama hicho, Dar es Salaam leo. Kulia ni Katibu Mkuu wa chama hicho, Makamu wa Kwanza wa Rais Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad.
Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba, akisisitiza jambo wakati alipokuwa akikifungua kikao cha kawaida cha Baraza Kuu la Uongozi la chama hicho, Dar es Salaam leo. Kushoto ni Makamu Mwenyekiti wa CUF, Juma Duni Haji na kulia ni Katibu Mkuu wa chama hicho, Makamu wa Kwanza wa Rais Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad.
Baadhi ya waandishi wa habari na wajumbe wa Baraza Kuu la Uongozi la Chama cha Wananchi (CUF), wakiwa katika ufunguzi wa kikao cha kawaida cha baraza hilo, Dar es Salaam leo.
Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba, akizungumza wakati alipokuwa akikifungua kikao hicho jijini leo.
Na Mwandishi wetu
CHAMA cha Wananchi (CUF), kimesema Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) ipo njia panda kuhusiana na namna Uchaguzi Mkuu utakavyofanyika mwaka huu.
Hiyo imetokana na kushindwa kukamilisha mchakato wa uandikishaji wananchi katika daftari la kudumu la wapiga kura kwa muda ulipangwa.
Akizungumza leo jijini Dar es Salaam, wakati akikifungua kikao cha kawaida cha Baraza Kuu la Uongozi la Chama cha Wananchi (CUF), Mwenyekiti wa chama hicho, Profesa Ibrahim Lipumba, alisema hali hiyo, imetoakana na tume hiyo kutokuwa na vifaa vya kutosha vya BRN ambavyo vingetumika kukamilisha zoezi hilo.
Alisema kuwa NEC, imekuwa ikitoa taarifa za mabadiliko kila mara kuhusu mchakato mzima wa uandikishaji, lakini hadi sasa hata mkoa mmoja haujamalizika huku ikiwa imebakia miezi mitano kuingia katika uchaguzi.
Prof. Lipumba alisema kutokana na kusuasua huko ni wazi NEC inaweka mchakato wa uchaguzi huo gizani jambo ambalo halikubaliki.
Alisema jambo la kusikitisha ni kuona NEC ikiwa na kigugumizi katika kutoa taarifa halisi za hatua ambayo imefikia hasa kuhusu kuchelewa kwa vifaa vya Biometrick Voters Registration (BVR), kwani vimekwamisha mchakato mzima wa uandikishaji.
"Unajua hali ya sintofahamu inayonekana katika kipindi hiki cha uchaguzi mkuu sababu kubwa NEC ndiyo inahusika lakini imeshindwa kuwa wazi na kuiacha Serikali kupitia rais na waziri mkuu wakitoa matamko wakati sheria inakataza,".
Lipumba alimtaka Mwenyekiti wa NEC kusimamia misingi ya kazi yake na kama ameshindwa aachie watu wengine waendeleze gurudumu hilo kwa maslahi ya Taifa.
Alisema ni vema Serikali ikapeleka marekebisho katika katiba hasa vipengele ambavyo Kituo cha Demokrasia Tanzania (TCD), kilikubaliana na Rais Jakaya Kikwete.
Mwenyekiti huyo alisema TCD walimuomba kuhakikisha Katiba inaruhusu mgombea binafsi, kuhoji ushindi wa rais, ushindi wa rais uwe kwa zaidi ya asilimia 50 na uwepo wa Tume Huru ya Uchaguzi.
Alisema iwapo marekebisho hayo yatafanyika ni wazi uchaguzi utafanyika na mchakato wa kura ya maoni kusubiri hadi mwakani.
Lipumba alisema CUF inalaani vitendo vya kigaidi ambavyo vinafanywa na kundi la Al Shabaab nchini Kenya kwani ni vya kusikitisha na kuhatarisha maisha ya wananchi wasio kuwa na hatia.
No comments:
Post a Comment