TANGAZO


Wednesday, February 18, 2015

Wasanii wa Filamu Nchini watakiwa kutokuwa makontena ya biashara haramu

Katibu Mtendaji Bodi ya Filamu Bibi Joyce Fisoo akizungumza na wasanii wa bongo movie wanaotarajia kwenda nchini Uingereza kurekodi filamu na kampuni ya Didas Entertainment iliyopo nchini Uingereza. Kulia ni Mama wa Didas Bi. Nuru Idrisa. (Picha zote na Genofeva Matemu – Maelezo) 
Wasanii kutoka kulia, Yusuph Mllela, Ofisa kutoka Bodi ya Filamu Bibi Beatrice Msumari, Msanii Esha Buheti na Msanii Husna Athumani wakimsikiliza kwa makini Katibu Mtendaji Bodi ya Filamu walipofika ofisini kwake kwa ajili ya kuwaaga wasanii hao wanaotarajia kwenda nchini Uingereza kurekodi filamu na kampuni ya Didas Entertainment.
Katibu Mtendaji Bodi ya Filamu Bibi Joyce Fisoo kulia akimpa mkono msanii Yusuph Mllela baada ya neno la kuwaaga wasanii watatu (Yusuph Mllela, Esha Buhet na Husna Athumani) wanaotarajia kwenda nchini Uingereza kurekodi filamu na kampuni ya Didas Entertainment. 
Msanii wa Bongo Movie Bi. Esha Buheti (kushoto), akifurahi wakati wa kuagana na Katibu Mtendaji Bodi ya Filamu Bibi Joyce Fisoo kwa ajili ya kuanza safari ya kwenda nchini Uingereza kurekodi filamu na kampuni ya Didas Entertainment. Katikati ni Mama wa Didas Bi. Nuru Idrisa.
Msanii Husna Athumani akipokea mkono wa pongezi kutoka kwa Katibu Mtendaji Bodi ya Filamu Bibi Joyce Fisoo (kulia) wakati wa kuwaaga wasania wanaotarajia kwenda nchini Uingereza kurekodi filamu na Kampuni ya Didas Entertainment. Katikati ni Mama wa Didas Bi. Nuru Idrisa. 

Na Genofeva Matemu – Maelezo
Tarehe 18/02/2015
WASANII wa Bongo Movie wameshauriwa kutumia taaluma waliyonayo kupanua wigo wa filamu nchini na kuitangaza Tanzania duniani kote kwa kuzingatia matumizi mazuri ya lugha ya Kiswahili katika filamu wanazozitengeneza.

Rai hiyo imetolewa na Katibu Mtendaji Bodi ya Filamu Bibi Joyce Fisoo leo alipokutana na wasanii wanaotarajia kwenda nchini Uingereza tarehe 19 ya mwezi Februari mwaka huu kurekodi filamu ya Sabasi na Kampuni ya Didas Entertainment iliyopo nchini humo.

Bibi Fisoo amesema kuwa wasanii wengi nchini wamekua makontena yanayopitisha biashara haramu kutoka nchi moja kwenda nchi nyingine hivyo kuwaomba wasanii wanaoekwenda Uingereza kuachana na tabia hiyo bali kutumie fursa waliyoipata kuiwakilisha Tanzania vizuri na kutengeneza filamu bora itakayowawezesha kujulikana na kushirikishwa katika filamu na nchi nyingine duniani.

Aidha Bibi Fisoo amewataka wasanii hao kuheshimu sheria, kanuni na taratibu za Uingereza kwani kwa kufanya hivyo watakuwa mabalozi bora na kutoa nafasi kwa wasanii wengine kupata fursa hizo.

Naye Mama wa Didas Entertainment Bibi Nuru Idrisa amewataka wasanii wa Bongo Movie waliopata nafasi ya kurekodi filamu na Didas Entertainment kujiheshimu na kuvaa mavazi ya staha yatakayostiri miili yao muda wote watakaokuwa nchini Uingereza kwani kwa kufanya hivyo watakuwa wamethamini na kulinda heshima ya nchi.

Akitoa neno la shukrani Msanii wa Bongo Movie Bw. Yusuph Mllela ameishukuru Bodi ya Filamu kwa kuwa bega kwa bega na wasanii na kuwahahidi wadau wa filamu nchini kukaa mkao wa kupokea kazi bora na yenye tija katika jamii.
Filamu ya Sabasi inayotarajiwa kurekodiwa hivi karibuni nchini Uingereza na Kampuni ya Didas Entertainment na kuwashirikisha wasanii Yusuph Mllela, Esha Buhet na Husna Athumani ni filamu ya pili kurekodiwa na kampuni hiyo na kuwashirikisha wasanii kutoka Tanzania, filamu ya kwanza kurekodiwa na Kampuni hiyo iliyowashirikisha wasanii kutoka Tanzania ni ile ijulikanayo kwa jina la Mateso yangu Ughaibuni.

No comments:

Post a Comment