TANGAZO


Friday, August 1, 2014

Rais Shein azindua Maonesho ya Kilimo ya Nane nane Kitaifa mkoani Lindi

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein akikata utepe kama ishara ya uzinduzi wa Maonesho ya kilimo ya nane nane kitaifa mwaka huu   katika viwanja vya Ngongo Mkoani  Lindi leo. (Picha na Ramadhan Othman Lindi)
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Ali Mohamed Shein akisalimiana na Viongozi mbali mbali wakati alipowasili katika  Viwanja vya Ngongo yanapofanyika maonesho ya Kilimo ya nane nane kitaifa Mkoani Lindi.  
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein akipata maelezo katika banda la Benki Kuu ya Tanzania BOT katika maonesho ya kilimo  ya nane nane kitaifa 
Mkoani Lindi katika viwanja vya Ngongo. 
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein akipata maelezo kutoka kwa Dk. Geoffrey Mkamito Mtafiti wa Mazao ya Mizizi, katika banda la Bodi ya Korosho katika maonesho ya kilimo ya nane nane kitaifa yanayo faanyika Mkoani Lindi katika viwanja vya Ngongo. 
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein akipata maelezo kutoka kwa Dk.Geoffrey Mkamito Mtafiti wa Mazao ya Mizizi, katika banda la Bodi ya Korosho katika maonesho ya kilimo ya Nane nane Kitaifa yanayofaanyika Mkoani Lindi katika viwanja vya Ngongo.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein akipata maelezo kutoka kwa Meneja Biashara na Masoko Numwagile A. Mwaijumba wa Shirika la Nyumbu kuhusu mashine ya utengenezaji wa matofali ya udongo katika maonesho ya kilimo ya nane nane kitaifa yanayofaanyika Mkoani Lindi katika viwanja vya Ngongo.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Ali Mohamed Shein akipata maelezo kutoka kwa Meneja Biashara na Masoko Numwagile A. Mwaijumba wa Shirika la Nyumbu kuhusu mashine ya utengenezaji wa matofali ya udongo katika maonesho ya kilimo ya nane nane kitaifa yanayofaanyika Mkoani Lindi katika viwanja vya Ngongo.

Na Mwandishi wetu, Lindi
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein ametoa wito kwa viongozi na wataalamu kuhakikisha kuwa matokeo ya tafiti zinazofanywa zinawafikia walengwa kwa muda muafaka ili matokeo hayo yaweze kuleta manufaa yaliyokusudiwa.
Wito huo ameutoa leo wakati uzinduzi wa wiki ya maadhimisho ya sikukuu ya wakulima (Nanenane) yanayofanyika kitaifa katika viwanja vya maonesho ya Kilimo Ngogo nje kidogo mwa mji wa Lindi.
Alisema kuwa matokeo ya tafiti za kilimo na mifugo yanayooneshwa katika maonesho hayo hayana budi kufikishwa kwa wakulima, wafugaji na wavuvi ili yaweze kutumika kuimarisha shughuli zao.
Alisisitiza kuwa utafiti ni suala la msingi katika maendeleo ya taifa hivyo kauli mbiu ya maadhimisho hayo Matokeo Makubwa Sasa, Kilimo ni Biashara utekelezaji wake hauna budi uzingatie umuhimu wa utafiti katika sekta za kilimo, mifugo na uvuvi ili kuzifanyia kazi changamoto zinazoweza kukwamisha kufikia lengo la kaulimbiu hiyo.
Dk. Shein aliwaeleza mamia ya wananchi waliohudhuria uzinduzi huo kuwa maeonesho hayo yanatoa fursa kwa wahusika katika sekta hizo kuanzia wataalamu, wakulima, wafugaji, wavuvi pamoja na wadau wengine kubadilishana uzoefu na utaalamu ikiwemo tekinolojia na mbinu za kisasa za katika sekta hiyo.
Kwa hivyo alisema hiyo ni fursa adhimu ya kuonesha mafanikio na kujifunza na hatimae kuongeza ufanisi katika kuimarisha ukuaji wa sekta hizo ambazo ni muhimu kwa maendeleo ya taifa.
Dk. Shein alibainisha kuwa kwa Tanzania Bara sekta ya kilimo  inachangia asilimia 24.5 ya pato la taifa na kutoa ajira kwa asilimia 80 na asilimia 30 ya mapato ya fedha za kigeni wakati kwa upande wa Zanzibar inachangia asilimia 30.1 ya pato la taifa na kutoa ajira kwa asilimia 70 na mapato ya fedha za kigeni asilimia 19.6.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi amesifu jitihada kubwa zinazofanywa na wakulima, wafugaji na wavuvi wa Tanzania na kueleza kuwa maonesho hayo yanadhihirisha jitihada zao hizo katika kuzalisha chakula na malighafi zinazotumiwa na viwanda humu nchini.
Halikadhalika ameeleza kuridhishwa kwake na kazi zinazofanywa na watafiti nchini na kutumia fursa hiyo kuwapongeza kwa kazi nzuri waifanyayo ambayo imechangia kuongeza tija katika kilimo, ufugaji na uvuvi.
Kwa hiyo ametoa wito kwa wakulima, wafugaji na wavuvi kuendelea kutumia vyema ushauri wa kitaalamu katika kufanya shughuli zao kwani kufanya hivyo watakuwa sio tu kuwa wameonesha thamani ya kazi za kitafti wa wataalamu wetu bali pia kuongeza kipato chao na kuinua uchumi wa taifa.
Katika hotuba yake hiyo alihimiza pia wakulima na wafugaji kuzingatia ubora wa mazao na mifugo yao kwa kuwa hicho ndicho kigezo muhimu katika kufikia bei ya kuuza na kununua.
Alisisitiza kuwa mifugo ni rasilimali muhimu na kubwa kwa taifa na ambayo inaweza kuchangia kwa kiasi kikubwa katika kupiga vita umasikini endapo wafugaji watazingatia miongozo na kanuni bora za ufugaji.
Dk. Shein aliwahakikishia wananchi kuwa lengo la Serikali za Jamhuri ya  Muungano wa Tanzania na ile ya Mapinduzi  Zanzibar ni kuona wakulima na wafugaji wanaishi maisha bora na wanachangia katika suala zima la kuwa na masiha bora jkwa kila mtanzania.
Alitoa mfano kuwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia programu mbalimbali ukiwemo Mkakati na Programu ya Kuendeleza Sekta ya Kilimo ili kuleta mabadiliko katika sekta ya kilimo nchini.
Katika mnasaba huo aliwataka viongozi na wataalamu wa kilimo na mifugo nchini kuitekeleza progamu hiyo kwa makini na kwa ufanisi kufikia malengo ya programu hiyo.
Alikumbusha na kusisitiza pia umuhimu wa wakulima kupatiwa elimu ya kutosha ya hifadhi na utunzaji wa mazingira hasa kwa kuzingatia matatizo yanayotokana na mabadiliko ya tabia nchi yanayoathiri shughuli za uchumi ikiwemo kilimo na ufugaji.
Wakati huo huo Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk Ali Mohamed Shein ametoa wito kwa vyombo vya habari kuwahamasisha wakulima, wafugaji na wananchi kwa ujumla kufika katika maonesho hayo ili kujionea mafanikio na kujifunza mambo mbalimbali yatakayoweza kuwasaidia kuendeleza shughuli zao.
Kabla ya kuzindua rasmi maadhimisho hayo Dk. Shein ambaye alikuwa amefuatana na mawaziri wa serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mpinduzi ya Zanzibar alipata fursa ya kutembelea mabanda mbalimbali katika manesho hayo.

No comments:

Post a Comment