TANGAZO


Sunday, September 14, 2014

MKALA: Kuzinduliwa utaratibu wa kuwa na muuzaji mkuu wa dawa mkoani Dodoma kutaboresha upatikanaji wa dawa kwenye vituo vya Afya



Naibu Waziri wa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, Mhe. Dkt. Kebwe Stephen Kebwe akiwahutubia wadau mbalimbali waliohudhuria sherehe ya Uzinduzi Uboreshaji wa Mfumo wa Upatikanaji wa Dawa naVifaa Tiba kupitia Mzabuni mmoja Mkoa wa Dodoma. (Pichana Benedict Liwenga, Maelezo-Dodoma)

Na Benedict Liwenga, MAELEZO-Dodoma.
HIVI karibuni Mkoa wa Dodoma umezindua mradi wa kusambaza vifaa tiba na dawa katika Hospitali na vituo vya afya katika Wilaya saba mkoani humo.
 
Hatua hiyo ililenga kukabiliana na upungufu na dawa na vifaa tiba katika Hospitali mbalimbali ili kuboresha afya za wananchi kwa kuwahakikishia upatikanaji wa huduma za tiba zilizobora na za uhakika.
Uhaba wa dawa ni changamoto inayokwamisha utoaji wa huduma bora katika vituo vingi vya afya ambapo watumiaji wa huduma katika vituo hivyo hudhania huduma ya afya waipatayo kuwa ni duni kutokana na kutopatikana kwa madawa na hivyo kuwalazimu kupata dawa hizo kutoka sehemu zingine.

Ili kuboresha upatikanaji wa madawa, wilaya Saba za mkoa wa Dodoma pamoja na viongozi wa mkoa kwa msaada wa mradi wa Health Promotion and System Strengthening (HPSS) waliamua kukabiliana kutafua ufumbuzi na tatizo la upungufu wa dawa na vifaa tiba  kwa kutumia mbinu ya ushirikiano na sekta binafsi yaani (Public-Private Partnership -PPP).
Kufuatia uzinduzi huo hivi sasa, Wilaya Saba za mkoa wa Dodoma zinaweza kuagiza dawa na vifaa tiba kwa kutumia mfumo wa utaratibu wa kupitia kwa muuzaji mkuu mmoja ambaye ni Duka la Bahari Limited .
 
Utaratibu huo wa kuwa na muuzaji mkuu ni mfumo uliotokana na mradi wa HPSS ambao pia unajulikana kama ‘Tuimarishe Afya Project’. Mradi huu ni sehemu ya ushirikiano kati ya Serikali ya Uswisi na Tanzania katika kuleta maendeleo na kuboresha afya za wananchi.
Akiongea wakati wa Uzinduzi wa Mfumo wa uboreshaji na kusaidia upatikanaji wa Dawa na Vifaa Tiba kupitia Mzabuni mmoja Mkoani Dodoma, Naibu Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Mhe. Dkt. Steven Kebwe alisema kuwa mfumo huo ni mzuri na utakuwa shirikishi kwani utahakikisha kuwa jamii inapata mahitaji sahihi ya dawa na pia watumishi wa sekta ya afya wanafanya kazi kwa bidii kwa lengo la kupambana na magonjwa nchini.
“Mifumo hii itatusaidia na kuboresha mahitaji ya dawa katika vituo vya afya, na hivyo kupunguza vifo mbalimbali vinavyotokana na wananchi kutumia dawa na tiba ambazo sio sahihi kwa sababu ya kukosa dawa katika vituo vya afya”, alisema Mhe. Kebwe.
 
Alisema kuwa, wananchi wanapokwenda katika vituo vya afya wanapenda wakute huduma nzuri na za kuridhisha huku wakipata dawa na huduma nyingine za upimaji kwa gharama nafuu.
Aliongeza kuwa mfumo huo utasaidia wananchi kuwa na imani na huduma watakazokuwa wakipata kwa sababu ya uwepo wa dawa za kutosha na vifaa tiba.
 
“Kama mpango huu mtautekeleza vizuri, utasaidia kujenga imani kwa wananchi juu ya huduma mbalimbali mnazitoa na hivyo kuondoa manung’uniko ambayo yamekuwa yakijitokeza kwa sababu ya wananchi kukosa huduma kwa sababu ya ukosefu wa dawa na vifaa tiba” alisisitiza Naibu Waziri huyo.
 
Alisema kuwa mpango huu unatekeleza mikakati ya Serikali ya kusogeza huduma za afya kwa wananchi kwa kuboresha upatikanaji wa dawa na vifaa tiba.
Hivyo Mhe. Dkt. Kebwe aliziagiza Wilaya zote za Mkoa wa Dodoma kuhakikisha zinatekeleza mfumo kwa ufanisi ili mikoa mingine ije kujifunza kutoka kwao kwa ajili ya kusaidia kupunguza upungufu wa dawa na vifaa vya tiba hapa nchini.
Aidha, Mhe. Dkt. Kebwe amefafanua kuwa, sasa hivi wameamua kuja na mfumo huo kwa kuwa utasaidia sana kuboresha afya za wananchi na kutekeleza malengo ya Milenia. 
Aliongeza kuwa Serikali itaendelea kujipanga zaidi katika kufundisha na kuelekeza watumishi na kutengeneza mifumo mipya kwa ajili ya  kusogeza huduma karibu na wananchi kulingana na bajeti.
Aidha , alisema kuwa kwa kuwa Mkoa wa Dodoma ndio umekuwa wa kwanza kutekeleza mradi huu ni vema wakautekeleza kwa ufanisi wa hali ya juu ili mikoa mingine ije kujifunza kutoka kwao.
Naye Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Dkt. Rehema Nchimbi aliishukuru Serikali ya Uswisi kwa msaada mkubwa  kwa Tanzania hasa mkoani Dodoma katika Wilaya husika kwani utasaidia kuboresha afya za wakazi wa Dodoma.
Dkt. Nchimbi aliongeza kuwa mfumo huo utasimamia na kutekelezwa kama ilivyopangwa ili mikoa mingine ipate kuja kujifunza kupitia mkoa wa Dodoma.
“Naomba Mhe. Mgeni rasmi wakati tunasherehekea Uzinduzi huu, tuombe tupate mwongozo kwa udhibiti wa dawa zinazosambaa kwa kasi kupitia vyombo vya habari”, alisema Mhe. Nchimbi.
Mfumo huo utatoa fursa kwa Duka la Dawa la Bahari Limited kuzindua mfumo wa usambazaji wa dawa na vifaa tiba katika vituo vya afya na Hospitali katika Wilaya zote saba za mkoa wa Dodoma.
Akiongea kama mmoja wa viongozi wa kikosikazi cha mradi huo, Profesa Meshack alisema kuwa tayari Kampuni binafsi ya Bahari Limited imeshachaguliwa kwa njia ya mchakato wa zabuni ambapo kampuni hiyo ndiyo itakayokuwa muuzaji mkuu, hivyo oda za dawa kutoka vituo vyote vya afya vya kila wilaya katika mkoa wa Dodoma zitanunuliwa kutoka kwa muuzaji mmoja yaani kutoka kwa muuzaji mkuu.
 
“Dawa hizi zitalipiwa kupitia vyanzo vya nyongeza vya fedha vya mara kwa mara kama vile mfuko wa afya wa jamii, fedha kutoka bima ya Afya, vyanzo vya ada na fedha za makusanyo mbalimbali”, alisema Profesa Meshack.
 
Akizungumzia namna ya Msambazaji wa huduma hiyo alivyochaguliwa, alisema kuwa msambazaji huyo mwenye uzoefu mzuri aliweza kuchaguliwa baada ya mchakato wa muda mrefu uliofanywa na Mamlaka ya mkoa ambapo Bahari Ltd ambaye ndiye muuzaji mkuu aliyechaguliwa tayari amekwisha saini mkataba na utawala wa mkoa wa Dodoma.
Bila shaka huu ndiyo mwanzo wa utekelezaji wa mfumo ambao unaweza kuja kuziba pengo lililopo katika upatikanaji wa madawa kwa ushirikiano na MSD ambao ndiyo wasambazaji wakuu wa madawa kwenye vituo vya afya.
 
Profesa aliongeza kuwa Kitabu cha muongozo chenye maelezo juu ya viwango na taratibu za uendeshaji wa vituo vya afya na wilaya ili kusaidia mfumo wa kuwa na muuzaji mkuu uweze kutekelezeka tayari kimekwisha tengenezwa.
 
Aidha, aliwaasa watendaji wote kuzingatia Kanuni za uendeshaji na kununua dawa za ziada kutoka kwa muuzaji mkuu wa kanda yao.
 
“Kupunguza uhaba wa madawa ya ziada, huduma nzuri za kliniki ikiwa ni pamoja na utoaji sahihi wa dawa na matumizi ya dawa kulingana na muongozo wa tiba wa taifa ni muhimu kwa ajili ya matokeo ya afya bora”, alisema Profesa Meshack
 
Akiongea kuhusu changamoto ambayo inaweza kujitokeza katika kusambaza madawa zaidi katika mfumo wa ugavi ambao unaweza kuongeza nafasi ya kuwepo kwa matumizi mabaya, aliweka bayana kuwa usimamizi na ukaguzi wa mara kwa mara utafanyika.
Naye Balozi wa Uswisi nchini Tanzania, Mhe. Balozi Olivier Chave alisema kuwa ni mara yake nyingine kufika mjini Dodoma kuja kutembelea miradi ambayo inafadhiliwa na Serikali yake ya Uswisi.
 
Balozi alieleza kuwa moja ya miradi aliyoweza kuitembelea ulikuwa ni mradi wa Promotion and System Strengthening Project ambao ulikuwa katika hatua za mwanza kabisa za utekelezaji katika kipindi hicho.
 
Balozi aliongeza kuwa mradi huo wa HPSS uliundwa kama mpango wa kina wa ngazi ya mkoa uliokusudia kuchangia katika jitihada za Wizara katika kuboresha mfumo wa afya katika Wilaya zote Saba za mkoa wa Dodoma.
 
“Mradi wa HPSS unahusisha nyanja Tatu muhimu katika kuboresha afya ya jamii ambazo ni kukuza afya, kuimarisha mfumo pamoja na utafiti wa kiutendaji”, alisema Balozi Chave.
Tukumbuke ya kuwa kusudio la mradi huu ni kuweza kuchangia katika jitihada za kuweza kufikia Malengo ya Maendeleo ya Milenia (MDGs) hasa malengo ya kupunguza idadi ya vifo vya watoto wachanga, afya ya uzazi, mapambano dhidi ya Ukimwi/VVU, Malaria, magonjwa mengine, afya ya mazingira, maji safi ya kunywa na kuboresha usafi wa mazingira.
 
Kwa upande mwingine, watoaji huduma za afya hutegemea sana upatikanaji wa dawa katika utoaji wa huduma nzuri ya afya, hivyo upatikanaji huu wa dawa utahimiza na kuipa moyo jamii hatimaye kuiwezesha kujiunga na huduma ya mfuko wa afya wa jamii (CHF).
Akifafanua kuhusu upembuzi yakinifu uliotolewa na mradi huo, Balozi alieleza kuwa mwaka 2010 na 2012, asilimia 53% ya upatikanaji wa dawa muhimu na asilimia 47% ya kiwango cha ukosefu wa dawa (stock-out) rate) ni changamoto kubwa katika sekta ya utoaji huduma ya afya, ambapo tofauti ya asilimia 40% inayotokana na upatikanaji wa dawa ikiwemo uhafifu, kutimizwa kwa uagizaji mpya kutoka MSD kumepelekea kuwepo na uhitaji wa kuweza kupata dawa kutoka sehemu zinginezo.
 
Licha ya vituo vya afya vingi kujitahidi kuziba pengo la kuagiza dawa kutoka vyanzo binafsi mbalimbali vilivyopo ndani na nje ya mkoa, kumekuwa na gharama kubwa za mfumo kufanya hivyo kwasababu gharama hizo zinahusisha masuala ya mengine yakiwemo gharama za usafiri, mafuta, malipo ya wanaokwenda kununua dawa hizo pamoja na bei kubwa za kununulia dawa hizo kiasi kinachopelekea kupanda kwa gharama.
Jitihada za uongozi wa mkoa wa Dodoma pamoja na uongozi wa serikali za mtaa wakishirikiana na mradi wa HPSS kwa kuanzisha mfumo wa kuwa na Muuzaji Mkuu (Prime Vendor) ni jambo la kujivunia na uwe mfano wa kuigwa kwa mikoa mengine nchini.
Mradi wa HPSS ulizinduliwa mwaka 2011 ukilenga kuusaidia mkoa wa Dodoma kwa kipindi cha miaka Kumi katika sekta ya Bima ya Afya, uboreshaji wa afya ya jamii, usimamiaji wa dawa na usimamiaji wa matengenezo ya vifaa vya afya, mradi huu umefadhiliwa na Ubalozi wa Uswisi nchini Tanzania na unatekelezwa na Shirika la The Swiss Tropical and Public Health Institute (Swiss TPH) likishirikiana na Shirika la Ujerumani la The Micro Insurance Academy (MIA) pamoja na Shirika la The Ifakara Health Institute la Tanzania.

No comments:

Post a Comment