Mnamo mwezi wa
Machi 2014, Serikali ilipokea taarifa kutoka Shirika la Afya Duniani (WHO)
kuhusu mlipuko wa ugonjwa wa Ebola uliotokea katika nchi za Afrika Magharibi. Ugonjwa huu ulianzia katika Nchi ya Guinea na
kusambaa katika nchi za Liberia, Siera Leone na Nigeria. Aidha Ugonjwa huu
umeshatolewa tarifa pia nchini Senegal na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo
(DRC). Hadi kufikia tarehe 18 Septemba 2014, dadi ya watu waliothibitishwa
kuambukizwa ugonjwa huu imefikia 5335 na vifo 2662 (CFR=48.9%).
Aidha, hadi
kufikia tarehe 16 Septemba 2014, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) idadi
ya wagonjwa imefikia 71 na vifo 40.
Hali hii
imepelekea Shirika la Afya Duniani (WHO) kuutangaza ugonjwa wa Ebola kuwa janga
la Dunia (Public Health Emegency of International Concern).
Ugonjwa wa Ebola
husababishwa na virusi vya Ebola. Virusi hivi
vipo katika kundi la Familia ya “Filovirus”. Kuna aina tano (5) za “species”
za virusi hivi yaani Bundibugyo, Côte
d’Ivoire, Reston, Sudan na Zaïre. Aidha inakadiriwa kuwa asilimia 25 hadi 90
ya waliopata maambukizo ya ugonjwa huu, hufariki dunia. Mlipuko uilotokea nchi
za Afrika Magharibi umesababishwa na kirusi aina ya Zaire Kwa kawaida virusi hivi hubebwa na popo na uambukizo wa
kwanza kabla ya kuenea kwa binadamu huanzia kwa wanyama hususan nyani na sokwe.
Binadamu hupata uambukizo kupitia popo au kupitia wanyama
(sokwe, nyani na swala wa porini) ambao wameambukizwa au waliokufa wakati wa
shghuli za uwindaji. Mara binadamu anapopata uambukizo huu, anaweza kueneza kutoka
kwa mtu mmoja kwenda kwa mtu mwingine kupitia njia zifuatazo;
o kugusa damu au majimaji kutoka mwilini mwa mtu aliyeambukizwa ugonjwa huo
o kugusa maiti ya mtu au mzoga wa mnyama aliyekufa kutokana na ugonjwa huu.
Dalili za
awali ni homa kali ya ghafla, kulegea
mwili, maumivu ya misuli, kuumwa na kichwa, na kutokwa na vidonda kooni. Mara
nyingi dalili hizi hufuatiwa na kutapika, kuharisha,kutokwa na vipele vya
ngozi, figo na ini kushindwa kufanya kazi na kwa baadhi ya wagonjwa hutokwa
damu ndani na nje ya mwili. Kipindi kati ya kupata maambukizi mpaka kuonekana
kwa dalili za ugonjwa ni kati ya siku 2 hadi 21. Ugonjwa wa Ebola hauna Tiba maalum wala chanjo. Hata hivyo mgonjwa
anatibiwa kutegemeana na dalili atakazokuwa nazo.
Hadi sasa hakuna
mgonjwa yoyote aliyehisiwa au kuthibitishwa kuwa na virusi vya Ebola hapa
nchini. Kumekuwa na tetesi za wagonjwa wanne (4) kutoka mkoa wa
Dar es salaam (2), mmoja (Nkasi) na mmoja (Geita) waliohisiwa kuwa na ugonjwa
wa Ebola, lakini vipimo vimethibitisha kuwa HAWANA UGONJWA HUO. Kwa kuwa magonjwa hayatambui mipaka ya nchi,
Serikali inaendelea kuchukua hatua za tahadhari dhidi ya Ugonjwa huu.
Hatua ambazo zinaendelea kuchukuliwa na Serikali ni
pamoja na;
1. Uratibu: Uratibu wa shughuli unasimamiwa na Ofisi ya Waziri Mkuu –Kitengo cha Maafa. Aidha
sekta ya afya ndio msimamizi wa wa ugonjwa huu kwa kuwa maambukizi yako kwa
binadamu. Kikosi kazi hukutana kila wiki siku ya alhamisi kufanya tathmini ya
hali ya ugonjwa katika nchi zilizoathirika pamoja na mikakati iliyowekwa
kitaifa. Vikao hivi vinasimamiwa na viongozi wa ngazi za Juu ikiwemo mawaziri
na vinajumuisha sekta mbalimbali pamoja na wadau wa maendeleo. Mpango kazi
umeendelea kuboreshwa kufuatia mwongozo wa Shirika la Afya Duniani na
kusambazwa mikoani na wilayani. AIdha kiasi cha Tshs500,000,000 zimeshapokelewa
Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii na
zinategemea kutekeleza yafuatayo;
-
Uimarishaji wa sehemu ya
kuwahudumia wagonjwa kwa mkoa wa Dar es salaam “Isolation Unit” iliyopo katika
eneo la hospital ya Temeke
-
Uendelezaji wa usambazaji
wa elimu, tarifa na habari kwa jamii kutumia mabango, vipeperushi, radio,
runinga, na meseji kwa njia ya simu
-
Ununuaji wa vifaa cha
kupimia joto (Thermoscanners) kwenye maeneo ya mipakani na viwanja vya ndege
-
Mafunzo kwa watumishi wa
afya
o
Katika uratibu vilevile, mnamo tarehe 9 Septemba 2014, Mheshimiwa Rais, Dkt
Jakaya Mrisho Kikwete alishiriki katika
ukaguzi wa hatua zilizofanyika na kufanya majadiliano na kikosi kazi ya namna
ya kuboresha baadhi ya mikakati iliyowekwa.
o
Aidha viongozi wa juu wa
Serikali wakiwemo makatibu wakuu na mawaziri wamekuwa wanahudhuria mikutano
mbalimbali ya kanda (Regional body
meetings) kama mikutano ya “Africa Union”, “SADC” na “EAC” ikiwa ni katika
kupanga na kuweka maazimio ya pamoja kudhibiti ugonjwa huu barani Afrika
2. Kuimarisha ufuatitiaji katika
viwanja vya ndege na mipakani: Serikali imeshaweka
vifaa vya kuchunguza wageni wanaoingia nchini “Walk
through Thermoscanners” kwenye viwanja vya ndege na mipakani kama uwanja wa
ndege wa Julius Nyerere, KIA, Mbeya, na Mwanza, na mipaka ya Namanga, Kabanga
na Zanzibar. Aidha katika maeneo ya
mipaka ya Holili, Sirari, Kasumulo, Mutukula na Pemba pia zimewekwa “Hand Thermoscanners”. Vifaa hivi si kwa
ajili ya kutambua iwapo mgonjwa ana ugonjwa wa Ebola bali vinalenga kurahisisha
utambuzi wa wasafiri watakaokuwa wanarudi na kuwa na dalili za mwanzo ambayo ni
Homa. Fomu maalum za kuhoji wasafiri zinaendelea kutumika kwa wasafiri
wanaobainika kuwa na ugonjwa huu. Orodha ya abiria kwenye ndege (Passenger
manifest) pia inaendelea kutumika ikishirikisha maafisa wa Uhamiaji
lengo likiwa ni kutambua kwa urahisi wasafiri ambao wamepitia nchi
zilizoathirika. Ili wasafiri waweze
kutambua kuwa kutakuwa na utarabu tajwa, mabango ya maelekezo yameandaliwa kuwekwa
kwenye maeneo ya kuwasili (Arrival) na kutokea (Departure).
3. Utoaji wa Elimu, Taarifa
na Habari kwa jamii: Serikali imeendelea kutoa
elimu kupitia njia nyingine zaidi ya redio na runinga. Aidha waandishi wa
Habari walipewa semina kuhusu ugonjwa wa Ebola.. Vilevile, Asasi ya TAYOA
imekubali kuchangia utumiaji wa mpango wa “toll
free numbers” ambazo tayari zinatumika kwa ugonjwa wa UKIMWI na zitaanza kutumika pia kwa ugonjwa wa Ebola ili jamii
iweze kupata ufafanuzi zaidi ya ugonjwa huu pindi itakapohitajika. Namba hiyo
ya “Toll free number” ni 117 na itaanza kutumika punde kuanzia saa sita mchana
na saa sita usiku kupata taarifa za ugonjwa wa Ebola.
4. Ufuatiliaji wa magonjwa
katika vituo vya afya: Kupitia ofisi ya
Waziri Mkuu TAMISEMI, Serikali imetoa maagizo kwa Makatibu Tawala na Waganga
wakuu wa mikoa wakati wa mkutano wa Waganga wakuu Septemba 2014, kuandaa mpango
kazi wa namna ya kukabiliana na ugonjwa huu na kuandaa sehemu ya kutolea matibabu
kwa wagonjwa watakaohisiwa kuwa na ugonjwa huu (Isolation Units). Kikosi kazi kitafanya
ufuatiliaji wa karibu wa Agizo katika mikoa na wilaya.
5. Mafunzo kwa watumishi wa
Afya: Mafunzo yameendelea kutolewa kwa watumishi wa viwanja
vya ndege, mipakani na vituo vya kutoa huduma za afya pamoja na Maafisa wa
Idara ya Uhamiaji yalifanyika Agosti 2014 kwa kushirikiana na ufadhili wa
Shirika la Afya Duniani (WHO). Idadi ya watumishi waliokwisha kupata mafunzo ni;
·
100
kutoka Dar es salaam
·
45
kutoka mkoani Arusha, Kagera, Rukwa, Mwanza, Kilimanjaro, na Kigoma na Zanzibar
o
Wizara
pia imepata nafasi ya kupeleka watumishi watatu (3) nchini Congo Brazaville; watano
(5) nchini Afrika kusini na wanne (4) nchini Uganda kwa lengo la kujifunza
kutoka nchi nyingine na pia kuboresha mpango mkakati ambao umeshaandaliwa.
o
Wizara
kwa kushirikana na TAMISEMI inaendelea kutoa mafunzo kwa watumishi wa afya
kuanzia ngazi ya chini mpaka ya juu.
6. Vifaa vya kujikinga
(Personal Protective Gears): Vifaa kinga vipo vya
kutosha kwa ajili ya matumizi kwa watoa huduma kwa wagonjwa. Jumla ya vifaa vya
kujikinga (Personal Protective Gears) 12,750 vimenunuliwa na kuanza kusambazwa
katika hospital za wilaya, mkoa na rufaa. Tunatarajia kupata vifaa vingine
kutoka Shirika la Afya Duniani (WHO) na Shirka la Afya la Marekani (CDC). Aidha
idadi hii itaongezwa kadiri ya mahitaji yatakavyojitokeza.
7. Maeneo ya kutolea huduma
za afya kwa watakaobanika na ugonjwa: Wizara
imebainisha vituo vya kutolea huduma kwa mikoa yote endapo ugonjwa huu utatokea
hapa nchini.. Katika mkoa wa Dar es salaam, Temeke Isolation Unit limetengwa
kama eneo la kuwahudumia wagonjwa wa Ebola kwa mkoa huu. Sehemu hii inaendelea
kuboreshwa kwa kuzingatia vigezo maalum ili iweze kukidhi matibabu ya Ugonjwa
huu. Aidha SUMA JKT wamepewa kazi ya ukarabati wa majengo na kazi hii
imeshaanza kufanyika.
8. Kuweka mkakati wa namna
ugonjwa huu utakavyoweza kutambulika mapema: Mipango ya awali ni kutumia maabara ya KEMRI, Nairobi kwa sasa wakati
uboreshaji wa maabara zetu unaendelea ili kupata ithibati na kuweza kufanya
utambuzi hapa nchini.
9. Wizara inaendelea
kuwasiliana na wadau mbalimbali ikiwemo wadau wa maendeleo ili kuweza kupata msaada wa mahitaji mbalimbali kama yalivyoainishwa
kwenye mpango wa dharura wa kukabiliana na ugonjwa wa Ebola. Aidha mkutano wa
pamoja wa wadau unaandaliwa mwezi Septemba 2014 ambapo utasimamiwa na Ofisi ya
Waziri Mkuu..
10. Kupeleka wataalamu wa
afya katika nchi zilizoathirika. Serikali
itapeleka wataalam 9 katika nchi zilizoathirika ikiwa ni kwa ajili ya kujenga
uwezo wa wataalam wetu hapa nchini. . Aidha upelekaji wa wataalam hawa unalenga
pia kuimarisha dhana ya kusaidiana kama ambavyo Baba wa Taifa alivyokuwa
anafanya miaka ya nyuma wakati wa kudai uhuru katika Bara la Afrika.
Hitimisho
Wizara inapenda kuwatoa hofu wananchi kuwa hadi sasa
hakuna mgonjwa yeyote aliyethibitishwa kuwa na virusi vya ugonjwa Ebola hapa
nchini.
Wananchi
wanashauriwa kutokuwa na hofu ila kuendelea kuchukua tahadhari. Ugonjwa wa Ebola unaweza kuzuilika.
Njia kuu za kujikinga na ugonjwa huu ni:-
o
Kuepuka kugusa au
kuingiwa na mate, damu, mkojo, jasho, kinyesi, machozi na majimaji mengine yanayotoka mwilini kwa mgonjwa mwenye dalili za
ugonjwa wa Ebola Kuhakikisha kuwa
unanawa mikono kwa maji na sabuni au kwa kutumia kwa dawa ya kuua vijidudu
(hand sanitizers)
o
Kuepuka
kushughulikia maiti ya mtu aliyekufa akiwa na dalili za ugonjwa wa
Ebola; badala yake watoe taarifa kwa uongozi wa kituo cha kutolea huduma za
Afya kwa ushauri. Wataalam watasimamia maziko ikiwa itatokea.
o
Wananchi waepuke mila na
desturi zinazoweza kuchelewesha kupata
huduma muhimu na kuzidi kueneza ugonjwa wa Ebola.
o
Kutoa taarifa mapema kwa
viongozi wa Serikali na watoa huduma za
Afya katika ngazi zote pale anapotokea mtu mwenye dalili za ugonjwa wa Ebola.
o
Kuwahi katika vituo vya
kutolea huduma za Afya pale mtu
anapohisiwa kuwa na dalili za ugonjwa
huu.
Wizara itaendelea na utaratibu wa kupashana habari na
taarifa hizi kila wiki kuanzia leo tarehe 18.9.2014 ikiwa ni lengo la
kushirikisha jamii ili iweze kushiriki
katka utekelezaji wa mikakati ya kudhibiti ugonjwa huu usiingie nchini.
Imetolewa na
Kitengo cha Mawasiliano Serikalini
Tarehe 18 Septemba 2014
No comments:
Post a Comment