Msanii wa muziki Bongo Fleva, Nassib Abdul 'Diamond'
Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dr. Jakaya Mrisho Kikwete amewapongeza mwanamuziki
Nassib Abdul maarufu kwa jina la Diamond na Mshindi wa Shindano la Big Brother
Africa, Idris Sultan kwa kuiletea sifa Tanzania kupitia sanaa.
Rais
Kikwete ametoa Pongezi hizo alipokutana na Msanii Diamond Ikulu jijini Dar es
salaam leo Jumanne Desemba 23, 2014 , ambapo Msanii huyo amemwonyesha tuzo tano
alizoshinda baada ya kupambanishwa na wasanii wengine wa Afrika.
Pamoja
na pongezi hizo kwa Diamond na Idris kwa kile alichosema wameitoa nchi
kimasomaso, Rais Kikwete amewasihi wasanii hao kujihadhari na athari za umaarufu
na utajiri katika umri mdogo,zikiwemo kujitumbukiza katika matumizi ya dawa za
kulevya na ulevi.
Kikwete
amewaasa kuwa ni muhimu kwa wasanii hao kutumia mapato wanayoyapata katika kazi
zao za usanii kwa kujijenga kifamilia ikiwa ni pamoja na kujenga nyumba zao za
kuishi na wanafamilia wanaowategemea pamoja kuwasaidia wasanii wenzao.
“Umaarufu
katika sanaa yoyote ile ni wa kupita hivyo tumieni umaarufu mlio nao sasa kama
fursa ya kujijenga kimaisha na sio kutumbukia katika kadhia za kidunia kama
vile ulevi, ukorofi mbele ya jamii na mambo mengine yasiyofaa",
aliwaasa Mhe. Rais.
Rais
Kikwete pia alimpongeza Sultan kwa
kuiletea Tanzania sifa na kumtakia mafanikio zaidi katika shughuli zake za
baadaye. Rais Kikwete alisema kuwa Sultan hakuifedhehesha Tanzania kwa
kutofanya mambo yaliyo kinyume na maadili ya Mwafrika alipokuwa katika jumba la
Big Brother Africa.
Kwa
upande wake,Diamond amemshukuru na kumpongeza Rais Kikwete kwa ushirikiano
anaoutoa kwa wasanii hapa nchini, hali ambayo amesema ndiyo
iliyowawezesha kupata mafanikio kitaifa na kimataifa.
Diamond
pia amemuahidi Rais Kikwete kutekeleza yote aliyomuasa kuhusu kujiheshimu na
kutolewa umaarufu alionao, na kwamba ataendelea kufanya kazi zake za usanii wa
Muziki kwa juhudi zake zote kuitangaza nchi.
Msanii
huyo pia amemweleza Rais Kikwete kuwa hivi karibuni atapokea tuzo nyingine ya
sita kutoka huko Nigeria.
Imetolewa
na:
Kurugenzi
ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu – Dar es
Salaam.
23
Desemba,2014
No comments:
Post a Comment