Mjumbe Msambatavangu, akiwasilisha maoni ya Kamati yake kwenye kikao cha bunge hilo, mjini Dodoma jana.
Na Benedict Liwenga na Magreth Kinabo, Maelezo-Dodoma.
04/09/2014.
KAMATI za Bunge Maalum la Katiba leo tarehe 4
Septemba, 2014 zimeendelea kuwasilisha taarifa zao mbele ya Bunge hilo.
Baadhi ya kamati zilizowasilisha taarifa zao katika
Bunge hilo ni Kamati Namba Mbili, Kamati
Namba Tisa, Kamati na Kumi, Kamati Namba Nne, Kamati Namba 12, ambazo
ziliwasilisha asubuhi hadi mchana.
Mambo makubwa yaliyozungumzwa katika Bunge hilo
yanahusu mambo mbalimbali yakiwemo ya Uongozi wa Bunge, ambapo wengi
wapendekeza wabunge wanaweza kuchaguliwa
Spika au Naibu Spika na Mbunge
kutowajibishwa na wananchi.
Pia kigezo cha kugombea nafasi ya ubunge kikiwa
ni kujua kusoma na kuandika kwa lugha ya
Kiswahili na Kiingereza.
Katika
uwasilishaji huo, Kamati Namba Nne ya Bunge hilo, iliwasilisha taarifa yake,
ambayo ilisomwa na Gosbert Blandes, taarifa,
ambapo katika Ibara ya 132 inahusu Spika
na Mamlaka ya Spika.
Wajumbe wengi wanapendekeza ibara hiyo ifanyiwe
marekebisho kwa kumwondoa mbunge kuwa miongoni mwa watu wasioruhusiwa kushika
madaraka ya Spika.
Aidha siku za kuwasilisha tamko rasmi kuhusu mali
zimeongezwa kutoka siku thelathini hadi tisini. Ibara hiyo ndogo ya (2) sasa
itasomeka kama; (2) Waziri, Naibu Waziri, Mbunge au mtu mwenye madaraka ya aina
nyingine yoyote yatakayotajwa na sheria za nchi kwa madhumuni ya Ibara hii,
hataweza kuchaguliwa kuwa Spika.
Sababu za mapendekezo ni kumwezesha Mbunge kugombea
nafasi ya Spika na kuongeza siku za kuwasilisha tamko rasmi kuhusu mali ili
kuondoa uwezekano wa Spika kushindwa kufanya hivyo kutokana na ufinyu wa muda.
Ibara ya 133, ibara hii inahusu ukomo wa Spika. Baada
ya mjadala Wajumbe walio wengi walipendekeza kufanya marekebisho kwa kufuta aya
ya (a) linaloweka sharti la kukoma kwa nafasi yake kutokana na kuchaguliwa kuwa
mbunge. Sababu za mapendekezo haya ni kutoa fursa kwa wabunge kushika madaraka
ya Spika na kuendelea kushikilia nafasi zao za ubunge.
Ibara ya 134, ibara hii inahusu Naibu Spika. Kamati
imejadili kwa kina ibara hii kasha wajumbe walio wengi walikuwa na mapendekezo
kuwa ibara ifanyiwe marekebisho kwa kuondoa neno Mbunge katika Ibara ndogo ya
(2). Ibara hiyo sasa itasomeka kama ifuatavyo; 134 (2) Waziri, Naibu Waziri au
mtu mwenye madaraka ya aina nyingine yoyote yatakayotajwa na sheria za nchi kwa
madhumuni ya Ibara hii, hataweza kuchaguliwa kuwa Naibu Spika. Sababu za
mapendekezo haya ni kuwawezesha Wabunge kuwa na sifa ya kuchaguliwa kuwa Spika.
Ibara ya 135,
Ibara hii inahusu sifa za mtu kuchaguliwa kuwa Spika au Naibu Spika. Kamati
imejadili kwa kina kuhusu sifa za mtu kuchaguliwa kuwa Spika au Naibu Spika.
Baada ya mjadala wajumbe walio wengi walipendekeza kuifanyia marekebisho ibara
hii. Lengo la marekebisho haya ni kutoa wigo mpana kwa watu wenye sifa za
kuchaguliwa kuwa wabunge kuwa na haki ya kuchaguliwa kuwa Spika na Naibu Spika
ilimradi wana shahada ya Chuo kikuu inayotambulika. Ibara hii sasa itasomeka
kama ifuatavyo;
135 (1) (1) Mtu atastahili kuchaguliwa kuwa Spika au
Naibu Spika endapo mtu huyo ana elimu ya shahada ya chuo cha elimu ya juu
kinachotambulika kwa mujibu wa sheria za nchi; (2) Bila ya kuathiri masharti ya
ibara ndogo ya (1), mtu atastahili kuchaguliwa kuwa Spika au Naibu Spika ikiwa
ana sifa za kumwezesha kuchaguliwa kuwa mbunge.
Kamati Namba Kumi ya Bunge Maalum nayo iliwasilisha taarifa yake kuhusu sura ya Rasimu ya katiba
ya Jamhuri ya Muungano kwa sura ya tisa na sura ya kumi, ambayo ilisomwa na Dk.
Dalaly Kafumu.
Dk. Kafumu
alisema katika suala la Uchaguzi wa wabunge, Ibara ya 124(4) ya Rasimu
ya Katiba inazungumzia uchaguzi wa mbunge endapo kiti cha ubunge kipo wazi.
“Kamati yangu inaona kuwa ibara hii inalenga kufuta
uchaguzi mdogo kwa kuwa ibara hii inatoa mwanya wa mtu kuteuliwa na kutangazwa
na Tume ya Uchaguzi, kutoka kwenye orodha ya majina ya wagombea iliyowasilishwa
kwa Tume Huru ya Uchaguzi.
“Kamati yangu haikubaliani na utaratibu huo, hivyo
inapendekeza kwa utaratibu unaotoa haki ya mtu kugombea na
kuchaguliwa kama ilivyo katika ya sasa,” alisema.
Utaratibu wa kutayarisha orodha ya majina uliotajwa
katika ibara ya 124 wa kumpata mbunge haujawekwa bayana kwa maana ya kuainisha
mfumo wa uwiano wa kura na idadi ya wagombea kwani inatakiwa kuwa sawa na idadi
ya viti bungeni. Aidha, mfumo unaopendekezwa utaleta dhana ya “Mbunge
mtarajiwa” hali inayoweza kuathiri demokrasia na hata utendaji wa kazi wa
mbunge anayekuwa madarakani. Kutokana na sababu hizo, Wajumbe wamependekeza
ibara ndogo ya (4) ifanyiwe marekebisho na kusomeka; “(4) Endapo Mbunge
anayetokana na chama cha siasa atapoteza sifa za kuwa Mbunge kwa sababu yoyote
isiyokuwa ya Bunge kumaliza muda wake, Tume Huru ya Uchaguzi itatangaza
uchaguzi wa Mbunge katika Jimbo hilo, kwa mujibu wa masharti ya Katiba hii”.
Alisema katika Ibara ya 125 (1) b kuhusu sifa za
kuchaguliwa kuwa mbunge kuwa elimu isiyopungua kidato cha nne. Wajumbe walio
wengi wamekubaliana kuwa ibara hiyo ifanyiwe marekebisho kwa kuondoa kiwango
cha elimu kwa kuwa suala la kugombea nafasi yoyote ni la kidemokrasia, haipaswi
mtu kuzuiwa kugombea kwa kigezo cha elimu, kwani ni haki ya Katiba.
“Hali kadhalika, Katiba haitakiwi kuweka kigezo chochote
kinachokiuka haki za msingi za kuchaguliwa na kuchagua. Pili haki ya kuamua
kama mgombea anafaa au hafai ni ya wapiga kura,wasizuiwe kikatiba kutumia haki
yao ya msingi ya kuchagua mtu wanayemtaka. Pia utaratibu huuu haupo duniani
kote hata kwa nchi zilizona demokrasia iliyokomaa,” alisema Blandes.
Aliongeza kuwa wajumbe walipendekeza Ibara hiyo
ifanyiwe marekebisho kwa kuweka cha kujua kusoma na kuandika na si kiwango
cha elimu kama sifa ya msingi.Hivyo isomeke
ifuatavyo:
“(1) (b) Anajua kusoma na kuandika lugha ya Kiswahili
na Kiingereza.”
Aidha Dk. Kafumu aliongeza kuwa katika Ibara ya 129 kuhusu haki ya wapiga kura kumwajibisha Mbunge .
“Wajumbe wengi wamependekeza kuwa, wapiga kura watumie
haki yao ya kumwajibisha mbunge kwa njia ya kidemokrasia ya kupiga kura kila
baada ya kipindi cha miaka mitano kinapokwisha. Kamati imeona kuwa, kwa kadri
demokrasia ya vyama vingi inayoendelea kukua, upo uwezekano wa watu wachache
kuweza kutumia mbinu hasi kumuondoa mbunge anayefaa bila ya kuwa na sababu za msingi. Hivyo basi wajumbe walio
wengi wamependekeza ibara hii ifutwe yote.
Wakati kwa upande wa maoni ya walio wachache, ambayo
yalisomwa na Dk. Tulia Ackson, ambapo alisema katika Ibara 124 inayohusu uchaguzi wa wabunge , walitofautiana
na walio wengi kwa kusema kuwa inajitosheleza.
“Hii Ibara ni muhimu ibaki kama ilivyo kwani
inapunguza matumizi makubwa ya fedha ambayo yameshuhudiwa na wananchi,” alisema
Dk. Tulia.
Aliongeza kwamba
katika Ibara ya 129 walitofautiana na wajumbe wali wengi kwa kusema kuwa ibara hiyo inajitosheleza
kwani iwapa wananchi haki ya kuweza kumwajibisha mbunge ambaye hawajibiki
ipasavyo katika kuwawakilisha wananchi na kuwatafuatia wananchi ufumbuzi wa matatizo yao.
Wajumbe walio wachache walipendekeza ibara hiyo ibaki
isipokuwa irekebishwe kama ifuatavyo:
129 (1) Bila kuathiri masharti ya Katiba hii, wananchiwatakuwa
na haki ya kumwondoa Mbunge wao madarakani, endapo Mbunge atashindwa
kuwasilisha aua kutetea kwa dhati hoja zinazotokana na kero za wapiga kura
wake.
(2)Bunge litatunga sheria kuweka masharti ya kuendesha
uchunguzi kwa mbunge atakayeshindwa kutekeleza majukumu yake kwa wapiga kura
wake na utaratibu wa kumwondoa katika Ubunge.
No comments:
Post a Comment