TANGAZO


Wednesday, April 1, 2015

Bungeni leo Mjini Dodoma

Bunge la Pitisha Sheria ya Kuanzishwa Baraza La Vijana

Waziri wa Habari Vijana Utamaduni na Michezo Mhe. Fenella Mukangara akisoma Muswada wa Baraza la Vijana ndani ya ukumbi Bunge, Mjini Dodoma. (Picha na Anitha Jonas – MAELEZO, Dodoma)

Na Anitha Jonas – MAELEZO,Dodoma.
SERIKALI inatarajia kuanzisha Baraza la Vijana litakalo kuwa chombo cha vijana kitakacho waunganisha Kitaifa bila kujali itikadi zao za Kisiasa,Imani zao za Kidini  wala tofauti zao za Rangi,hayo yamesemwa na Waziri wa Habari,Vijana,Utamaduni na Michezo Mhe.Fenella Mukangara alipokuwa akisoma Muswada wa Sheria ya Baraza la Vijana Tanzania Bungeni Mjini Dodoma.

Mheshimiwa Mukangara aliendelea kusema Baraza hilo litaisaidia Serikali kuweza kuwafikia vijana kwa urahisi na kusikiliza shida zao pamoja na kutoa ufumbuzi wa hoja mbalimbali za vijana.Hata hivyo  chimbuko la Muswada huo ni katika kutekeleza Sera ya Taifa ya Maendeleo ya Vijana ya 2007,Ibara ya 3 Sehemu ndogo ya 11 inayosema kwa uwazi Serikali itawezesha kuundwa kwa Baraza Baraza la Vijana na kuanzisha mfumo wa kisheria ili kuliwezesha kufanya kazi.

“Madhumuni ya Muswada huu ni Kutunga Sheria ya Baraza la Vijana Tanzania(The Youth Council of Tanzania 2015) ili kuwa na chombo cha Kitaifa cha kuwewezesha vijana kujadili masuala yao,kutambua majukumu yao,kukuza maadili mema,kukuza moyo wa umoja ,uzalendo,uwajibikaji na kujitolea kwa malengo chanya miongoni mwao katika nchi yetu,”alisema Mhe.Mukangara.

Mbali na hayo katika sehemu ya pili kifungu cha 4-15 cha Muswada huo unaeleza juu ya masharti mbalimbali kuhusu Uanzishwaji,Uanachama,Muundo na kazi za Baraza.Pia sehemu hii imefafanua Mamlaka ya Baraza na vyombo vya utendaji katika ngazi ya Taifa,Mkoa na Wilaya.

Aidha, kwa upande wa maoni ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Maendeleo ya Jamii yaliyosomwa na Mwenyekiti wake Said Mtanda aliishauri Serikali katika kifungu cha 4(3)Kisomeke Uanachama utakuwa na uwazi na hiari kwa kijana yeyote mwenye umri  wa kuanzia miaka 15 mpaka 35.Pia kifungu cha 4(4) imeeleza kuwa baraza halitakuwa kisiasa liongezwe neno halitakuwa na Itikadi za Kidini.

Katika kipindi cha majadiliao ya Muswada huo naye Mhe.Kuluthum Mchuchuri  (Mb) Viti Maalum CUF aliipongeza Serikali kwa mchakato wake mzuri wa kuandaa Baraza la Vijana litakalo saidia vijana kujadili matatizo yao na kuyawasilisha Serikali kwa kupatiwa ufumbuzi kwa urahisi,pia ameishauri Serikali katika suala la wajumbe  uwawakilishi waanze kuanzia ngazi ya Kata na Serikali pia iweke wazi ni kwa utaratibu gani wawakilishi hao watapatikana.

Naye Mhe.Magret Sitta Mbunge wa Viti Maalum CCM aliiomba Serikali kuandaa ziara kwenda kuangalia mabaraza ya Vijana katika  nchi za wenzetu yanafanyaje kazi na kujifunza,pia aliendelea kuiomba Serikali itoe mafunzo mbalimbali ya ufundi kwa kushirikia na taasisi ya Veta na Vyuo vya Wananchi ilikuwapatia elimu itakayo wasaidia vijana kujikwamua kiuchumi na kupunguza idadi ya vijana wa vijiweni.

Pamoja na hayo naye Mbunge wa Kasulu Mjini (NCCR) Mhe. Moses Machali alishauri Serikali Kuanzisha asasi moja ambayo vijana watakayo jiunga huko ili kudhibiti uanzishwaji wa asasi bandia kwa watu wenye nia ya kujinufaisha,pia aliipongeza Serikali kwa kuleta Muswada huo kwani unamanufaa Makubwa kwa vijana.

Aidha,mbali ya kuwepo na marekebisho mbalimbali ya Muswada huo Serikali iliyapokea maombi ya Suala la Baraza hilo kuanzia katika ngazi ya Kata ilikupata uwakilishi uliyowa uhakika na baraza likalete manufaa kwa kuanzia ngazi ya chini ambapo ndipo vijana wengi wanapatikana na jamii inawafahamu kwa usahihi zaidi.


Halikadhalika Serikali iliridhia kuanzishwa kwa uwakilishi wa vijana watano kutoka kundi maalum kwa maana ya wenye ulemavu na ili kuweka uwianao wa vijana hawa kuweza kuwasilisha maombi yao kwa Serikali kwa urahisi huku ikizingatia mahitaji yao maalum. 

Matokeo ya Tafiti kuondoa adha ya 
wanawake watumia kuni
Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano), Mhe. Stephen Masele.

Na Johary Kachwamba - MAELEZO, DODOMA
TAFITI mbalimbali zimefanyika na zinaendelea kufanyika ili kupata majiko mbadala yasiyotumia nishati ya kuni hapa nchini.

Hayo yamesemwa na Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano), Mhe. Stephen Masele wakati akijibu swali la msingi la Mhe. Amina Makilagi, Mbunge wa Viti Maalum iliyehoji matumizi ya tafiti za kupata majiko mbadala.

“Tafiti hizi zinahusu matumizi ya gesi inayotokana na kinyesi cha mifugo, matumizi ya gesi asilia, matumizi ya nishati itokanayo na mimea, matumizi ya makaa ya mawe, tungamotaka na majiko yanayotumia kiasi kidogo cha kuni na mkaa” alisema Mhe. Masele.

Alisema baadhi ya taasisi zinazofanya utafiti huu ni pamoja na Chuo Kikuu cha Dar-es-salaam, Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine, COSTECH, CARMATEC, MIGESADO na TaTEDO.

Mhe. Masele amesema Serikali imekuwa ikitumia matokeo ya tafiti hizi katika utekelezaji wa miradi ya hifadhi ya mazingira kama vile Mradi wa Hifadhi ya Mazingira wa Ziwa Tanganyika ambao umewezesha baadhi ya taasisi za Magereza, JKT, Shule za Sekondari na Vyuo vya Ualimu na Wananchi kutumia majiko hayo katika mikoa ya Katavi, Rukwa na Kigoma.

Aidha Serikali kupitia Mradi wa Kuhimili Mabadiliko ya Tabianchi katika maeneo ya Pwani unaotekelezwa katika mikoa ya Pwani na Dar-es-salaam kwa mwaka wa fedha 2014/2015 itasambaza majiko 1500 kwa kaya na kutoa mafunzo ya matumizi ya majiko hayo katika Wilaya za Ilala, Temeke na Kinondoni.

“napenda kuhimiza taasisi na wananchi kutumia majiko yanayotokana na tafiti hizi ili kupunguza matumizi makubwa ya kuni na mkaa, na pia kuondoa adha kwa wanawake ya kutafuta kuni, kupunguza athari kwa afya zao na pia kuchangia katika hifadhi ya Mazingira” alisisitiza Mhe. Masele.

Serikali kwa kushirikiana na taasisi binafsi imeendelea kusambaza technolojia hii na kutoa elimu ya matumizi ya majiko haya kupitia vyombo vya habari, maonyesho na maadhimisho ya na Siku ya Mazingira Duniani.


Spika atoa  Ufafanuzi juu ya Muswada wa Binafsi wa Mhe. John Mnyika

Spika wa Bunge la Tanzania Mhe. Anne Makinda 

Na Anitha Jonas-MAELEZO, Dodoma.
SPIKA wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Anne Makinda ametoa ufafanuzi juu ya suala la Muswada binafsi wa Baraza la Vijana uliyowasilishwa  na Mhe. John Mnyika Mbunge wa Ubungo (CHADEMA) hapo mwaka jana.

Mhe.Makinda alisema Ofisi yake  inataratibu zinazofuatwa katika  uwasilishwaji wa Miswada bungeni na Kamati ya Bunge ya Kudumu ya Maendeleo ya Jamii ilifanya taratibu zake na kuiletea Ofisi yake taarifa ya makubaliano ya Muswada wa Serikali ndiyo utako somwa Bungeni baada ya kufuata taratibu zote muhimu.

“Ofisi yangu haifanyi maamuzi  binafsi katika uwasilishwaji wa Miswada Bungeni na zipo hatua mbalimbali Miswada  inayopitia pamoja na Kanuni za Bunge zinatoa muongozo katika utekelezaji wake na Kamati huzingatia  hayo na mwisho hutoa  taarifa ya kuomba Muswada kusomwa ndani ya Bunge,”alisema Mhe.Makinda.

Naye Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Maendeleo ya Jamii  Mhe.Said Mtanda (Mb) wa Mchinga CCM alisema Kamati ilipokea Miswada miwili ya kuundwa kwa Baraza la Vijana ukiwemo wa Mhe.John Mnyika Mb wa Ubungo CHADEMA na Muswada wa Serikali.

Baada ya hapo Kamati ilikaa Kikao  tarehe 20-31 Oktoba 2014 na kujadili Muswada huo ambapo pamoja na mambo mengine iliwaita wadau mbalimbali ambao walitoa maoni yao  na mapendekezo ya Kamati,Kamati iliona Muswada huo haukuwa tayari na hivyo ulirudishwa katika Ofisi ya Spika tarehe 06 Novemba,2014.   

Aidha,Kamati ilipokea Muswada wa Serikali kuhusu hoja ya kuanzishwa kwa Baraza la Vijana Tanzania Muswada na Kamati ilipata nafasi ya kuujadili kwa kina, kupata maoni, ushauri na mapendekezo ya wadau na hivyo badae kamati iliamua kuwa mtoa hoja Binafsi na Serikali wakutane na na kushauriana kisha kupata muafaka wa Muswada upi uingie  ndani ya  bunge.

“Kamati ilipata nafasi ya kujadili hoja zote mbili na kufanya uamuzi wa kidemokrasia wa mashauriano na maridhiano juu ya muswada upi uingie ndani ya Bunge.

Aidha Kamati ilizingatia Kanuni ya 177 ya Kanuni za Kudumu za Bunge, inayosema akidi ya Mkutano wowote wa Kamati ya kudumu itakuwa theluthi moja ya wajumbe wote wa kamati, kwenye kikao hicho kulikuwa na wajumbe 13 kati ya 22 wa kamati nzima na hivyo theluthi moja ya wajumbe hao ni 7, wajumbe 9 walipiga kura ya Muswada wa Serikali usomwe bungeni wajumbe wanne wa walikataka Muswada binafsi uswomwe bungeni”,alisema Mhe. Mtanda.

Mwisho Kamati ilikubali kwa pamoja mambo yote ya msingi yaliyomo kwenye Muswada binafsi yatumike kuboresha Muswada wa Serikali utakaowasilishwa Bungeni. 


Waziri wa Nishati na Madini (wapili kulia), Mhe. George Simbachawene akizungumza na waandishi wa Habari Mjini Dodoma kuhusu Ugunduzi wa nane wa gesi asilia uliyofanywa na Kampuni ya Statoil katika eneo la Bahari Kuu. Wa kwanza kulia ni Naibu Waziri Nishati na Madini Dkt. Charles Mwijage na wa kwanza kushoto ni Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu Nishati na Madini Mhe. Richard Ndassa (Mb) wa Sumve CCM. (Picha na Anitha Jonas – MAELEZO, Dodoma)

No comments:

Post a Comment