Frank Mvungi-Maelezo
SERIKALI imewataka wananchi kujihadhari na makampuni yanayojiingiza
katika kazi za upimaji ardhi au uthamini bila ya kusajiliwa na bodi au Halmashauri zenye mamlaka ya
kusimamia taaluma husika.
Hayo yamesemwa jana, jijini Dar es Salaam na Mkurugenzi wa
Upimaji na Ramani wa Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi bw.Justo
Lyamuya wakati wa mkutano na waandishi wa habari uliolenga kutoa utaratibu
unaotakiwa kufuatwa na wananchi katika upimaji ardhi.
“Hadi sasa wapima ardhi waliosajiliwa ni 290 wakati
makampuni yaliyosajiliwa na Baraza la Taifa la wapima na wathamini ardhi ni 58”
hivyo hakuna haja ya wananchi kutapeliwa na vishoka. Alisema Bw. Lyamuya.
Akifafanua Lyamuya amesema kuwa ni vyema wananchi wakatumia
makampuni yaliyosajiliwa kufanya kazi ya kupima ardhi ili kuepuka migogoro
ambayo kwa kiasi kikubwa inachangiwa na ukiukwakwaji wa sheria na taratibu za
upimaji ardhi.
Akifafanua kuhusu wathamini (valuers) Lyamuya amesema hadi
sasa wataalamu waliosajiliwa ni 320 na makampuni yalisajiliwa na Baraza ni 54.
Pia Lyamuya alisema kuwa kazi za upimaji viwanja
zitakazowasilishwa Wizarani ambazo hazikufuata taratibu na kwa mujibu wa sheria
ya upimaji Ardhi sura 324 ya mwaka 1957 hazitapokelewa.
Pia mambo yanayopaswa kuzingatiwa katika upimaji wa ardhi
(mashamba na viwanja) lyamuya amesema upimaji usiozingatia ushirikishwaji na
kutambua mipaka kwa maridhiano hautapokelewa.
Aidha makampuni ya upimaji yanayowasilisha kazi za upimaji
kwa Mkurugenzi waUpimaji na Ramani ambazo hawakuzisimamia wao wenyewe au
wawakilishi wao na kudhibitika kazi hizo hazitapokelewa na kwa mujibu wa sheria
za kusajili makampuni ya upimaji Na.2 ya mwaka 1977 yataadhibiwa ikiwa ni
pamoja na kusimamishwa.
Halmashuri ya Taifa ya wapima Ardhi ni chombo cha Serikali
kilichoundwa kwa mujibu wa sheria Na.2 ya mwaka 1977, Jukumu kubwa la chombo
hiki ni kufanya usajili wa wataalam wapima Ardhi,kusimamia weledi wa taaluma na
mwenendo wa utendaji katika masuala ya kupima ardhi (Land Survey) kuthamini
mali (property valuation) na kuendeleza ardhi (estate management).
No comments:
Post a Comment