Rais wa Tanzania Jakaya Kikwete leo amezindua ujenzi wa kituo cha vijana cha michezo cha kimataifa mjini Dar es Salaam.
Mwandishi wa BBC Baruan Muhuza aliyehudhuria shughuli hiyo amesema kuwa mradi huo unagharamiwa kwa pamoja na kampuni ya nishati ya umeme Symbion Power ya Marekani na klabu ya soka ya Sunderland inayoshiriki ligi kuu ya England.
Katika sherehe za uzinduzi huo kwenye eneo la Kidongo Chekundu Mnazi Mmoja Rais huyo aliungana kwa pamoja na Afisa Mtendaji Mkuu wa Sunderland Margaret Bryne na Afisa Mtendaji Mkuu wa Symbion Power Paul Hinks.
Akizungumza katika shughuli hiyo Bryne alisema “Tunafurahia kuwa hapa Tanzania leo na kuona maendeleo yanayofanywa na mradi huu.
Uwanja huu wa michezo ni sehemu ya msingi wa ushirikiano wa kipekee kati yetu na kandanda ya Tanzania, ni furaha kuona kituo hiki kikijengwa.”
Kituo hicho kitakapokamilika mwezi machi 2015 kitakuwa na uwanja mkubwa wa soka wenye nyasi za bandia za kiwango cha kimataifa cha 3G, uwanja wa wachezaji watano kila upande, viwanja viwili vya mchanga na uwanja wa mpira wa kikapu na wavu.
Katika mradi huu kampuni ya Symbion Power inagharamia ujenzi wa kila kitu katika kituo hicho huku Klabu ya Sunderland ikitoa wataalamu wa ufundi na mafunzo ya soka kwa watoto na vijana.
Akihutubia umma wa watu waliojitokeza katika shughuli ya uzinduzi huo, Rais Kikwete alieleza matumaini yake ya matunda yatakayotokana na mradi huo, huku akielezea jinsi alivyopata wazo la kuanzishwa kwa kituo hicho ambacho kimepewa jina lake.
No comments:
Post a Comment