Baadhi ya Madereva wakifuatilia mafunzo yaliyoandaliwa na Ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali ili kuwezesha usafirishaji salama wa Kemikali ili kulinda afya na mazingira dhidi ya madhara ya kemikali.
Mkemia Mkuu wa Serikali Prof. Samweli Manyele Mwenye suti nyeusi (katikaki) akiwa pamoja na madereva wa magari yanayosafirisha kemikali mara baada yakufungua mafunzo hayo. Kulia kwake ni baadhi ya Viongozi wa Ofisi hiyo na kulia ni Mkaguzi wa Polisi Kuruthumu Bambe.
(Picha zote na MAELEZO)
Frank Mvungi-Maelezo
SERIKALI inaendelea kuimarisha mifumo yausafirishaji wa Kemikali ndani na nje ya nchi kwa kutoa mafunzo kwa wasafirishaji.
Hayo yamesemwa leo Jijini Dar es salaam na Mkemia Mkuu wa Serikali Prof. Samwel Manyele wakati akifungua mafunzo ya siku mbili yanayowahusisha madereva zaidi ya 50 wa malori yanayosafirisha Kemikali.
Akizungumzia lengo la mafunzo hayo, Prof. Manyele amesema kuwa yanalenga kuwajengea uwezo madereva wote wanaohusika katika kusafirisha kemikali ili wawe na uwezo wa kuchukua hatua stahiki pale ambapo majanga yanayotokana na kemikali hizo yanapotokea.
Zaidi ya hayo, Mkemia Mkuu wa Serikali amesema lengo jingine ni kuwapa mbinu stahiki Madereva hao ili kuweza kusafirisha kemikali hizo kwa kuzingatia sheria na kanuni zilizowekwa ili kupunguza au kuondoa kabisa majanga yanayoweza kutokana na kutozingatiwa kwa taratibu husika.
Ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali katika kipindi cha miezi 20 iliyopita ilitekeleza mradi wa kuzuia, kujiandaa na kukabiliana na ajali za Kemikali lengo likiwa kuongeza uwezo kwa wadau juu ya mbinu bora za kupambana na majanga hayo yanapotokea. Alisisitiza Prof. Manyele.
Kuhusu wajibu wa madereva wanaosafirisha Kemikali, Prof. Manyele amesema kuwa ni lazima wawe na kadi ya usalama wa kemikali kama nyaraka muhimu kuhusiana na usafirishaji salama wa kemikali.
Akizungumzia matukio ya ajali zilizotokea kati ya mwezi Januari hadi Desemba 2014, Prof. Manyele alisema kuwa matukio 11 ya ajali hizo yalisababisha vifo vya watu zaidi ya 14 na uharibifu wa mali ikiwemo kuungua kwa moto tani zaidi ya 250 za kemikali na kuungua kwa maduka.
Kwa upande wa mazingira yanahusisha kutokea kwa ajali za kemikali, Prof. Manyele amesema kuwa mara nyingi hutokea wakati wa kupakia na kupakua, hivyo mafunzo hayo yataweka mkazo na kuhakikisha kuwa madereva pamoja na wadau wote wanaohusika na usafirishaji huo wanakuwa na uwezo wa kuzingatia taratibu zote za usalama ili kuepusha majanga hayo.
Baadhi ya Mada zitakazowasilishwa katika mafunzo hayo ya siku mbili ni Sheria ya Kemikali za viwandani na majumbani ya mwaka 2003 na kanuni zake za mwaka 2015 zinazohusu usafirishaji salama wa kemikali, wajibu wa wamiliki wa kampuni za usafirishaji wa kemikali na wajibu wa madereva wakaqti wa kusafirisha kemikali hizo.
No comments:
Post a Comment