TANGAZO


Thursday, March 19, 2015

Maadhimisho ya Wiki ya Maji Mpiji Magohe watoa ardhi bila fidia kupata umeme wa uhakika kwenye chanzo cha maji

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Mhe. Said Meck Sadiki  na Mbunge wa Ubungo Mhe. John Mnyika wakifungua maji ya bomba kwenye Zahanati ya Kijiji cha Mpiji Magohe mara baada ya kuzindua mradi wa maji katika kijiji hicho manispaa ya Kinondani jijini Dar es Salaam.(Photo zote na Aron Msigwa-MAELEZO) 
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Mhe. Said Meck Sadiki akizindua Tenki la kuhifadhia maji  katika kijiji cha Mpiji Magohe, manispaa ya Kinondani jijini Dar es salaam leo wakati wa mwendelezo wa maadhimisho ya Wiki ya Maji yanayoendelea mkoani Dar es salaam.
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Mhe. Said Meck Sadiki akizindua Tenki la kuhifadhia maji  katika kijiji cha Mpiji Magohe, manispaa ya Kinondani jijini Dar es salaam leo wakati wa mwendelezo wa maadhimisho ya Wiki ya Maji yanayoendelea mkoani Dar es salaam. 
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Mhe. Said Meck Sadiki akizungumza na wakazi wa kijiji cha Mpiji Magohe Kata ya Mbezi, manispaa ya Kinondoni jijini Dar es salaam mara baada ya kuzindua mradi wa maji wa kijiji hicho leo. 
Mbunge wa Ubungo Mhe. John Mnyika akizungumza na wa kijiji cha Mpiji Magohe Kata ya Mbezi, manispaa ya Kinondoni jijini Dar es salaam mara baada ya kuzindua mradi wa maji wa kijiji hicho leo. 

Na Aron Msigwa – MAELEZO
19/3/2015.
Dar es Salaam.
Wakazi wa kijiji cha Mpiji Magohe, Kata ya Mbezi wilayani Kinondoni jijini Dar es salaam wamekubali kuyatoa maeneo ya ardhi wanayomiliki bila fidia ili yaweze kutumiwa na Shirika la Ugavi wa Umeme nchini (TANESCO) kupitisha nguzo za umeme kuelekea  mahali ilipo  pampu ya kusukuma maji kwenye chanzo cha maji kijijini hapo ili waweze kupata  huduma ya uhakika  ya  maji kutokana na chanzo hicho kutumia umeme wa jenereta.     
Wananchi hao wametoa uamuzi huo leo mbele ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam Mhe. Saidi Meck Sadiki ambaye alikuwa mgeni rasmi wakati wa maadhimisho ya Wiki ya Maji kijijini hapo, yaliyoambatana na uzinduzi wa mradi
wa maji wa kijiji hicho uliogharimu kiasi cha fedha za kitanzania zaidi ya shilingi milioni 460.
Akizungumza na wakazi hao, Mhe. Sadiki amesema kuwa  kukamilika kwa mradi ni moja ya juhudi za Serikali za kuhakikisha wananchi wanapata maji safi katika maeneo yao na kuongeza kuwa mradi  huo  utawanufaisha zaidi ya watu 6600 wa kijiji hicho na kuondoa kero ya kupata maji safi iliyodumu kwa zaidi ya miaka 20.
Amesema kuwa uamuzi walioufanya wananchi hao kuruhusu maeneo yao kupitisha nguzo za umeme bila kudai fidia ni wa kipekee na unafaa kuigwa na wananchi wa maeneo mengine ili kurahisisha upatikanaji wa huduma zao za msingi na kuwaahidi wananchi hao kuwa atawasiliana na mamlaka husika ili umeme wa TANESCO uweze kufika katika chanzo chao cha maji kupunguza gharama za uendeshaji na kuharakisha kukamilishwa kwa mradi huo.
 
Ameitaka kamati ya maji inayosimamia mradi wa kijiji hicho kuhakikisha kuwa inafanya kazi kwa ufanisi, uadilifu na uwazi ili kuondoa migogoro ya uongozi na wananchi hali inayoweza kutishia uhai wa mradi huo.
 
“Natoa agizo kwa viongozi wa kamati ya maji ya kijiji hiki muhakikishe kuwa mnafanya kazi zenu kwa ufanisi mkubwa, uadilifu, mzingatie sheria na kuhakikisha taarifa za fedha za mradi hasa mapato na matumizi mnazitoa kwa wananchi kila baada ya miezi 3 kulingana na mwongozo uliopo” Amesisitiza.
 
Kuhusu maadhimisho hayo ya wiki ya Wiki ya Maji ambayo huadhimishwa duniani kote kila ifikapo Machi 16 hadi 22 kila mwaka kuanzia ngazi ya taifa, mkoa na wilaya amesema kwa mwaka huu jijini Dar es salaam maadhimisho hayo yameambatana na uzinduzi wa miradi ya maji katika maeneo mbalimbali, utoaji wa elimu kuhusu huduma za maji , utunzaji wa vyanzo vya  maji na miundombinu ya maji kote nchini.
Amesema  maadhimisho ya mwaka huu pia yanawakutanisha wananchi na taasisi za uendeshaji huduma, usimamizi na usambazaji wa maji ambazo hutoa elimu kuhusu huduma za maji wanazotoa, kupokea maoni na kero za wananchi na kuendesha operesheni mbalimbali za kuwakamata baadhi ya watu wanaoiba maji na kuhujumu miundominu ya maji nchini.
 
Kuhusu usambazaji wa maji katika maeneo mengine amesema kuwa uchimbaji wa visima 20 awamu ya kwanza imeanza na itakamilika mwezi Agosti mwaka huu ikihusisha upanuzi wa mtandao wa usambazaji wa maji katika maeneo yaliyo kandokando ya mabomba makuu kutoka Ruvu chini na Ruvu juu na kuvinufaisha vitongoji vilivyopo kati ya mji wa Bagamoyo hadi eneo la Tegeta-Mpiji na vitongoji vilivyopo kati ya mji wa Mlandizi –Kiluvya na maeneo ya Mbezi, Kimara na Goba.
 
Awamu ya pili itahusisha upanuzi wa mfumo wa usambazaji wa maji katika maeneo yote ya jiji yatakayopata maji kutoka Kimbiji na Mpera na maeneo mengine ya jiji yasiyo na mabomba ya usambazaji wa maji.
 
Kwa upande wake Mbunge wa jimbo la Ubungo Mhe. John Mnyika akizungumza na wakazi wa Mpiji Magohe ameishukuru Serikali na wananchi wa kijiji cha Mpiji Magohe kwa kutoa ushirikiano  ambao umefanikisha kukamilika kwa mradi huo.
 
Amesema yeye kama mbunge wa eneo  hilo ataendelea kushirikiana na viongozi wa  Serikali wa mkoa wa Dar es salaam kuhamasisha maendeleo ya wananchi kushirikiana kikamilifu katika ujenzi wa miundombinu ya barabara na maji na kutoa wito kwa wananchi kuhakikisha wanalinda vyanzo vya maji na kutunza miundombinu iliyowekwa ili iendelee kuwa na manufaa kwa kipindi kirefu.

No comments:

Post a Comment