Mkurugenzi Idara ya Utamaduni kutoka Wizara ya Habari, Vijana,Utamaduni na Michezo Prof. Herman Mwansoko akiongea na wasanii nchini na kuwaeleza kuhusu umuhimu wa sekta hiyo kushiriki kikamilifu katika masuala ya kitaifa hasa katika kipindi hiki cha kuelekea upatikanaji wa Katiba Mpya, Kulia ni Katibu wa Bodi ya Filamu Bi. Joyce Fisoo.
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam Dkt. Francis Michael akiongea na wasanii nchini na kuwaeleza namna gani makundi mbalimbali yalivyoainishwa kwenye Katiba Inayopendekezwa ikiwemo haki za wasanii tofauti na Katiba ya Mwaka 1977.
Waziri wa Habari, Vijana,Utamaduni na Michezo Dkt. Fenella Mukangara akiongea na baadhi ya wasanii mara baada ya kuisha kwa mkutano huo leo Jijini Dar es Salaam.
Waziri wa Habari, Vijana,Utamaduni na Michezo Dkt. Fenella Mukangara akibadilishana mawazo na baadhi ya wasanii mara baada ya kuisha kwa mkutano huo leo Jijini Dar es Salaam.
Waziri wa Habari, Vijana,Utamaduni na Michezo Dkt. Fenella Mukangara akiwasikiliza baadhi ya wasanii wakati wa mkutano huo.
Waziri wa Habari, Vijana,Utamaduni na Michezo Dkt. Fenella Mukangara akiongea na wasanii nchini na kuwaasa wasanii kuielimisha na kuhamasisha Jamii kuhusu Katiba Inayopendekezwa kupitia kazi mbalimbali za sanaa, wakati wa mkutano na wasanii nchini uliofanyika leo Jijini Dar es Salaam.
Hotuba ya Waziri Fenella Mukangara kwa wasanii
Katibu Mkuu, Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na
Michezo,
Viongozi wa Wasanii wa fani mbalimbali,
Wakurugenzi Wizara ya Habari , Vijana , Utamaduni na
Michezo,
Mtoa Mada,
Waandishi wa Habari
Mabibi na Mabwana
Habari za
Mchana,
Nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutuwezesha
kufika siku ya leo na kuuona mwaka 2015. Niwatakie wote heri ya mwaka mpya,
uwe wa baraka na mafanikio makubwa
katika shughuli zenu za kila siku.
Nichukue nafasi hii
kuwashukuru kwa kuitikia mwaliko wetu na kujitokeza kwa wingi kushiriki
katika Mkutano wa leo pamoja na majukumu mazito mlionayo.
Ndugu Wasanii,
Napenda kutoa pongezi za dhati kwa kazi kubwa
mnayoifanya ya kueleimsha Jamii katika masuala mbalimbali. Aidha kazi zenu zimekuwa ni chachu ya kuleta mabadiliko
chanya katika Taifa letu na zimekuwa ni utambulisho wa Utaifa wetu nje ya
Tanzania. Nawapongeza wote mlioshinda
tuzo mbalimbali za kitaifa na kimataifa mmekuwa mstari wa mbele kuitangaza nchi
yetu nje ya mipaka yetu kupitia usanii.
Tunajivunia kazi zenu.
Ndugu Wasanii,
Niwahakikishie kuwa siku zote tupo pamoja na nimekuwa nikifuatilia kazi
zenu mbalimbali, katika Luninga, kusikiliza Nyimbo, kuona michoro mbalimbali,
ubunifu katika mavazi na sanaa zinginezo. Kwa hakika ubora wa kazi zetu za
Sanaa naushuhudia ukiongezeka siku hadi hadi siku.
Ndugu Wasanii,
Kama mnavyojua mwaka huu 2015, Taifa letu linatarajia kuwa na matukio makubwa mawili,
kura ya maoni ya Katiba Inayopendekezwa na Uchaguzi Mkuu.
Serikali kwa kutambua
umuhimu wenu, imeona ikutane na wadau wa Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na
Michezo kwa lengo la kuelimishana na kukumbushana kuhusu jukumu letu kama
Wasanii katika kuelimisha na kuhamasisha
umma katika masuala mbalimbali muhimu
kwa taifa letu.
Katika Mkutano wa leo tutajikita zaidi katika
kuelimishana juu ya wajibu wenu kama Wasanii katika kuielimisha Jamii kuhusu
Katiba Inayopendekezwa na kujadili juu ya nafasi ya Sanaa/ Wasanii katika katiba
inayopendekezwa, ikiwemo haki mbalimbali za Wasanii.
Ndugu Wasanii,
Taifa linatarajia kuendesha kura ya maoni tarehe 30
Aprili mwaka huu na ili zoezi hili lifanikiwe kwa kiasi kikubwa taaluma na
nafasi yenu kama wasanii inahitajika
kutumika kwa ufasaha na umakini mkubwa.
Ni ukweli usiopingika kuwa ili wananchi waweze kufanya maamuzi
sahihi wakati utakapowadia ni vyema wakapata elimu kupitia
njia mbalimbali hususan kupitia sanaa juu ya katiba inayopendekezwa, bila
kusahau makundi yenye mahitaji maalum.
Tunafahamu kwamba mna washabiki wengi ambao kupitia Sanaa mnaweza
kuwaelimisha kuhusu mchakato wa upatikanaji wa Katiba Inayopendekezwa na
umuhimu wa ushiriki wao katika kuunga mkono Katiba Inayopendekezwa.
Ndugu Waasanii
Tumeona ni vyema sisi kama Wizara yenye jukumu la
msingi la kuelimisha jamii katika masuala makuu ya kitaifa pamoja na nyinyi
Wasanii tukawa na ufahamu wa kutosha juu ya mategemeo yetu kwenu katika jambo
hili muhimu la Kitaifa. Hasa la kuinadi Katiba Inayopendekezwa, kuhimiza
wananchi kujiandikisha na kujitokeza kwa wingi kupiga kura ya maoni.
Kama mnavyofahamu na watoa mada walivyowasilisha kwenu
kwamba katika Katiba Inayopendekezwa, yapo mambo mazuri yanayoendana na wakati
uliopo sasa ukilinganisha na Katiba ya Mwaka 1977. Naamini kabisa baada ya
kikao hiki, mmepata uelewa zaidi na ukweli kuhusu katiba Inayopendekezwa. Tumieni sasa nafasi yenu kuwafikia wananchi
kwa weledi na usahihi.
Waifahamu Katiba
Inayopendekezwa, wajiandikishe na kuipigia kura hapo ifikapo Aprili 30,
2015.
Ni ukweli usiopingika kuwa Katiba
Inayopendekezwa imesheheni haki za makundi mbalimbali bila kusahau kundi la
wasanii na haki zenu zilizofafanuliwa vizuri katika Ibara ya 59 ya Katiba
Inayopendekezwa. Hii inamaanisha kwamba
wasanii kwa mara ya kwanza kilio chenu kuhusu ulinzi na haki zetu kikatiba
umezingatiwa. Hivyo kazi zenu za ubunifu
zitaweza kulindwa kikatiba
Ndugu Wasanii,
Nimeelezwa Mada zilizowasilishwa na kujadiliwa leo, zimetolewa
na mtu mahiri ambaye alishiriki katika
Bunge Maalum la Katiba. Hivyo ni
matumaini yangu kwamba kupitia kwake
tutaongeza uelewa wetu juu ya wajibu wetu na umuhimu wa Katiba Inayopendekezwa.
Ni matumaini yangu kwamba tumesikiliza, tumeuliza maswali, tumejadili na kutoa
maoni ambayo yatatusaidia kutoa elimu sahihi kwa umma. Hasa kwa kuisemea na kuitangaza Katiba
Inayopendekezwa kwa mlengo wa kuvuka katika kura ya maoni na wingi wa kura ya
Ndiyo.
Ndugu Wasanii,
Kwa mara nyingine nitumie nafasi hii kipekee
kuwashukuru na kuwapongeza kwa kazi nzuri mnayoendelea kuifanya ya kuelimisha
na kuburudisha Jamii bila kusahau kulitangaza Taifa la Tanzania .
Mwisho nawaomba sana tusaidiane katika kufanikisha
hili jambo muhimu tuweze kuendelea kujipanga vizuri katika kujenga na kuilinda
nchi yetu.
Niwashukuru tena kwa kuja na kushiriki nasi na niwatakie kazi njema ya
kulijenga Taifa letu.






No comments:
Post a Comment