Michuano ya netball ya Afrika ya Mashariki imemalizika Zanzibar huku timu ya MOICT ya Kenya ikitwaa ubingwa kwa upande wa wanawake baada ya kuifunga timu ya NIC ya Uganda kwa mabao 32-29.
NIC ndio walikuwa mabingwa watetezi baada ya kulinyakua kombe hilo mwaka jana katika michuano iliyofanyika Dar es Salaam. Hii ni mara ya pili kwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuandaa michuano hiyo mara mbili mfululizo, zamu hii ikiwa ni upande wa Tanzania Zanzibar (visiwani) katika viwanja vya Gymkhana.
Netball, au mpira wa pete ni mchezo ambao kwa miaka mingi umekuwa ukihusisha timu za wanawake pekee, lakini katika kuleta usawa (gender balance) kama ilivyo kwa michezo mingine kama vile mpira wa kikapu (basketball), wavu na mingineyo, mchezo huo katika miaka ya hivi karibuni, umekuwa ukishirikisha timu za wanaume katika kuleta hamasa na ushindani.
Kwa upande wa wanaume, wenyeji Polisi ya Zanzibar waliibuka washindi wa michuano hiyo ya Afrika Mashariki, baada ya kuwafunga wenzao wa JKU (pia ya Zanzibar) kwa mabao 38-34 katika mechi ya vuta nikuvute.
Michuano hiyo hufanyika kila mwaka kwa nchi wanachama kupeana zamu za kuandaa mashindano hayo. Nchi zilizoshiriki ni wenyeji Zanzibar, Kenya, Uganda na Tanzania Bara. Rwanda na Burundi ni sehemu ya jumuiya hiyo ya Afrika ya Mashariki lakini hawana historia kubwa ya kuwa sehemu ya kuwa nchi shiriki.
No comments:
Post a Comment