Jeshi nchini Libya limetaka wakazi wa mjini Benghazi kuondoka mjini humo kabla ya operesheni ya nchi hiyo dhidi ya wanamgambo wa kiislamu kuanza.
Zaidi ya watu 200 waliuawa mjini humo tangu Jeshi lilipoanza operesheni za kuudhibiti mji wa Benghazi kutoka mikononi mwa wanamgambo mwezi uliopita.
Kampeni hizo za sasa zinaongozwa na Jenereali Khalifa Haftar ambaye inaripotiwa anaungwa mkono na jeshi.
Libya imekua katika hali ya machafuko tangu kuangushwa utawala wa Kanali Gaddafi mwaka 2011.
Libya imegawanyika katika mfumo wa serikali mbili hasimu, pia makundi ya waasi ya kikabila,wanamgambo, na makundi ya kisiasa yamekua yakipigania madaraka ya nchi hiyo.
Serikali mpya inayotambuliwa kimataifa imelazimika kuhamia mashariki mwa Libya mjini Tobruk karibu na mpaka wa nchi hiyo na Misri, baada ya kuondolewa mjini Tripoli,wanamgambo waliposhambulia mji huo mwezi julai.
Makundi ya kiislamu likiwemo la Ansar al-Sharia , ambalo limeorodheshwa na nchi za magharibi ikiwemo Marekani kuwa kundi la kigaidi yameutangaza mji wa Derna kuwa himaya yao.
No comments:
Post a Comment