TANGAZO


Monday, January 5, 2015

Naibu Waziri wa Maji Amos Makala afanya ziara ya kushtukiza Boko jijini Dar es Salaam

Naibu Waziri wa Maji, Amos Makala (watatu kushoto), akiwa amefuatana na wajumbe wa Bodi, Menejimenti, Watendaji wa Mamlaka ya Maji safi na Maji Taka Dar es Salaam (Dawasco), waandishi wa habari na wakazi wa Boko, wakati alipofikia maeneo hayo yenye matatizo ya maji jana, katika ziara ya kushtukiza kuangalia chanzo cha tatizo la wananchi kukosa huduma hiyo.
Naibu Waziri wa Maji, Amos Makala (wapili kushoto), akiwa amefuatana na wajumbe wa Bodi, Menejimenti, Watendaji wa Mamlaka ya Maji safi na Maji Taka Dar es Salaam (Dawasco), waandishi wa habari na wakazi wa Boko, wakati alipofikia maeneo hayo yenye matatizo ya maji jana, katika ziara ya kushtukiza kuangalia chanzo cha tatizo la wananchi kukosa huduma hiyo. 
Naibu Waziri wa Maji, Amos Makala (katikati) pamoja na wananchi wakishuhudia moja ya eneo ambalo linahusishwa na kuhujumu maji katika eneo la Boko jana jijini Dar es Salaam. (Picha zote na Eleuteri Mangi-MAELEZO)

Na Eleuteri Mangi- MAELEZO, 05/01/2015
NAIBU Waziri wa Maji Amos Makala ameiagiza Bodi na Menejimenti ya Mamlaka ya Maji Safi na Maji Taka ya jiji la Dar es salaam (DAWASCO) kuviwezesha vitengo vya Habari na Biashara ili vifanye kazi karibu na wananchi.

Naibu Waziri Makala alisema hayo mwishoni mwa wiki alipofanya ziara ya kushtukiza ya kukagua na kujionea namna miundo mbinu ya maji ya DAWASCO inavyohujumiwa na baadhi ya watu wachache na kuwakosesha wananchi waliowengi huduma muhimu ya maji katika maeneo yao wanakoendesha maisha yao ya kila siku.

“Kumekuwa na mawasiliano mabovu kati ya baadhi ya viongozi wa DAWASCO na wananchi, ni lazima mbadilike na kila mmoja atoe taarifa kwa wananchi ili wawe wanajua tatizo la wao kutokupata maji ni nini na litatatuliwa linatatuliwaje” alisema Makala. 

Akizungumza na wakazi wa Boko jijini Dar es salaam, Makala alisema kuwa viongozi wanamaelezo mazuri ila hawana mawasiliano mazuri na wananchi pia wawe na lugha nzuri kwa wateja wao wanapofika ofisini kuhitaji huduma ya kuunganishiwa maji, kutoa kero zinazowasibu au tatizo la miundo mbinu ya maji kwenye maeneo yao inayosababisha upotevu wa maji mengi bila sababu.  

Aidha, wakati wa ziara hiyo Naibu Waziri Makala aliwasimamisha kazi Meneja wa DAWASCO eneo la Boko Robert Mugabe na Meneja wa Kimara Peter Chacha na kuagiza Bodi na Menejimenti ya DAWASCO kuwapangia kazi nyingine na nafasi zao zijazwe mara moja.

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa DAWASCO alisema kuwa operesheni ya wahujumu maji Dar es salaam itakuwa ni endelevu, wale wote waliokamatwa watafikishwa kwenye vyombo vya sheria na sheria itachukua mkondo wake.

Ziara ya Naibu Waziri Makala akifuatana na wajumbe wa Bodi na Menejimenti, watendaji wa DAWASCO na waandishi wa habari ilianzia kukagua maeneo yenye matatizo maji ambayo yanapelekea wananchi kukosa maji ya maeneo mbalimnbali jijini Dar es salaam yakiwemo Mgomeni, Manzese, Boko na kuhitimisha ziara hiyo maeneo ya Kimara.

No comments:

Post a Comment