TANGAZO


Tuesday, July 8, 2014

Kimbunga chawahamisha maelfu Japan


Serikali ya Japan imewashauri karibu watu nusu milioni kuhama makwao na kutafuta hifadhi kwengineko wakati kimbunga kwa jina Neoguri kikipiga visiwa vilivyo kusini mwa nchi hiyo.
Upepo unaovuma kwa kasi ya zaidi ya kilomita 200 kwa saa umeripotiwa kwenye visiwa vya Okinawa. Upepo huo umeambatana na gharika.
Shirika la utabiri wa hali ya hewa limeonya kuwa eneo hilo litakabiliwa na mawimbi makali ya bahari yenye urefu wa hadi mita 14.
Mwandishi wa BBC mjini Tokyo anasema kuwa nguvu za kimbunga hicho zinapungua lakini mvua kubwa huenda ikasababisha mafuriko na maporomoko ya udongo.
Safari za ndege zimesitishwa huku maelfu ya nyumba zikibaki bila umeme. Marekani tayari imeamuru ndege zake katika kambi ya kijeshi iliyoko Okinawa kuondolewa mara moja.
Maafisa wakuu wamewataka wakazi 480,000 kusalia nyumbani au wahame na kwenda maeneo ya nyanda za juu.
Polisi mjini Okinawa wanasema kuwa watu 3 akiwemo mwanamke mwenye umri wa miaka 83 walijeruhiwa. Mvuvi mmoja pia ameripotiwa kutoweka asijulikane aliko.
Kuna tisho la mawimbi makali na mvua kubwa. ''Tafadhali mjizuie kuondoka nje,'' shirika la utabiri wa hali hewa liliwashauri wananchi.
Zaidi ya watu 50,000 waliripotiwa kukosa umeme na maji huku shughuli za kiwanda kikubwa cha mafuta zikisitishwa.
Maafisa wakuu nchini China na Taiwan wamewashauri mabaharia pia kujizuia kufanya safari za baharini.

No comments:

Post a Comment