TANGAZO


Friday, August 15, 2014

Mashabiki kukata kiu cha ligi ya EPL





Hatimaye kiu cha mashabiki wa soka hususan Ligi kuu ya England kitaanza kukatwa wikendi hii pale Ligi hiyo maarufu kaka EPL, itakapoanza rasmi kutimua vumbi katika msimu huu wa 2014/2015.
Kuondoka kwa Luis Suarez,na kuwasili kwa Luis Van Gaal,na kurejea kwa Cesc Fabregas safari hii akiwa Stamford Bridge,na uchawi wa Diego Costa bila shaka ni baadhi ya mambo yanayotaraji kuteka hisia za mashabiki wa soka kila pembe ya Dunia hususan wale manazi wa Ligi kuu ya kandanda nchini England.
Huu ni wakati ambao kwa wale mashabiki wa soka hasa wa timu kubwa Liverpool,Manchester United ,Arsenal,Chelsea na Man City watakapokuwa matumbo joto kwa kufuatilia mechi zinazohusu timu zao.
'Liverpool'


Katika usajili wake Meneja wa Liverpool Brendan Rogers amemsajili mlinzi Dejan Lovren
Baada ya kuishia kunawa katika mechi tatu za mwisho msimu uliopita, Liverpool hadi sasa imekwishasajili wachezaji wanane wapya ikiwa ni kujiandaa kwa msimu mpya ambapo pia itashiriki michuano ya Ligi ya Mabingwa barani Ulaya huku wakiwa na kikosi kipana kilichosheheni nyota kadhaa mahiri katika usakataji kabumbu.
Katika usajili wake Meneja wa Liverpool Brendan Rogers amewasajili mlinzi Dejan Lovren, Kiungo Adam Lalana, na mshambuliaji Rickie Lambert.
Wote hao kutoka Southampton, huku akiwasajili kiungo Emre Can, na mshambuliaji wa pembeni Lazar Markovic na sasa ameimarisha tena idara ya ulinzi kwa kumleta Beki wa Pembeni Alberto Moreno kutoka Sevilla ya Uhispania ili kuimarisha mapengo yaliyojitokeza msimu uliopita.
Ingawa inaaminika kuwa Pengo la Luis Suarez litakuwa gumu kuzibika hasa kutokana na kiwango alichokionyesha msimu uliopita pale alipoweza kutupia kambani bao 30
'Arsenal'


Arsenal imemsajili winga machachari wa Chile Alexis Sanchez
Nayo Arsenal baada ya ukame wa miaka mingi hatimaye ndani ya miezi mitatu imekwishaanza kuzoa mataji mawili baada ya kutwaa kombe la FA majuzi iliopowachapa Mabingwa watetezi Man City bao 3-0 katika mechi ya ngao ya jamii kufungua pazia la msimu huu unaoanza.
Bila shaka mashabiki wa Arsenal watakuwa wanasubiri kwa hamu kuona iwapo timu hiyo itaendeleza moto huo pamoja na kumpoteza mlinzi wake Thomas Vermaelen aliyejiunga na Barcelona na Bacary Sagna aliyetimkia Man City ,lakini wamemsajili winger machachari wa Chile Alexis Sanchez,Mathieu Debuchy wa Ufaransa,na mlinzi Calum Chambers ili kuimarisha kikosi cha timu hiyo almaaruf the Gunners.
'Manchester united'


Kocha mpya Van Gaal anatarajiwa na wengi kurejesha moto wa kabumbu katika klabu ya Man u
Kwa upande wake Manchester United baada ya kutepeta msimu uliopita imeanza kwa kupata kocha mpya mwenye rekodi ya mafanikio Mholanzi Luis Van Gaal,huku pia ikimsajili Kiungo Ander Herrera na Mlinzi kinda wa pembeni Luke Shaw ambao wanataraji kushirikiana na wakongwe waliosalia kwenye timu hiyo.
Ingawa bado usajili unaweza kufanyika katika wiki tatu zijazo kabla ya kufungwa dirisha la usajili huku akiwa tayari ameshashinda mechi mbili za kujiandaa na msimu kwa kuilaza Liverpool na Valencia matokeo ambayo yamewapa matumaini makubwa mashabiki wa Timu hiyo maarufu kama mashetani wekundu.
'Chelsea'


Didier Drogba atachezea Chelesea licha ya wnegi kusema kuw aumri wake umesonga mno
Naye Kocha Jose Mourinho akiwa na kikosi kilichozidi kuongezewa ubora kwa kuwasajili Diego Costa na Cesc Fabregas,anataraji kuwa na kikosi kamili msimu huu ambapo pia amemrejesha mkongwe Didier Drogba licha ya kuwa umri wake umesonga mbele.
'Manchester City'
Nao mabingwa watetezi Manchester City wakiwa wameimarisha idara ya ulinzi kwa kuwasajili Mlinzi ghali Eliaquim Mangala kutoka Porto na Bacary Sagna kutoka Arsenal msimu huu watakabiliana na changamoto kubwa ya kuhakikisha kuwa wanatetea Ubingwa wao,huku wakiwa wamemuazima Kwa muda Kiungo wa zamani wa Chelsea Frank Lampard
'Timu nyinginezo'
Ingawa Timu kubwa kubwa ndizo zinatajwa sana,lakini Everton,Tottenham Hotspurs, na Swansea nazo huenda zikatoa changamoto katika mbio za kuwania Ubingwa huo wa Ligi kuu England.
Aidha mashabiki wa soka watakuwa wakifuatilia kuona Southampton itakabiliana vipi na timu pinzani hasa baada ya kuondokewa na nyota wake watano bila shaka ambao wameuzwa katika timu kubwa na Liverpool,Man United na Arsenal.
Huu ni msimu mpya utakaokamilika mwezi May mwakani ambapo Idhaa ya Kiswahili ya BBC kupitia Ulimwengu wa soka itakuwa hewani kila Jumamosi na Jumapili kukuletea moja kwa moja mechi hizo kupitia Radio washirika.

No comments:

Post a Comment