TANGAZO


Saturday, September 20, 2014

Ujumbe wa Chama cha Frelimo cha Msumbiji chakutana na baadhi ya wajumbe wa Chama Cha Mapinduzi Zanzibar



Mjumbe wa Kamati ya CCM Taifa Bi. Khadija Hassan Aboud akimkaribisha Mbunge ambae pia ni Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chama cha FRELIMO cha Msumbiji Bi. Nyeleti Mondlane Ofisi kuu ya CCM Zanzibar.
Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chama cha FRELIMO cha Msumbiji Bi. Nyeleti Mondlane akisaini kitabu cha wageni alipofika Ofisi kuu ya CCM Zanzibar (kulia) Katibu wa FRELIMO Zanzibar Bw. Agostino Andrea.
Kiongozi wa Ujumbe wa Chama cha FRELIMO Bi. Nyeleti Mondlane (watatu kushoto) akibadilishana mawazo na wenyeji wake wajumbe wa Chama cha Mapinduzi katika Ofisi Kuu Kisiwandui Zanzibar ikiwa ni mkakati wa kuimarisha Uhusiano wa Vyama vyao na kuzindua Kampeni ya Uchaguzi Mkuu Nchini Msumbiji.
Picha ya pamoja ya Ujumbe wa Chama cha FRELIMO na baadhi ya wajumbe wa Chama cha Mapinduzi CCM wakiongozwa na Mjumbe wa Kamati ya CCM Taifa Bi. Khadija Hassan Aboud wakatikati. (Picha zote na Makame Mshenga-Maelezo Zanzibar)

Na Makame Mshenga-Maelezo Zanzibar

CHAMA cha FRELIMO kimesema Wananchi wa Msumbiji wataendelea kukumbuka na kuthamini juhudi mbali mbali zilizochukuliwa na Watanzania wakati wa harakati za ukombozi na kuwafanya kuwa watu huru.

Kauli hiyo imetolewa na Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chama cha FRELIMO Bibi Nyeleti Mondlane, alipokuwa na mazungumzo maalum na Uongozi wa CCM Zanzibar, hapo Afisi Kuu ya CCM, Kisiwandui.

Amesema Wananchi wa Msumbiji wana kila sababu ya kuwapongeza Watanzania kutokana na misaada yao ya hali na mali, jambo lililosaidia kwa kiasi kikubwa wananchi wa Msumbiji kujikomboa na kuishi wakiwa watu huru ndani ya nchi yao huru.



Mjumbe huyo wa Kamati Kuu ya FRELIMO na pia ni Mbunge, amesema nchi hiyo imo katika amani na utulivu mkubwa, hali inayotoa fursa kwa Serikali ya FRELIMO  kuweza kufanikisha shughuli za kimaendeleo kwa maslahi ya wananchi na Taifa kwa ujumla.

Ametumia kikao hicho kutoa wito kwa Wana FRELIMO wanaoishi Zanzibar kuendeleza mashirikiano ya karibu na wananchi wa Tanzania, CCM na Serikali zake, ili umoja na maendeleo kwa wananchi wa pande zote mbili.

Naye Mjumbe wa Kamati Kuu ya Taifa ya CCM Mhe. Khadija Hassan Aboud, amemuhakikishia Bibi Mondlane kuwa Chama Cha Mapinduzi kitafanya kila linalowezekana kuhakikisha uhusiano wa kihistoria baina ya CCM na FRELIKO unaendelezwa kwa nguvu zote.

Amesema Vyama vya CCM mrithi wa ASP na FRELIMO, vina undugu wa kihistoria uliodumu kwa miaka mingi na kumesisitiza haja kwa Viongozi wa Vyama hivyo wanapaswa kuuendeleza na kuudumisha kwa manufaa ya wananchi wa nchi hizo.



Bibi Mondlane yupo Visiwani Zanzibar kwa ziara ya kikazi ya kichama, ambapo katika mazungumzo hayo aliongoza Ujumbe wa watu watano, akiwemo Balozi Mdogo wa Msumbiji nchini Zanzibar Bwana Jorge Augusto Menezes.

No comments:

Post a Comment