TANGAZO


Friday, October 3, 2014

Taasisi ya Co-operation for Assisting Handcapped People yahitaji Sh. Bilioni 5 kujenge mabweni ya Shule za Kata

Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Watu Wasiojiweza Tanzania (CAHPT), Mhina Shengena, akizungumza na waandishi wa habari, Dar es Salaam jana kuhusu kuwataka watu wenye uwezo pamoja na Kampuni mbalimbali kuwasaidia katika kampeni yao ya ujenzi wa mabweni kwa Shule za Sekondri za Kata Tanzania Bara. Kulia ni Ofisa Habari wa Idara ya Habari, Maelezo, Beatrice Lyimo. (Picha na Kassim Mbarouk-www.bayana.blogspot.com)

Na Beatrice Lyimo, Maelezo Dar es Salaam
02.Oktoba, 2014

TAASISI ya Co-Operation For Assisting Handcapped People Tanzania imepanga kukusanya kiasi cha Tsh. Bilioni 5 kwa ajili ya kufanikisha mpango wa taasisi hiyo ya kujenga mabweni ya wanafunzi wa kike na Kiume katika Shule za Sekondari za Kata Nchini.
Wilaya ya Temeke inatajwa kuwa Halmashauri ya kwanza itayoweza kunufaika na mpango huo kutokana  na ukubwa na idadi ya shule zilizopo katika eneo hilo.
Akizungumza na Waandishi wa Habari jana, Alhamisi (Okt 2, 2014) Jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi hiyo, Mhina Shengena alisema fedha hizo zitaweza kukusanywa kupitia harambee mbalimbali zitakazofanywa na Ofisi yake ndani na nje ya nchi.
Kwa mujibu wa Shengena alisema taasisi hiyo imepanga kukusanya kiasi cha Tsh. 2400 kwa mwezi kutoka kwa kila Mtanzania pamoja na kupitia kwa waajiri na taasisi mbalimbali na mara baada ya kufanikiwa kukusanya fedha hizo, ujenzi wa makazi ya wanafunzi hao unatarajiwa kuanza mara moja.
“Wanafunzi wetu hususani wa kike wanaishi katika mazingira hatarishi sana, wapo baadhi wamepanga katika makazi ya watu mara kwa  mara tumekuwa tukisikia  matukio ya wao kubakwa na kupewa mimba, hii yote inatokana na ukosefu wa makazi ya kudumu” alisema Shengena.
Aidha Shengena aliipongeza Serikali kupitia Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa pamoja na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi kwa msaada na ushirikiano wa karibu wanaonyesha kwao katika kufanikisha malengo ya Taasisi hiyo.
Aliongeza kuwa Ofisi yake tayari imekwishafanya mawasiliano na Watanzania mbalimbali waliopo nje ya Nchi ambao baadhi yao wameonyesha nia ya dhati ya kusaidia harambee ya ujenzi huo, ikiwemo Watanzania wanaoishi nchini Uingereza.
 
Akifafanua zaidi Shengena alisema kwa Watanzania walioopo nchini wanaweza kutuma michango yao katika Benki ya Posta Tanzania (TPB) katika akaunti na. 016-002156 Tawi la Kijitonyama Jijini Dar esa Salaam na kwa wale waliopo nje ya nchi watume michango hiyo katika benki ya CRDB kwa akaunti na. 01j2070153800.  
Shengena alisema suluhu ya elimu bora kwa mtoto wa kike na kiume Tanzania ni ujenzi wa mabweni, na hivyo aliwataka Watanzania wote waguswe na kilio cha watoto hao ambao ni taifa la kesho.
Taasisi ya Co-Operation For Assisting Handcapped People Tanzania, ni taasisi isiyo ya kiserikali iliyoanzishwa mwaka 1998 na inajishughulisha katika kusaidia makundi ya watu wasiojiweza ikiwemo yatima, walemavu na watoto wanaoishi katika mazingira magumu na hatarishi.
 

No comments:

Post a Comment