Katibu wa Ngara Saccoss
Bw.Joackim Jordan (wapili kushoto) akiwaonesha
Maofisa wa Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo walipowatembelea
hivi karibuni baadhi ya tofali aina ya vibrated
blocks zinazotengenezwa kwa udongo na simenti ambazo vikundi kumi vya
vijana vilipata mafunzo ya kutengeneza matofali hayo kama sehemu ya miradi wanayofanya. Kulia ni Mwenyekiti wa
kikundi cha vijana cha Hekima Group Ngara
Bw. George Kessy. (Picha zote na
Anitha Jonas – Maelezo)
Na Anitha Jonas – Maelezo
KIKUNDI cha vijana cha Ngara Youth Foundation chenye wanachama
wapatao kumi na moja waliomaliza
elimu ya juu wamenufaika baada ya
kupata mkopo wa Milioni tano kupitia mfuko
wa Maendeleo ya Vijana na kuanzisha miradi miwili ikiwemo mradi wa kuuza
mbao na mradi wa kuosha magari.
Hayo yalisemwa jana na
Katibu wa kikundi hicho Bw. Jason Athanas alipotembelewa na maafisa kutoka
Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo kutathimini miradi inayoendeshwa na vikundi
baada ya kupatiwa mkopo kwa ajili ya kujikwamua kiuchumi kutokana na changamoto ya ajira iliyopo
nchini.
Kikundi hicho
kimeishukuru Serikali kwa kuwapatia
mkopo uliopelekea kuongeza kipato
kwa kila mwanachama hivyo kuboresha hali
ya maisha baada ya kukosa ajira na
kuwafanya kuwa wabunifu katika jamii.
“Tuliamua kuanzisha
kikundi hiki baada ya kumaliza chuo na kutafuta ajira kwa muda mrefu hivyo
tuliamuamu kuungana kuanzisha kikundi chetu ambapo tulibuni mradi tulioona
unafaa na kuomba mkopo, kwa sasa tuna
miradi miwili ambayo ni mradi wa kuuza mbao na wakuosha magari (Car
Wash)”,alisema Bw. Athanas.
Naye Mkurugenzi Msaidizi
Tathmini na Ufuatiliaji kutoka Wizara ya Habari, Vjana, Utamaduni na Michezo Bibi.Verdiana Mushi, aliwapongeza
vijana hao kwa juhudi kubwa wanazozifanya na kutoa wito kwa vijana wengine kuiga mfano wa vijana hao kwa
kuanzisha vikundi vyao na kuomba mkopo katika mfuko wa maendeleo ya vijana unaosimamiwa
na Wizara.
Aidha Ofisa
Vijana kutoka Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na
Michezo Bw. Eliakim Mtawa
aliwashauri vijana wa Ngara Youth Foundation kuendelea kufanya kazi kwa bidii na kwa ubunifu huku
wakizingati matumizi mazuri ya mapato yanayotokana na miradi yao pamoja na
kuendelea kutafuta vyanzo mbalimbali vya
fedha kukua kiuchumi na kukuza miradi ya kikundi.
No comments:
Post a Comment