TANGAZO


Saturday, September 20, 2014

Shule za Sekondari Mkoa wa Mara zakabiliwa na changamoto nyingi

*Wanafunzi wanaoanza kidato cha kwanza hawajui kusoma na kuandika


Ofisa elimu wa shule za msingi katika wilaya ya Bunda, Jeshi Pembe (aliyesimama) akifungua kikao cha wakuu wa shule za sekondari mkoani Mara, kwa niaba ya mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya Wilaya ya Bunda. Aliyevaa miwani wa pili kulia ni mwenyekiti wa umoja huo mkoani humo. (Picha na Ahmed Makongo)

Na Ahmed Makongo, Bunda;

Sept 20, 2014;

SHULE za Sekondari katika Mkoa wa Mara, zinakabiliwa na changamoto nyingi za kitaaluma, ikiwa ni pamoja na baadhi ya wanafunzi wanaomaliza elimu ya msingi na kjiunga na sekondari hizo, kutokujua kusoma na kuandika.

Changamoto hizo zilitolewa jana na wakuu wa shule hizo katika kikao chao cha umoja wa wakuu wa shule za sekondari Tanzania (Tahossa) Mkoani Mara, kilichofanyika mjini Bunda.


Walimu hao walisema kuwa shule hizo zinakabiliwa na changamoto nyingi, ikiwemo hiyo ya wanafunzi wanaomaliza elimu ya msingi na kujiunga katika kidato cha kwanza, wakiwa hawajuhi kusoma, kuandika na kuhesabu yaani kkk tatu.


Baadhi ya walimu hao walisema kuwa shule zao zinakabiliwa na changamoto nyingi sana ikiwemo ya kupokea wanafunzi wanaoanza kidato cha kwanza wakiwa hawahui kusoma, kuandika wala kuhesabu (KKK 3)

“Taaluma itazidi kushuka kutokana na hali hiii ya kupokea wanafunzi wakiwa hawajui kusoma, kuandika wala kuhesabu yaani hizi kkt tatu” alisema mmoja wa walimu hao.


Walisema kuwa hali hiyo imekuwa ikiwapa wakati mgumu wa kufundisha watoto hao na kwamba hata kipindi hiki cha mitihani ya kumaliza darasa la saba walibaini kuwepo kwa watoto wa aina hiyo.

Walisema kuwa changamoto nyingine ni kwa walimu wa shule za sekondari za binafsi, kutokupewa kipaumbele katika kusimamia mitihani ya kitaifa na badala yake upendeleo kupewa walimu wa shule za serikali tu.

Aidha, walisema kuwa suala jingine ni shule za serikali kutumia mbinu na kuwachukuwa walimu wanaofundisha katika shule binafsi.

Walisema kuwa ipo haja ya serikali kuhakikisha shule binafsi nazo zinathaminiwa kwani zina mchango mkubwa kwa taifa ili katika kutoa elimu kwa watoto wa nchi hii.

Awali akisoma taarifa ya kikao hicho kinachoshirikisha walimu wakuu wote 189 wa shule za sekondari zilizoko mkoani Mara, mwenyekiti wa umoja huo Jonathan Masambu, alisema kuwa madhumuni ya kikao hicho pamoja na mambo mengine ni kupeana uzoefu kuhusu uendeshaji wa shule za sekondari.


Adiha, Masambu alizitaja baadhi ya changamoto zinazozikabii shule hizo, ambazo kwa namna moja ama nyingine zimekuwa zikiathiri umoja wao, kuwa ni pamoja na ulipaji wa ada na michango ya shule kutoka kwa wanafunzi wao kuwa wa kusuasua.


Alisema hali hiyo imekuwa ikisababisha baadhi ya wanafunzi humaliza kidato cha nne wakiwa wameacha madeni makubwa.


Alisema kuwa nyingine ni pamoja na ufinyu wa fedha za ruzuku na fedha za fidia ya ada kutoka serikali kuu, kwa kutokufika katika shule hizo kwa wakati muafaka.

Aliongeza kuwa nyingine ni kushuka kwa nidhamu kwa wanafunzi na baadhi ya walimu, ikiwa ni pamoja na badhi ya wakuu wa shule kutokuhudhuria kwenye vikao bila sababu za msingi, hali ambayo husababisha shule husika kuwa kisiwa na kuwanyima fursa walimu kutokupata huduma zitolewazo na Tahossa.


Akifungua kikao hicho mgeni rasmi, Jeshi Pembe, ambaye ni afisa elimu wa shule za msingi wilayani hapa, aliyemwakilisha mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Bunda,  aliwataka wakuu wa shule hizo kutekelezwa wajibu wao ipasavyo, ili kuinua kiwango cha taaluma.

Jeshi alisema kuwa kitaaluma mkoa wa Mara, uko nyuma sana ikilinganishwa na mikoa mingine hapa nchini, ikiwemo mikoa ya kasikazini.

Alisema kuwa ni jukumu la kila mwananchi na viongozi wote mkoani hapa, kuhakikisha kiwango cha taaluma kinapanda kwa kasi kubwa, kwa sababu elimu ndio msingi wa maisha.

No comments:

Post a Comment