TANGAZO


Tuesday, March 3, 2015

Rais Kikwete awaongoza maelfu ya waombolezaji katika mazishi ya Kapteni John Komba

Waombolezaji wakilishusha jenenza lenye mwili wa aliyekuwa Mbunge wa Jimbo la Mbinga Magharibi, Kapteni John Komba wakati wa mazishi yaliyofanyika Kijijini kwao, Lituhi wilayani Nyasa. (Picha zote na Ikulu)
Rais Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete na mkewe Mama Salma Kikwete wakiweka udongo katika kaburi la aliyekuwa mbunge wa Mbinga Magharibi marehemu Kapteni John Damiano Komba wakati wa ibada ya mazishi yake yaliyofanyika kijijini kwake Lituhi wilayani Nyasa, Mkoani Ruvuma leo jioni.
Rais Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete na mkewe Mama Salma Kikwete wakiweka shada la maua katika kaburi la aliyekuwa Mbunge wa Mbinga Magharibi marehemu Kapteni John Komba wakati wa ibada ya mazishi yake yaliyofanyika kijijini kwake Lituhi wilayani Nyasa, mkoani Ruvuma leo jioni.

Na Julius Konala, Mbinga
RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Jakaya Kikwete,ameongoza maelfu ya wananchi wa mkoa wa Ruvuma katika mazishi ya aliyekuwa Mbunge wa Jimbo la Mbinga Magharibi kapteni John Komba kijijini kwake Lituhi.
Marehemu Komba amezikwa majira ya jioni katika makaburi ya misheni katika kijiji cha Lituhi Nyasa ambapo maziko hayo yalitanguliwa na ibada ya misa Takatifu iliyoongozwa na Askofu wa Jimbo la Mbinga John Ndimbo.

Akihubiri katika ibada hiyo ya misa takatifu ya mazishi,Askofu Ndimbo alisema kuwa viongozi hawapaswi kujisahau katika utumishi wao wa kuwatumikia wananchi waliowachagua.

Askofu Ndimbo alisema kuwa badala yake viongozi hao wanatakiwa kutatua kero na changamoto mbalimbali kama marehemu kapteni Komba alivyowatumikia wananchi wake kwa uaminifu.
Alisema kuwa Wananchi wa kijiji cha Lituhi walikuwa na kero ya muda mrefu ya ukosefu wa barabara lakini toka marehemu kapteni Komba awe Mbunge aliweza kusimamia mpaka tatizo hilo limetatuliwa.

Aidha katibu wa Wabunge wa mkoa wa Ruvuma Jenista Mhagama,aliwataka wananchi wa Lituhi kuwa wavumilivu na kudai kwamba ahadi zote walizoahidiwa na marehemu kapteni Komba zitatekelezwa.

Hata hivyo baadhi ya wananchi wa kijiji hicho ambao walikuwa wameahidiwa kupewa misaada na marehemu Komba walipohojiwa na Jambo Leo walisema kuwa hawana uhakika kama ahadi walizoahidiwa kupewa ikiwemo bati kama zitatimizwa.
Akizungumza na jambo Leo Katibu wa aliyekuwa mbunge wa Mbinga magharibi kapteni Komba,aliyejulikana kwa jina la Charles Makenzie alisema kuwa siku ya jumamosi kabla ya kifo chake aliongea na marehemu  kwa masaa matatu kwa simu akimpa maelekezo ya namna ya kugawa bati 900 alizozinunua kwa ajili ya watu wasiojiweza.

Mazishi ya marehemu kapteni Komba aliyefariki dunia siku ya jumamosi yalihudhuriwa na viongozi mbalimbali wa vyama vya siasa na serikali wakiwemo Waziri mkuu mstaafu Edward Lowasa,waziri wa kilimo na chakula Steven Wasira,Waziri wa mchi ofisi ya Rais Mark Mwandosya,spika wa bunge Anne Makinda pamoja na wabunge wa mkoa wa Ruvuma.

 Kaburi la kepteni Komba lilichimbwa kwa mtambo wa kutengenezea barabara katapila.

No comments:

Post a Comment