TANGAZO


Wednesday, July 9, 2014

Maafisa wa usalama watimuliwa Somalia



Hii ni mara ya pili kwa Ikulu ya Rais kushambuliwa Somalia
Baadhi ya polisi na maafisa wa ujasusi nchini Somalia, wameachishwa kazi kufuatia shambulizi dhidi ya Ikulu ya Rais katika mji mkuu Mogadishu.
Taarifa hii ni kwa mujibu wa waziri wa habari.
Waliopigwa kalamu ni pamoja na Abdihakim Saaid na Bashir Gobe. Nyadhifa zao zimechukuliwa na maafisa wengine wakuu.
Mashabulizi hayo yalifanywa na wapiganaji wa Al Shabaab ambao walishambulia Ikulu hiyo iliyokuwa na ulinzi mkali mnamo siku ya Jumanne kwa kutegua bomu lililokuwa limetegwa ndani ya gari.
Wanajeshi wa serikali kwa ushirikiano na vikosi vya Muungano wa Afrika walifanikiwa kuwadhibiti washambuliaji hao, watatu kati yao wakiuawa na mwingine mmoja kukamatwa.
Shambulizi hilo ni la pili dhidi ya Ikulu ya Rais mwaka huu kufanywa na Al Shabaab.
Rais Hassan Sheikh Mohamud, hakuwepo katika Ikulu hiyo wakati wa mashambulizi.
Wanamgambo ambao walidai kuwaua wanajeshi 14 wameahidi kuzidisha mashambulizi wakati huu wa mwezi Mtukufu wa Ramadhan.
Hata hivyo maafisa wa serikali walikanusha madai kuwa wanajeshi wa serikali waliuawa wakati wa mashambulizi hayo.

No comments:

Post a Comment