TANGAZO


Monday, October 6, 2014

Hofu ya baa la njaa Sudan Kusini

Maelfu ya wamekuwa wakipokea chakula cha msaada kutoka kwa mashirika ya misaada
Mashirika ya kimataifa ya misaada yameonya kuwa huenda Sudan Kusini ikakabiliwa na baa kubwa la njaa mapema mwakani iwapo, mapigano nchini humo hayatasitishwa.
Mashirika hayo yanaonya kuwa hakuna dalili za mapigano hayo yaliyodumu zaidi ya miezi tisa kumalizika, huku pande zote mbili zikiendelea kujihami.
Katika ripoti mpya, mashirika hayo yanasema idadi ya watu wanaokabiliwa na njaa itaongezeka kwa milioni moja kufikia miezi mitatu ya kwanza mwaka wa 2015.
Ni wiki chache tuu ambapo Umoja wa Mataifa ulisema kuwa Sudan Kusini imeepuka tisho la njaa mwaka huu, kufuatia juhudi za kimataifa kutoa msaada na ufadhili.
Licha ya taarifa hiyo ya Umoja wa Mataifa, mwandishi wa BBC wa maswala ya Sudan Kusini Emmanuel Igunza anasema kuwa hofu ya mashirika hayo ni kwamba hali itazorota kutokana na mapigano hayo ambayo yamekuwa yakiendelea
Mashirika hayo yanakadiria dadi ya wanaokabiliwa na upungufu wa chakula itaongezeka kwa milioni moja kati ya mwezi Januari na machi mwaka ujao.
Licha ya msaada huu hali heunda ikawa mbaya zaidi kutokana na vita vinavyoendelea
Hii, wanasema ni kutokana na dalili kuwa mapigano nchini Sudan Kusini yataendelea baada ya msimu wa mvua, ambao ulikuwa umetuliza joto nchini humo.
Ripoti hiyo inasema hali nchini Sudan Kusini inaendelea kuwa mbaya zaidi, huku watu milioni moja unusu waliofurushwa makwao, wakiendelea kukumbwa na uhaba wa chakula.
Bei ya vyakula katika masoko ambayo yamesalia pia ni ghali mno, na tayari watu wamekula mbegu walizotarajiwa kupanda msimu wa mvua.
Aidha wengine wamekuwa wakila matunda na majani ya misituni, kutokana na njaa.
Mashirika hayo sasa yametaka jamii ya kimataifa kushinikiza pande mbili hasimu kusitisha mapigano na kuhakikisha kuwa msaada wa dharura unawafikia wale wanaouhitaji.
Maelfu ya watu wamefariki na wengine zaidi ya laki moja unusu kufurushwa makwao kufuatia mapigano hayo yaliyozuka mwezi Disemba mwaka 2013.

No comments:

Post a Comment