Mkurugenzi
wa Takwimu za Uchumi wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu, Bw. Morrice Oyuke (katikati),
akizungumza na waandishi wa habari, kuhusu ukuaji wa Pato la Taifa kwa bei
ya Soko leo jijini Dar es Salaam. Wengine ni Bw. Fred Matola, Mtakwimu Mkuu
Takwimu za Uchumi (kushoto), Bi. Adella Ndesangia (wa pili kutoka kulia) ambaye
ni Mtwakimu Mkuu wa Ofisi hiyo na Bi. Jovitha Rugemalila. (Picha na Aron Msigwa – MAELEZO)
Na Aron Msigwa – MAELEZO
3/10/2014. Dar es salaam.
Sekta za Kilimo, Viwanda,
Biashara za jumla na rejareja zimetajwa kuongoza katika kuchangia kukua kwa
pato la Taifa kwa asilimia 6.9 katika kipindi cha robo ya pili ya mwaka 2014.
Akitoa taarifa ya kukua
kwa pato la Taifa leo jijini Dar es salaam, Mkurugenzi wa Takwimu za Uchumi wa
Ofisi ya Taifa ya Takwimu, Bw. Morrice Oyuke amesema kuwa kuanzia mwezi Aprili
hadi Juni 2014 sekta hizo zimetoa mchango mkubwa wa kukuza pato la Taifa.
Amesema ukusanyaji wa
taarifa kutoka vyanzo mbalimbali vya uzalishaji uliofanywa na wataalam wa Ofisi
ya Taifa ya Takwimu kwa kuzingatia kanuni za kimataifa za kukokotoa pato la
Taifa unaonyesha kuwa jumla ya thamani
ya pato hilo imefikia kiasi cha shilingi trilioni 5.4 ikilinganishwa na
trilioni 5.0 za mwaka 2013.
Bw. Oyuke amesema katika kipindi hicho shughuli za kilimo cha
mazao zimekua na kufikia asilimia 6.5 ikilinganishwa na 5.4 za mwaka uliopita huku mifugo ikifikia asilimia
0.9, misitu na uwindaji zikifikia
asilimia 0.8, shughuli za uvuvi zikikua
kwa asilimia 2.1.
Ameongeza shughuli za
uchimbaji wa madini ya Almasi, Tanzanite, mawe, na kokoto zimechangia kukua kwa
pato la taifa kwa kasi ya asilimia 3.0
katika kipindi hicho ikilinganishwa na asilimia 2.6 za kipindi kilichopita.
Aidha, amesema sekta ya
uzalishaji wa bidhaa za viwandani imekua kwa asilimia 7.0 ikilinganishwa na 6.6
za mwaka uliopita kutokana na kuongezeka kwa uzalishaji na uhifadhi wa bidhaa
za nyama, samaki, matunda, mboga za majani na mafuta.
Shughuli nyingine
zinahusisha uzalishaji wa bidhaa za vyakula, nguo na simenti, utoaji wa huduma
na uchumi zikiwemo za ukarabati wa magari, pikipiki na vifaa vingine vya
majumbani zikikua kwa asilimia 7.1 ikilinganishwa na asilimia 6.6 ya kipindi
kama hicho kwa mwaka 2013.
Bw. Oyuke ameeleza kuwa
shughuli za uchukuzi na mawasiliano zimekua na kufikia asilimia 16.8 katika kipindi hicho huku huduma
za hoteli na migahawa zikifikia kasi ya ukuaji wa asilimia 4.0, shughuli za
uendeshaji wa Serikali zikiwa asilimia 4.8, Elimu asilimia 6.3, huduma za afya
na shughuli nyingine zikikua kwa asilimia
4.8.
Amebainisha kuwa sekta ya
umeme katika robo ya pili mwaka 2014 imeendelea kukua kutokana na kupatikana
kwa vyanzo mbadala vya kuzalisha umeme hususan ugunduzi na matumizi ya gesi
nchini ambayo yameondoa tatizo la utegemezi wa umeme wa maji katika kuzalisha.
“Kwa kipindi kirefu
sekta ya umeme imekuwa na mawimbi kwa kiasi kikubwa , umeme wetu umekuwa wa
kutegemea maji ya mvua, baada ya juhudi za Serikali na kugundulika kwa nishati
ya Gesi nchini na kupatikana chanzo mbadala cha nishati tatizo hili
limeshghulikiwa sasa sekta hii imeimarika” Amesema.
Amesema Tanzania sasa
inafanya vizuri kiuchumi katika nchi za Afrika ya Mashariki kwa kuendelea
kushika nafasi ya pili ikifuatiwa na Uganda, Rwanda na Burundi na kuongeza kuwa
hali ya amani na utulivu iliyopo nchini inaiweka Tanzania katika nafasi nzuri
ya kukua zaidi kiuchumi.
Aidha amefafanua kuwa katika Afrika Mashariki,
Tanzania inaendelea kufanya vizuri katika sekta ya utalii kwa kuwa na ongezeko la
idadi ya watalii wanaoingia nchini kutokana na hali ya usalama na amani iliyopo.
No comments:
Post a Comment