TANGAZO


Monday, February 16, 2015

Makamu wa Pili wa Rais Zanzibar, Balozi Seif Idd awataka wanachama kuwatafakari walioanza harakati za kuomba kuteuliwa kuwa wagombea kabla ya wakati uliopangwa

Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM Taifa Balozi Seif Ali Iddi akiwa sambamba na Mwenyekiti Mstaafu wa CCM Taifa Mzee Ali Hassan Mwinyi wakikata utepe kuashiria kuzinduliwa kwa Jengo la Ofisi ya Tawi la CCM la Kijiji cha Ghana Jimboni Uzini Mkoa wa Kusini Unguja.

Balozi Seif akiwa na Mjumbe wa Kamati ya Siasa ya Mkoa wa Kusini Unguja  aliyepo Kati kati Dr. Idriss Muslim Hijja na Mwakilishi wa Jimbo la Uzini Mh. Moh’d Raza wakifurahia mazingira safi ya Ofisi Mpya ya CCM Tawi la Ghana mara baada ya kuzinduliwa rasmi.
Mwakilishi wa Jimbo la Uzini Mh. Moh’d Raza akielezea umuhimu wa wana CCM kuendelea kushirikiana pamoja ili kupata faraja wakati wa hafla fupi ya kuzinduliwa  kwa Ofisi ya Tawi la CCM Ghana Mkoa wa Kusini Unguja.
Mwenyekiti Mstaafu wa CCM Taifa Mzee Ali Hassan Mwinyi akiwanasihi Wananchi kuendelea kuheshimu Historia ya Kijiji cha Ghana kiliopo Wilaya ya Kati ambacho kilihusika kikamilifu katika maandalizi ya Mapinduzi ya Zanzibar ya Mwaka 1964.
Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM Balozi Seif Ali Iddi akizungumza na Wana CCM na Wananchi wa Kijiji cha Ghana ndani ya Jimbo la Uzini mara baada ya kulizindua Tawi lao jipya. Kulia ya Balozi Seif ni Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Kusini Unguja Nd. Ramadhan Abdullah  Ali, kushoto ya Balozi Seif ni Mwenyekiti wa CCM Tawi la Ghana Ndugu Daud Haji Hassan pamoja na Mjumbe wa Kamati ya Siasa ya Mkoa wa Kusini Unguja Dr. Idriss Muslim Hijja.


Mandhari  nzuri ya kupendeza inayoonekana ya Jengo la Ofisi ya CCM Tawi la Ghana liliopo Jimbo la Uzini, Wilaya ya Kati, Mkoa wa Kusini Unguja. (Picha zote na Hassan Issa – OMPR – ZNZ)

Na Othma n Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
16/2/2015.
MJUMBE wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM Balozi Seif Ali Iddi amewaasa wana CCM Nchini kutafakari kwa makini wimbi la Wanachama walioanza harakati za kuomba kuteuliwa kuwa wagombea  wa nafasi za Uongozi kabla ya wakati maalum ulipangwa na chama kwa mujibu wa katiba na miongozo iliyowekwa.

Alisema  CCM itamteua mwanachama  mwenye sifa zinazozingatia maadili na miongozo ya Chama kugombea nafasi ya Uongozi baada ya  wanachama hao kuwachambua  wahusika hao katika vikao vitakavyowahusu kwenye maeneo yao.

Balozi Seif Ali Iddi alitoa nasaha hizo wakati wa hafla fupi ya kulizindua jengo la Ofisi ya Tawi jipya la CCM  la Kijiji cha Ghana shughuli aliyoifanya sambamba na Mwenyekiti Mstaafu wa CCM Taifa Mzee Ali Hassan Mwinyi ndani ya Jimbo la Uzini Wilaya ya Kati Mkoa wa Kusni Unguja.

Ujenzi wa Tawi hilo la CCM uliofanywa na Mwakilishi wa Jimbo la Uzini Mh. Moh’d Raza Hassanali umekuja kufuatia lile la mwanzo  lililojengwa na Mbunge wa Jimbo hilo Mh. Moh’d Seif Khatib mwaka 2000 kupata athari wakati wa ujenzi wa Barabara.

Balozi Seif ambae pia ni Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alisema licha ya kwamba Chama cha Mapinduzi kina utajiri mkubwa wa Viongozi wa kuongoza Dola ya Tanzania lakini bado wanachama na wananchi wanapaswa kuwa makini  kuwapima viongozi wanaokusudia kuwachagua ili wawaongoze.

Alieleza kwamba zipo nchi kadhaa Duniani ambazo wananchi wake walidanganywa na kupewa matumaini makubwa ya maisha kiasi kwamba sasa wanaishi katika maisha ya dhiki  na udhalili.

“ Wanachama  wa CCM lazima wawe makini na hadhari na Watu wanaotafuta fursa za kutaka kuongoza kabla ya wakati uliopangwa kwa mujibu wa katiba, sera na miongozo ya chama“.   Alitahadharisha Balozi Seif.
Akizungumzia upigaji wa  kura ya maoni na uchaguzi Mkuu unaolikabili Taifa ndani ya mwaka huu wa 2015  Mjumbe huyo wa Kamati Kuu ya CCM Taifa Balozi Seif alitanabahisha kwamba vyombo vya dola vitakuwa makini katika kukabiliana na vikundi au mtu ye yote atakayeamua kusababisha vurugu kwenye chaguzi hizo.

Alisema mbinu za kisiasa zilizokuwa zikitumiwa na baadhi ya wafuasi wa vyama vya kisiasa kwa kuwatumia vijana  katika kuvuruga amani ya nchi zinaeleweka na kamwe Serikali zote mbili hazitakuwa tayari kuona amani hiyo inachezewa kizembe.

“ Kwanini Serikali kupitia vyombo vyake vya ulinzi  viwaachie watu wasababishe vurugu na uvunjifu wa amani  ya Nchi ? “. Aliuliza Balozi Seif.
Mjumbe huyo wa Kamati Kuu ya CCM Taifa amempongeza Mwakilishi wa Jimbo la Uzini Mh. Moh’d  Raza kwa kusimamia ujenzi wa Jengo la Ofisi ya Chama Tawi la Ghana akionyesha  kutekeleza kwa vitendo agizo la  CCM la kuwataka wanachama wake wajenge Ofisi zitakazofanana na chama chenyewe.

Balozi Seif alisema ukamilikaji wa ujenzi huo wa Ofisi utawapa fursa nzuri wanachama wa Tawi hilo kufanya vikao vyao ndani ya ofisi na kuacha tabia ya kurundika  vikao kwani  waelewe kwamba nje ya vikao ni kukaribisha fitina zitakazozaa makundi na kukigawa chama.
Akimuunga mkono Mwakilishi wa Jimbo la Uzini Mh. Moh’d Raza Mjumbe huyo wa Kamati Kuu ya CCM Taifa Balozi Seif aliahidi kuwasaidia Wanachama wa Tai la Ghana Seti ya TV, Deki pamoja na King’amuzi chake ili kuwapa fursa wanachama na wananchi wa Kijiji hicho kupata Habari na Matukio mbali mbali ya Kitaifa na Kimataifa.
Akisoma Risala ya Wana CCM wa Tawi la Ghana Katibu wa Tawi hilo Bibi Khadija Awadh Omar alisema Tawi lao lilijengwa mwaka 2000 lakini ujenzi wa Miundo mbinu ya Bara bara liyopita pembezoni mwa Jengo hilo umesababisha ubovu wa jengo hilo.

Bibi Khadija alisema Jengo hilo limeanza kujengwa  tena mnamo Tarehe 24 Oktoba mwaka 2014 chini ya usimamizi wa Mwakilishi wa Jimbo hilo ambapo hivi sasa liko tayari kwa matumizi na lina vifaa vyake kamili vya ofisi ikiwemo huduma za umeme.

Naye Mwakilishi wa Jimbo la Uzini Mh. Moh’d Raza akitoa shukrani zake kwa     kuungwa mkono wana CCM na wananchi wa Jimbo hilo  katika ujenzi wa Jengo hilo alihimiza umuhimu wa ushirikiano utakaoongeza  nguvu za kuleta faraja kwa masuala yoyote watakayoamuwa kuyapanga.

Mh. Raza aliwaahidi wanachama hao wa CCM na Wananchi hao kwamba Uogozi wa Jimbo hilo utahakikisha kwamba bara bara zote za ndani zilizomo kwenye Jimbo hilo zinashughulikiwa  ipasavyo ili kuwapa unafuu wa mawasiliano ya usafiri wananchi wa vijiji hivyo.
Akitoa salamu zake kwenye hafla hiyo Mwenyekiti Mstaafu wa CCM Taifa ambae pia ni Rais Mstaafu wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Mzee Ali Hassan Mwinyi aliwapongeza Wananchi wa Kijiji cha Ghana kwa kupata jengo jipya la Chama.

Mzee Mwinyi alisema Kijiji cha Ghana kina Historia kubwa ya uhusiano wa watu wote waliokuwa wakishirikiana Barani Afrika kudai Uhuru wao kutokana na madhila ya wakoloni.

Alisema Kijiji cha Ghana kimeleta mchango mkubwa katika upatikanaji wa Mapinduzi ya Zanzibar ya mwaka 1964 ambapo  Mikutano mingi ya kupanga njia za  kudai Uhuru iliyoongozwa na Rais wa Kwanza wa Zanzibar Marehemu Mzee Abeid Karume ilifanywa kwenye Kijiji hicho.

“ Bwana Abeid Karudi Ghana Kavaa Pakacha Mchana. Ni ubeti wa Shairi ya moja kati ya  nyimbo za wakati wa kudai uhuru lilioimbwa  na Mwenyekiti wa CCM Mkoa Kusini Unguja Nd. Ramdhan Abdullah Ali kwenye ghafla hiyo“. 

Lengo la kuimba  kwake shairi hilo ni kukikumbusha  kizazi kipya juhudi zilizochukuliwa na wazazi wao wakati wa kudai uhuru wa Visiwa hivi.
Ujenzi wa Jengo la Ofisi ya Chama cha Mapinduzi Tawi la Ghana Jimbo la Uzini uliosimamiwa na Mwakilishi wa Jimbo hilo umegharimu jumla ya shilingi za Kitanzania Milioni 45,000,000/-.

No comments:

Post a Comment