*Utekelezaji
wa miongozo ya Luanda kuimarisha haki za binadamu nchini
UTEKELEZAJI wa Miongozo ya Luanda
(Luanda Guidelines) kuhusu ukamataji
na ushikiliaji wa watuhumiwa kabla ya kufunguliwa mashtaka utakaoanza hivi
karibuni unatarajiwa kuimarisha haki za watuhumiwa na mahabusu nchini.
Aidha, miongozo hiyo inatarajiwa
kuipunguzia Serikali mzigo mkubwa wa gharama za uendeshaji wa mahabusu na
magereza ambayo mengi yao yana msongamano mkubwa wa watuhumiwa na wafungwa.
Kutokana na tafiti zilizofanyika barani
Afrika ikiwemo Tanzania imebainika kuwa, kuna uvunjifu mkubwa wa haki za
binadamu kwenye mchakato mzima wa mfumo wa haki–jinai (criminal justice) ambao
unaanzia pale mtu anapokamatwa na vyombo vya dola (arrest), wakati wa mahojiano
(interrogation) na hata anapokuwa mahabusu katika vituo vya polisi na
magerezani.
Kwa mujibu wa taarifa za
kiutafiti, wengi wao wanakamatwa pasipo utaratibu, kudhalilishwa, kuteswa,
kubambikiwa kesi, kuwekwa muda mrefu bila kufikishwa mahakamani na kuwepo
mazingira magumu ya dhamana jambo linalokiuka haki za binadamu zilizoainishwa
katika Ibara ya 12 mpaka 24 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya
mwaka 1977, sheria nyinginezo za nchi pamoja na Mikataba ya Kimataifa ambayo
nchi imeridhia.
Miongozo hii inatanabaisha namna
binadamu walioko katika hali na mazingira tajwa wanapaswa kuangaliwa kulingana
na taratibu, kanuni na sheria zenye vigezo na viwango vya kitaifa na kimataifa
kuhusu haki za binadamu.
Miongozo hii inahimiza
uzingatiaji wa haki za binadamu katika mfumo wa haki-jinai - yaani katika hatua
ya ukamataji na uhifadhi wa watuhumiwa wa uhalifu kabla hawajafikishwa
mahakamani (Arrest and Pre-Trial detention) kama vile mahabusu za polisi na
magereza
Kwa mujibu wa matokeo ya utafiti
uliofanywa hivi karibuni na Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB)
kwa kushirikiana na Mtandao wa wataalamu wa masuala ya kipolisi kutoka taasisi
za Serikali na zisizo za Kiserikali Afrika (African Policing Civilian Oversight
Forum – APCOF) yenye makao yake makuu nchini Afrika Kusini asilimia 50 ya watu wanaoshikiliwa
maeneo mbalimbali nchini ni mahabusu ambao, ama wanasubiri kufikishwa
mahakamani au kesi zao bado zinaendelea katika mahakama mbalimbali (yaani hawajahukumiwa).
Hali hii inaisababishia Serikali gharama kubwa za uendeshaji wa taasisi hizo.
Kuanza kutekelezwa kwa Miongozo
hii ya Luanda kutaipunguzia Serikali gharama za uendeshaji kutokana na kupungua
kwa idadi ya watu watakaokuwa wakishikiliwa vizuizini kwa kuwa wengi wengi wao
wanashikiliwa kwa makosa ambayo yana dhamana (bailable offences) yakiwemo
makosa madogo madogo kama vile wizi mdogo mdogo na kadhalika
Athari za watu kushikiliwa
vizuizini pasipo ulazima ni pamoja na Serikali kuendelea kubeba mzigo mkubwa wa
gharama za uendeshaji, watuhumiwa wa uhalifu (mahabusu) kupata magonjwa ya
kuambukizwa kutokana na msongamano, kupata ulemavu na hata kufariki kutokana na
mateso pale ambapo watumishi wa vyombo vya dola wanapotumia nguvu kupita kiasi
wakati wa ukamataji na mahojiano.
Athari za kiuchumi ni pamoja na familia
nyingi huathirika kwa kukosa mahitaji muhimu kama vile chakula, elimu kwa
watoto, matibabu n.k kutokana na watafutaji (breadwinners) kushikiliwa
vizuizini kwa muda mrefu.
Matatizo yaliyopo
Ukamataji unaofanywa na vyombo
vya dola hususan jeshi la polisi mara nyingi unakiuka haki za binadamu kwani
tafiti zinaonyesha kwamba kumekuwepo na matumizi ya nguvu kupita kiasi dhidi ya
watuhumiwa, ambapo huambatana na vitendo vya utesaji wa watuhumiwa. Utesaji huo
hufanywa wakati wa mahojiano (interrogation) kwa lengo la kuwashinikiza
watuhumiwa kukiri makosa. Takwimu za tafiti zilizofanywa na Tume nyakati
tofauti zinaonyesha pia kwamba yapo malalamiko mengi yanayopokelewa kutoka kwa
watuhumiwa na wafungwa wanaolalamikia kubambikiwa kesi na polisi.
Aidha, kuna mapungufu katika
mfumo wa sheria za jinai nchini Tanzania. Mathalani, ingawa Ibara ya 13(6)(e)
ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano ya mwaka 1977 inakataza utesaji kwa watuhumiwa
na kuelekeza mamlaka za nchi kutunga sheria kwa minajili hiyo, bado kuna
upungufu katika sheria kwani Kifungu cha 29 cha Sheria ya Ushahidi, Sura ya 6
ya Sheria za Tanzania kinakataza ushahidi uliopatikana kwa shinikizo la aina
yoyote kutumika kama ushahidi halali mbele ya mahakama.
Hivyo, mapungufu yanayojitokeza
ni kwamba Sheria za nchi zinakataza vitendo vya utesaji kwa watuhumiwa wa
uhalifu lakini hazitamki wazi ni hatua gani zitachukuliwa dhidi ya mtumishi wa
chombo cha dola ambaye atajihusisha na vitendo vya utesaji wa watuhumiwa. Nafuu
(remedy) pekee ya kisheria inayopatikana
ni muathirika (victim) kufungua kesi ya madai dhidi ya serikali. Kwa upande
mwingine, Sheria ya Kukazia Haki na Wajibu (Basic
Rights and Duties Enforcement Act) ya mwaka 1994 nayo pia changamoto kwani
ili kesi inahyohusu ukiukwaji wa haki za binadamu isikilizwe, linahitajika jopo
la majaji watatu wa Mahakama Kuu. Katika mazingira ya sasa, upatikanaji wa jopo
hilo ni mgumu kutokana na upungufu wa maji.
Tatizo jingine kubwa katika
ukamataji, ushikiliaji watuhumiwa vituo vya polisi na kabla ya kesi kusikilizwa
ni uelewa mdogo wa sheria, kanuni na taratibu zinazohusiana na haki za binadamu katika mfumo wa haki-jinai.
Kufuatia matatizo yaliyobainishwa
hapo juu (matatizo katika ukamataji na ushikiliaji wa watuhumiwa katika mahabusu
zilizoko katika vituo vya polisi na sehemu nyingine wanamoshikiliwa watuhumiwa
kabla ya kushtakiwa), Tume ya Afrika ya Haki za Binadamu na Watu (African
Commission on Human and Peoples Rights - ACHPR) ilianzisha mchakato wa kuandaa Miongozo
(Guidelines) ya namna ya kukuza na kulinda haki za binadamu nyakati za
kukamatwa kwa watuhumiwa, kuwekwa ndani ya selo za polisi na wakiwa mahabusu za
magereza.
Miongozo hii iliridhiwa katika
Mkutano Mkuu wa 55 wa Tume hiyo uliofanyika Luanda, Angola Mei, 2014 na hivyo
kujulikana kama “Luanda Guidelines.” Luanda Guideline ziliandaliwa kwa mujibu
wa Ibara ya 45(1)(b) ya Mkataba wa Afrika wa Haki za Binadamu na Watu (African
Charter on Human and People Rights) wa mwaka 1981.
Aidha, katika kutekeleza jukumu
tajwa na mchakato uliopitishwa na ACHPR,
Miongozo imeanza kufanyiwa kazi kwa kuitambulisha kwa nchi wanachama wa Umoja
wa Nchi Huru za Afrika (AU) ili kuijua na kisha kurekebisha taratibu, kanuni na
sheria za jinai za nchi husika ili ziendane na miongozo tajwa.
Tanzania ni miongoni mwa nchi
tano (5) za mwanzo Afrika zilizopewa kipaumbele katika utekelezaji wa miongozo
hiyo ambayo itapelekea maboresho ya mfumo wake wa haki-jinai. Nchi nyingine
zilizopewa kipaumbele sambamba na Tanzania ni Zimbabwe, Malawi, Tunisia na
Ivory Coast.
Mwelekeo
THBUB kwa kushirikiana na African
Policing Civilian Oversight Forum – APCOF, Tume ya Afrika ya Haki za Binadamu
na Watu (ACHPR) pamoja na wadau wengine ndani ya serikali na asasi zisizo za
serikali imeanza mchakato wa kuhamasisha utekelezaji wa Luanda Guideline
hapa nchini. Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP), Ofisi ya Kanda ya
Afrika ndilo linalofadhili mchakato huu kwa sasa.
Mchakato bado upo katika hatua za
awali ikiwa ni pamoja na kuandaa Mpango-Kazi wa Utekelezaji, kubaini taasisi
zitakazo husika na utekelezaji huo na muda wa utekelezaji wa Luanda Guidelines.
Hata hivyo, zoezi la kutambulisha
miongozo hii limekwishaanza tangu mwishoni mwa mwezi uliopita kwa warsha
iliyowashirikisha wadau mbalimbali wa hapa nchini. Katika warsha hiyo ya siku
mbili wadau walipata fursa ya kutoa mawazo yao juu ya Mpango-Kazi wa Utekelezaji
wa miongozo hii. Na kwa kupitia kwenu tunatarajia wadau na wananchi wengi zaidi
watapata taarifa juu ya miongozo hii - tunaomba ushirikiano wenu.
Hatua zitakazofuata hapo baadaye
zitajumuisha kufanya mapitio ya sheria za jinai zinazohusiana na ukamataji na
ushikiliaji wa watuhumiwa na kubainisha mapungufu yaliyomo na kisha kuzifanyia
marekebisho sheria hizo ili zikidhi viwango vilivyoainishwa katika Luanda Guidelines.
Pale ambapo mapungufu yatabainika
kuwepo katika utekelezaji, sheria zitungwe au kurekebishwa ili kuwabana watendaji
wa vyombo vya dola wanaokiuka sheria na miongozo ya kazi zao.
Kwa ujumla utekelezaji wa dhati wa
sheria zilizopo au zitakazofanyiwa marekebisho au zitakazotungwa upya utasaidia
kuimarisha utawala wa sheria, utu wa mtu, uhuru binafsi wa mtu, amani na utulivu
nchini.
Tanzania ni mwanachama wa Umoja
wa Afrika na imeridhia Mkataba wa Afrika wa Haki za Binadamu na Watu (African
Charter on Human and Peoples Rights). Kwa kuridhia mkataba huo, Tanzania
inapaswa kutekeleza Haki za Binadamu kama zilivyoainishwa katika Mkataba huo
pamoja na miongozo mingine ya Haki za Binadamu
ambayo imebuniwa kwa mujibu wa Mkataba huo.
ACHPR imepewa mamlaka ya
kusimamia haki za binadamu barani Afrika kama zilivyoainishwa katika Mkataba.
Ili kufanikisha majukumu yake,
ACHPR imekuwa ikishirikiana na Taasisi za Kitaifa za Haki za Binadamu kama vile
Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora kwa upande wa Tanzania. THBUB ina
hadhi ya mwanachama shirikishi (affiliate member) katika ACHPR.
THBUB inatoa wito kwa wadau
kuonesha ushirikiano ili tuwe na mifumo mizuri itakayoimarisha haki za binadamu
nchini Tanzania.
Pamoja
tunaweza, tekeleza wajibu wako, tulete maboresho katika mfumo wa haki-jinai
nchini.



No comments:
Post a Comment