TANGAZO


Tuesday, March 10, 2015

Maendeleo ya Tiba Asili na Tiba Mbadala nchini Tanzania

Kaimu Mkurugenzi Msaidizi Kitengo cha Tiba Asilia na Tiba Mbadala, Dk. Paulo Mhame, akizungumza na waandishi wa habari, Dar es Salaam leo kuhusu kazi na wajibu ya Wizara kwa jamii, Pia maendeleo ya masuala ya Tiba Asili na Tiba Mbadala nchini. Kulia ni Ofisa Habari wa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, Catherine Sungura. (Picha zote na Kassim Mbarouk-www.bayana.blogspot.com)
Msajili Baraza la Tiba Asili na Tiba Mbadala, Mboni Zuwena Bakari, akifafanua jambo kwa waandishi wa habari, wakati alipokuwa akielezea kuhusu maendeleo ya tiba hiyo. Katikati ni Kaimu Mkurugenzi Msaidizi Kitengo cha Tiba Asilia na Tiba Mbadala, Dk. Paulo Mhame na kulia ni Ofisa Habari wa Wizara, Catherine Sungura.
Kaimu Mkurugenzi Msaidizi Kitengo cha Tiba Asilia na Tiba Mbadala, Dk. Paulo Mhame, akizungumza na waandishi wa habari, Dar es Salaam leo kuhusu kazi na wajibu ya Wizara kwa jamii, Pia maendeleo ya masuala ya Tiba Asili na Tiba Mbadala nchini. Kushoto ni Msajili Baraza la Tiba Asili na Tiba Mbadala, Mboni Zuwena Bakari na kulia ni Ofisa Habari wa Wizara, Catherine Sungura.
Kaimu Mkurugenzi Msaidizi Kitengo cha Tiba Asilia na Tiba Mbadala, Dk. Paulo Mhame, akizungumza na waandishi wa habari, wakati wa mkutano huo, Dar es Salaam leo.
Baadhi ya waandishi wa habari, wakiwa kwenye mkutano huo jijini leo.

Ndugu Waandishi wa Habari
Maendeleo ya tiba asili nchini yalianza mara baada ya Uhuru. Aidha, nia halisi ya Serikali ya kuleta maendeleo katika tiba asili ilijidhihirisha mwaka 1969 na kujifunua mwaka 1974 Julai, Serikali ilipoanzisha kitengo cha utafiti katika tiba asili kwenye Kitivo cha Afya cha Muhimbili. Leo hii kitengo kile kimekuwa Taasisi kamili chini ya Chuo Kikuu kamili cha MUHAS.

Maendeleo ya jambo linalohusisha taasisi zaidi ya moja huchukua muda mrefu, tiba asili vivyo hivyo. Hadi mwaka, 2002  Serikali ilitunga sheria Na. 23 ya Tiba Asili na Tiba Mbadala. Katika kipindi hichohicho Taasisi ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu ilianzisha Idara ya utafiti wa tiba asili kwa lengo la kuongeza nguvu za utafiti.

Mwaka 2005 BARAZA la kwanza la  Tiba Asili na Tiba Mbadala lilianzishwa kwa mujibu wa sheria Na. 23 ya mwaka 2002. Baraza liliweka utaratibu wa namna ya kuwasajili waganga wa tiba asili na tiba mbadala.

Waganga wa tiba mbadala ni wataalamu wa tiba kulinga na tiba asili za nchi zisizo za Kiafrika kusini ya jangwa la sahara. Taaluma hizo ni nyingi na zinahusisha nchi nyingi dunia; kwa mfano Tiba Asili ya Kichina, Tiba Asili ya Korea, Tiba Asili ya India, Tiba Asili ya Ugiriki, Ujerumani, Uingereza nakadhalika.

Waganga wa tiba asili wa asili ya Tanzania pia wapo wa aina nyingi kulingana na kabila analotoka. Tanzania Bara kuna aina 120 au zaidi za makabila na hivyo kuna taaluma za tiba asili 120. Inakadiriwa kuwa Tanzania Bara ina waganga na wakunga wa tiba asili 75,000. Idadi hii ni kubwa kuweza kuiratibu na kuwasajili kwa kupindi kifupi.

Pamoja na ugumu huo BARAZA limeweza kuwahamasisha na kuwasajili waganga 6000 nchi nzima na bado kazi ya kuwasajili inaendelea.

Ili kurahisisha kazi ya uhamasishaji na usajili kufanyika, Baraza kwa kushirikiana na Serikali wameteuliwa waratibu wa tiba asili katika ngazi za mikoa na halmashauri.

Tunawashukuru sana waratibu hao kwa kuitikia wito wa uteuzi wao huo kwani kazi iliyopo mbele yetu siyo nyepesi ina changamoto nyingi. Moja ya changamoto zilizopo ni kuwa taaluma ya tiba asili ya asili ya Tanzania haipo katika maandishi. Kinachozungumzwa siyo rahisi kukithibitisha na hususan jambo lisilohusisha dawa ambazo ndizo pekee zinafanyiwa utafiti na Taasisi zetu.

KUANZISHWA KWA SHIRIKISHO LA VYAMA VYA WAGANGA WA TIBA ASILI TANZANIA

Katika kuweza kufanisha malengo ya kuendeleza na kuboresha huduma za tiba asili nchini Serikali ilikaa na vyama vya waganga wa tiba asili ili kuweza kuungana na kuunda Shirikisho la Vyama vya Tiba Asili Tanzania (SHIVYATIATA). Baadhi ya malengo ya SHIVYATIATA ni kuviwakilisha vyama wanachama na kuwa msemaji mkuu wa vyama vya Tiba Asili kwa Serikali, Taasisi za kitaifa, kimataifa na mahali popote pale itakapotakiwa. Pili ni kuvishirikisha vyama wanachama wa Tiba Asili nchini Tanzania kuungana kwa lengo la kuleta ushirikiano na mahusiano yenye manufaa miongoni mwa vyama, wanachama, Serikali na mashirika mengine ya kitaifa na kimataifa ili kuwa na mtizamo wa pamoja katika kuboresha taaluma, tafiti, haki na maslahi yatokanayo na Tiba Asili. Tatu kuwafanya watabibu wa Tiba Asili nchini wa shirikiane, wawe wamoja na kauli moja kwa ajili ya kulinda taaluma ya Tiba Asili, kutetea kazi na maslahi yatokanayo na kazi ya Tiba Asili nchini

Vivyo hivyo kwa waganga wa tiba mbadala nao wamaanzisha Chama cha Waganga wa Tiba Mbadala Tanzania.

CHANGAMOTO ZA UENDELEZAJI NA UBORESHAJI WA TIBA ASILI TANZANIA
Pamoja kuwa mwaka huu tunafikia mwaka wa 54 wa Uhuru wetu, katika kuboresha na kuendeleza huduma za Tiba Asili tuna changamoto nyingi.

Ø  Moja utafiti wetu haujatoa majibu yanayokusudiwa, ikiwa pamoja na kupata dawa zetu za asili au zilizoboreshwa kutoka katika miti dawa yetu.
Ø  Utoaji wa huduma katika tiba asili usiohusisha dawa hauna maelezo ya kisayansi
Ø  Waganga na wakunga wa tiba asili waliopo ni wengi na ni changamoto ya kuwafikia wote mara moja
Ø  Utoaji wa huduma za tiba asili unatolewa kwa aina 120 tofauti
Ø  Waganga au wakunga wa tiba asili wanazo taaluma za asili zaidi ya uganga au ukunga.

Kwa kuwa kabla ya miaka ya 1880 mtu anayeitwa mganga walijumuisha:
Ø  Mganga wa kutibu na kuponya
Ø  Mganga wa kumshauri kiongozi kuhusu namna bora ya kutawala
Ø  Mganga wa kumshauri kiongozi kuhusu namna bora ya kuleta ustawi katika eneo lao
Ø  Mganga wa kumshauri kiongozi kuhusu kwenda au kutokwenda vitani na wahasimu wao
Leo makundi hayo yote hayapo lipo kundi moja tu la waganga wa tiba asili, inakuwa siyo rahisi kumtambua yupi mwenye taaluma nyingine pia.

Kuwa na aina nyingi za tiba asili (120) na kuwepo kwa vyama vingi vya waganga wa tiba asili nayo ni changamoto inayoathiri:
Ø  Ushirikishwaji wa mganga ili kuboresha huduma za tiba asili
Ø  Vyama kutumika kama chachu ya mganga kufanya kazi kwa pamoja kwa kuungana
Ø  waganga wa taaluma tofauti kutofanya kazi kwa pamoja kiushirika kwa kuungana na kutoa huduma au kuuza dawa zao

Ndugu waandishi wa habari,

MATUMIZI YA VYOMBO VYA HABARI KUHUSU TIBA ASILI TANZANIA

Kupitia kazi yenu ya uandishi wa habari ni matarajio makubwa ya BARAZA na Serikali kuwa mtawahabarisha wananchi kuhusu tiba asili na tiba mbadala kwa kuzingatia sheria, kanuni na miongozo iliyopo. Kwa kufanya hivyo wananchi watapata taarifa zilizo sahihi.

Kuna taarifa za aina nyingi zinazohusu tiba asili na tiba mbadala;
Ø  Uelimishaji  hii ni kwa kuwa wananchi wengi hawajui kuhus tiba asili na au tiba mbadala [taarifa hizi zitolewe na wataalamu waliobobea na taarifa zenyewe ziwe zimehakikiwa na BARAZA kama sheria inavyoelekeza]
Ø  Dawa na matumizi ya dawa mbalimbali zinazotolewa [sheria inazuia kutangaza]
Ø  Kutangaza kituo kinachotoa huduma za tiba asili na tiba mbadala [sheria inazuia kutangaza vituo vinavyotoa huduma za tiba]

Ni matarajio ya Serikali na Baraza kuwa vyombo vya habari vitajitahidi kufanya kazi kulingana na sheria, kanuni na miongozo.

1 comment: